Kabla
hatujaangalia dhana ya mtindo ni vema tukajua kwanza dhana ya fasihi.
Wataalamu
wengi akiwamo Wamitila (2003) wanakubaliana
kuwa fasihi ni sanaa inayotumia lugha na ambayo hujishughulisha na binadamu
pamoja na maisha yake na huathiri, hugusa, au huacha athari fulani na
hupatikana katika umbo ambalo linatambuliwa na jamii. Kwa ujumla fasihi ni
sanaa inayotumia lugha na yenye maudhui katika jamii husika.
Baada
ya kuangalia dhana ya fasihi kwa ujumla sasa tuangalie dhana ya mtindo na
nafasi yake katika fasihi.
Senkoro
(1982) anasema mtindo katika kazi ya fasihi ni ile namna ambayo msanii hutunga
kazi hiyo na kuipa sura ambayo kifani na kimaudhui huainisha kanuni au kawaida
zilizofuatwa (za kimapokeo) ama ni za kipekee. Anaendelea kusema, mtindo ni
upangaji wa fani na maudhui katika kazi ya fasihi kwa njia ambayo hutokeza au
huonyesha nafsi na labda upekee wa mtungaji wa kazi hiyo.
Katika
fasili hii tunaweza kuona anachokieleza mtaalamu huyu ni kwamba mtindo huhusisha
upangaji wa fani na maudhui katika kazi ya fasihi ambapo upangaji huu hutegemea
upekee alionao msanii. Kwa maana nyingine, unaposoma kazi fulani ya fasihi
unaweza kumwona mtunzi wa kazi hiyo kulingana na jinsi alivyoiandika, kwa maana
kwamba jambo moja linaweza kuongelewa na wasanii wawili tofauti lakini namna
linavyowasilishwa likatofautiana, na hii ni kulingana na upekee wao.
Wamitlia
(2003) naye anasema ‘mtindo ni jumla ya mbinu au sifa zinazomwezesha mwandishi
kuwasilisha ujumbe wake, huelezea mwandishi
anavyounda kazi yake’. Anaendelea kusema, dhana ya mtindo hurejelea sifa
maalumu za mwandishi au mazoea ya mwandishi fulani ambayo hujionyesha kwenye
fani yake, mazoea hayo ya mwandishi ya kuandika, kuteua msamiati, tamathali za
semi, taswira, uakifishi, sentensi na kadhalika ndio yanayompambanua mwandishi
huyu na mwanzake.
Kitu
anachokisema hapa Wamitila hakitofautiani na Senkoro, kinachoongelewa hapa ni
upekee wa mwandishi husika lakini Wamitila kasema kitu kimoja zaidi, kwamba msanii anaonekana kuwa na mtindo fulani
kwa sababu amezoea kutunga kazi zake za fasihi kwa namna fulani ambayo
inadhihirisha upekee wake. Kwa kauli hii ya Wamitila tunaweza kusema kwamba
mtindo wa mtunzi huonekana baada ya kuandika kazi zake kadhaa na kimsingi hii
ndio huleta maana halisi ya mazoea.
Nakubaliana
na kauli hii, kwani hata hivyo huwezi ukahitimisha kuwa mtunzi fulani mtindo
wake ni huu kama umesoma kazi yake moja tu, kwa hiyo mtindo (upekee) wa
mwandishi huweza kubainishwa baada ya kupitia kazi zake kadhaa na ndipo
tunaweza kuona mazoea ya mwandishi huyo katika kuandika kazi zake.
Kwa
sentensi fupi tunaweza kusema kuwa
mtindo ni ule upekee alionao mtunzi wa kazi ya fasihi katika kuipa kazi yake
sura fulani kifani na kimaudhui ambapo mtunzi mwingine hawezi kufanya hivyo
hata kama kitu kinachoongelewa ni kilekile.
Sasa
mtu anaweza kujiuliza, nitawezaje kubainisha mtindo wa mtunzi katika kazi ya
fasihi? Swali hili linaweza kujibiwa kwa kuangalia vipengele fulanifulani.
Tunapotaka
kujua mtindo wa msanii katika kazi husika, kwa mfano katika riwaya tunaangalia vipengele vifuatavyo:
- Matumizi ya lugha; je, lugha ni rahisi au ngumu, je kuna matumizi ya maneno ya kiufundi na kadhalika
- Matumizi ya daiolojia; je, ni kwa kiasi gani mtunzi ametumia dailojia, ni kwa kiasi gani daiolojia husimulia hadithi?
- Namna ya usimulizi; je, anatumia nafsi ya kwanza, ya pili au ya tatu na kadhalika.
- Ukuaji wa wahusika; kwa vipi mtunzi anawatambulisha wahusika na kwa vipi wanabadilika katika hadithi.
- Hisia za mwandishi; je hisia zake zinaonekanaje katika hadithi? Je, anaonekana ni mwenye dhihaka? Mwenye mapenzi, mwenye matumaini, mkali, mwenye kejeli na kadhalika.
- Namna anavyopanga sura au matukio katika hadithi. Je, sura ni fupifupi au ndefu? Ni nyingi kiasi gani, zimepangwaje? Na kwa nini imepangwa hivyo?
- Tamathali za semi; je, mwandishi katumia kwa kiasi gani tashibiha, sitiari, tashihisi au alama?
- Mandhari; je mandhari yaliyotumika ni halisi au ya kubuni?
- Uteuzi wa msamiati; je, ni kwa jinsi gani msamiati uliotumika unaleta mvuto kwa msomaji.
Kwa
ujumla hivi ni baadhi tu ya vipengele
vya mtindo vinavyoweza kujitokeza katika
riwaya.
Baada
ya kuangalia dhana ya mtindo ni vema sasa tukaangalia nafasi yake katika
fasihi. Kwa ujumla mtindo una nafasi kubwa tu katika kazi ya fasihi.
Mtindo
humtambulisha mtunzi wa kazi ya fasihi; watu hupenda kazi ya mtunzi fulani kwa
sababu mtindo anaoutumia huwavutia wasomaji wake.
Mtindo
ndicho kipengele kinachotenganisha kazi
nyingine za kisayansi au za kawaida, bila mtindo kazi za kifasihi zisingepata
mashabiki wengi. Kwa hiyo mtindo ndio huibua hisia na kuwafanya wasomaji
wapende zaidi kusoma kazi za msanii husika.
Kwa
hiyo tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa, tunapozungumzia dhana ya mtindo
tunakuwa tunarejelea mwandishi husika, kwa maana kwamba ubinafsi wake ndicho
kile kinachoonekana kwenye kazi yake. Tunaposema hadithi fulani ina taswira
nyingi, ina sitiari nyingi au lugha yake ni rahisi au lugha yake inavutia na
kadhalika tunakuwa tunarejelea mtindo wa mtunzi husika. Kwa mantiki hiyo dhana
ya mtindo kama ilivyokwisha jadiliwa inaonekana kwa namna mtunzi anavyopangilia
kazi yake kifani na kimaudhui, yaani namna anavyotumia lugha, anavyopanga visa
na matukio, uteuzi wa mandhari, falsafa anayoiwasilisha,ujumbe dhamira na
kadhalika.
Marejeo
Senkoro,
F.E.M.K (1982) Fasihi. Dar es salaam: Press and Publicity Centre.
Wamitila,
K.W. (2003) Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Naiobi: Focus Publishers.
25 comments:
Kazi nzuri
Kazi hii ni safi sana imenifaa katika uchunguzi wangu.
Kazi hii ni safi sana imenifaa katika uchunguzi wangu.
Kazi nzuri, mtindo wa MTU ni sawa anavyovalia
Kazi nadhifu
Sadakta.inamanufa
Kazi mahiri
Kazi nzuri, imenifaa sana
Kazi nzuri..imenifaa katika utafiti wangu
Mitindo gani imetumika katika riwaya ya Rosa misitika?? Samahani kwa anaejua anisaidie
Kazi nzuri
Kazi murwa
Kazi murwa ,, nzuri kabisa
Kazi nzur inatusudia sis tunaojifunza fasihi
Kazi safi kabisa
Kazi nzuri sana imenifaa sana
Jadili jinsi dhana ya mtindo ni tata kuifasili
Nmefurahikia kazi hii! Hongera
Ni kazi nzuri kulingana na Mimi @Ssempala madan
Naomba msaada wa swali hili "fasihi ni sanaa kama zilivyo sanaa nyingine lakini inajipambanua kwa namna yake.jadili kauli hiyo
Kazi ni nzuri Tena sana
Kazi nzuri sana
Mbn hamna marejeleo??
Kazi nzur meipenda
Inajipambanua kwasabab ya vipengele vifuatavy
1-muundo wake
2-mtindo wake
3-matumiz yak ya lugha
4-wahusika wak
5-uwasilishaji wak
6-Wahusika wak
Post a Comment