Kabla hatujaangalia
dhana ya mtindo ni vema tukajua kwanza dhana ya fasihi.
Wataalamu wengi akiwamo Wamitila (2003) wanakubaliana kuwa
fasihi ni sanaa inayotumia lugha na ambayo hujishughulisha na binadamu pamoja
na maisha yake na huathiri, hugusa, au huacha athari Fulani na hupatikana
katika umbo ambalo linatambuliwa na jamii. Kwa ujumla fasihi ni sanaa
inayotumia lugha na yenye maudhui katika jamii husika.
Baada ya kuangalia
dhana ya fasihi kwa ujumla sasa tuangalie dhana ya mtindo na nafasi yake katika
fasihi.
Senkoro (1982) anasema
mtindo katika kazi ya fasihi ni ile namna ambayo msanii hutunga kazi hiyo na
huipa sura ambayo kifani na kimaudhui huainisha kanuni au kawaida zilizofuatwa
(za kimapokeo) ama ni za kipekee. Anaendele kusema, mtindo ni upangaji wa fani
na maudhui katika kazi ya fasihi kwa njia ambayo hutokeza au huonyesha nafsi na
labda upekee wa mtungaji wa kazi hiyo.
Katika fasili hii
tunaweza kuona anachokieleza mtaalamu huyu ni kwamba mtindo huhusiha upangaji
wa fani na maudhui katika kazi ya fasihi ambapo upangaji huu hutegemea upekee
alionao msanii. Kwa maana nyingine, unaposoma kazi Fulani ya fasihi unaweza
kumwona mtunzi wa kazi hiyo kulingana na jinsi alivyoiandika, kwa maana kwamba
jambo moja linaweza kuongelewa na wasanii wawili tofauti lakini namna
linavyowasilishwa likatofautiana na hii ni kulingana na upekee wao.
Wamitlia (2003) naye
anasema “mtindo ni jumla ya mbinu au sifa zinazomwezesha mwandishi kuwasilisha
ujumbe wake. Huelezea mwandishi
anavyounda kazi yake “. Anaendelea kusema, dhana ya mtindo hurejelea sifa
maalumu za mwandishi au mazoea ya mwandishi Fulani ambayo hujionyesha kwenye
fani yake, mazoea hayo ya mwandishi ya kuandika, kuteua msamiati, tamathali za
semi, taswira, uakifishi, sentensi na kadhalika ndio yanayompambanua mwandishi
huyu na mwanzake.
Kitu anachokisema hapa Wamitila hakitofautiani na Senkoro, kinachoongelewa hapa ni upekee wa mwandishi husika lakini Wamitila kasema kitu kimoja zaidi ambacho naonekana Senkoro hakukiweka bayana, kwamba msanii anaonekana kuwa na mtindo Fulani kwa sababu amezoea kutungakazi zake za fasihi kwa namna Fulani ambayo inadhihirisha upekee wake. Kwa kauli hii ya Wamitila tunaweza kusema kwamba mtindo wa mtunzi huonekana baada ya kuandika kazi zake kadhaa na kimsingi hii ndio huleta maana halisi ya mazoea.
Nakubaliana na kauli
hii kwani hata hivyo huwezi ukahitimisha kuwa mtunzi Fulani mtindo wake ni huu
kama umesoma kazi yake moja tu, kwa hiyo mtindo (upekee) wa mwandishi huweza
kubainishwa baada ya kupitia kazi zake kadhaa.
Kwa sentensi fupi tunaweza kusema kuwa mtindo ni
ule upekee alionao mtunzi wa kazi ya fasihi katika kuipa kazi yake sura Fulani
kifani na kimaudhui ambapo mtunzi mwingine hawezi kufanya hivyo hata kama kitu
kinachoongelewa ni kilekile.
Sasa mtu anaweza
kujiuliza, nitawezaje kubainisha mtindo wa mtunzi katika kazi ya fasihi? Swali
hili linaweza kujibiwa kwa kuangalia vipengele fulanifulani.
Tunapotaka kujua mtindo
wa msanii katika kazi husika hususani riwaya tunaangalia vipengele vifuatavyo:
- Matumizi ya lugha; je, lugha ni rahisi au ngumu, je kuna matumizi ya maneno ya kiufundi na kadhalika.
- Matumizi ya daiolojia; je, ni kwa kiasi gani mtunzi ametumia dailojia, ni kwa kiasi gani daiolojia husimulia hadithi?
- Namna ya usimulizi; je, anatumia nafsi ya kwanza ya pili au ya tatu na kadhalika.
- Ukuaji wa wahusika; kwa vipi mtunzi anawatambulisha wahusika na kwa vipi wanabadilika katika hadithi.
- Hisia za mwandishi; je hisia zake zinaonekanaje katika hadithi? Je, anaonekana ni mwenye dhihaka? Mwenye mapenzi, mwenye matumaini, mkali, mwenye kejeli na kadhalika.
- Namana anavyopanga sura au matukio katika hadithi. Je, sura ni fupifupi au ndefu? Ni nyingi kiasi gani, zimepangwaje? Na kwa nini imepangwa hivyo?.
- Tamathali za semi; je, mwandishi katumia kwa kiasi gani tashibiha, sitiari, tashihisi au alama?
- Mandhari; je mandhari yaliyotumika ni halisi au ya kubuni?
- Uteuzi wa msamiati; je, ni kwa jinsi gani msamiati uliotumika unaleta mvuto kwa msomaji.
Kwa ujumla hivi ni
baadhi tu ya vipengele vya mtindo
vinavyoweza kujitokeza katika riwaya.
Baada ya kuangalia
dhana ya mtindo ni vema sasa tukaangalia nafasi yake katika fasihi. Kwa ujumla
mtindo una nafasi kubwa tu katika kazi ya fasihi.
Mtindo humtambulisha
mtunzi wa kazi ya fasihi; watu hupenda kazi ya msanii fulani kwa sababu mtindo
anaoutumia huwavutia wasomaji wake.
Mtindo ndicho kipengele
kinachotenganisha kazi nyingine za
kisayansi au za kawaida, bila mtindo kazi za kifasihi zisingepata mashabiki
wengi. Kwa hiyo mtindo ndio huibua hisia na kuwafanya wapende zaidi kusoma kazi
za msanii husika.
Kwa hiyo tunaweza
kuhitimisha kwa kusema kuwa, tunapozungumzia dhana ya mtindo tunakuwa
tunarejelea mwandishi husika, kwa maana kwamba ubinafsi wake ndicho kile
kinachoonekana kwenye kazi yake. Kwa hiyo tunaposema hadithi Fulani ina taswira
nyingi, ina sitiari nyingi au lugha yake ni rahisi au lugha yake inavutia na
kadhalika tunakuwa tunarejelea mtindo wa mtunzi husika. Kwa mantiki hiyo dhana
ya mtindo kama ilivyokwisha jadiliwa inaonekana kwa namna mtunzi anavyopangilia
kazi yake kifani na kimaudhui, yaani namna anavyotumia lugha, anavyopanga visa
na matukio, uteuzi wa mandhari, falsafa anayoiwasilisha,ujumbe dhamira na
kadhalika.
Marejeo
Senkoro, F.E.M.K (1982)
Fasihi. Dar es salaam: Press and Publicity Centre.
Wamitila, K.W. (2003)
Kichocheo cha Fasihi Simulizi na Andishi. Naiobi: Focus Publishers.
http:// teachers.lakesideschool.org/us/ErikChristensen/WRITING%20STRATEGIES/literarystyle.htm
http://
lisakoski.hubpages.com/hub/Writing-styles-of-English-Literature.htm
No comments:
Post a Comment