MAENDELEO YA KISWAHILI
KATIKA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO (TEHAMA)
Aritamba Malagira
Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam
Ikisiri
Teknolojia ya habari na mawasiliano imekuwa ikikua kila siku
kutoka simu ya kukoroga hadi simu ya mkononi, matumizi ya wavuti na nyinginezo
nyingi, kwa kweli ni hatua kubwa ya maendeleo katika teknolojia. Hivi sasa watu
wanawasiliana ndani ya sekunde chache kwa umbali wa kutoka bara hadi bara
kupitia wavuti. Katika hali kama hii lugha za ulimwengu nazo zimekuwa
zikijitahidi kukabiliana na ukuaji huu wa teknolojia kwa kutafuta istilahi mpya
ili kuelezea dhana mpya za kiteknolojia zinazoibuka. Katika harakati hizi,
Kiswahili hakiko nyuma, istilahi mpya za Kiswahili zimekuwa zikiundwa ili
kukidhi haja ya kuwasiliana kupitia Teknolojia ya habari na mawasiliano. Makala
hii inalenga kuangalia hatua iliyofikiwa na Kiswahili katika tasnia ya
teknolojia ya habari na mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuchunguza istilahi za
ki-TEHAMA zinazotumika.
1.
Utangulizi
Teknolojia
ya habari na mawasiliano imekuwa kiungo muhimu sana katika maendeleo ya watu
duniani. Watu wamekuwa wakitumia teknolojia hii katika kufanya mawasiliano
muhimu, kufanya bishara na mambo mengine mengi yanayowanufaisha watu. Kompyuta/
Talakirishi ni moja ya kifaa kilicholeta mapinduzi katika TEHAMA kama asemavyo
Katambi (2011) “Kompyuta ama Tarakilishi
katika lugha ya Kiswahili ni kifaa ambacho kimebadilisha kabisa mfumo wa
maisha ya binadamu katika miongo takribani sita iliyopita. Kutokana na kuwapo
kifaa hiki dunia imejikuta katika maendeleo makubwa kabisa kuliko kipindi
chochote kile katika historia ya kuwapo kwake. Kifaa hiki kimeleta mabadiliko
makubwa Sana katika maisha ya kawaida ya binadamu. Kifaa hiki kimesababisha
mambo mengi kufanyika katika hali ambayo hakika isingewezekana au ambayo awali
ingeonekana kama ya kufikirika!. Kompyuta imeyafanya maisha kuwa rahisi zaidi.
Kompyuta imeifanya dunia kuwa Kama kijiji kidogo ambacho unaweza kukizunguka
katika muda mfupi Sana wa sekunde chache”. Maneno haya ya Katambi yanaonesha ni
jinsi gani kompyuta ilivyo muhimi katika TEHAMA, mawasiliano yote ya teknolojia
ya habari hufanywa kwa kutumia kompyuta, mfano; matangazo ya redio na
televisheni, magazeti na n.k huandaliwa
kwa kutumia kompyuta na kuwa tayari kwa ajili ya kupasha habari.
Makala hii, kwa kuzingatia umuhimu wa
TEHAMA katika dunia ya sasa imejikita katika kuchunguza maendeleo ya Kiswahili
katika uga wa habari na mawasiliano kwa umahususi zaidi katika mawasiliano
yanayohusisha matumizi ya kompyuta hususani wavuti na programu nyingine za kompyuta.
Tutaangalia umuhimu wa matumizi ya Kiswahili katika TEHAMA, maendeleo
yaliyofikiwa, changamoto na mwisho ni hitimisho.
2.
Usuli
Neno Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA) kwa ujumla wake hurejelea mifumo yote ya kiteknolojia
inayotumika kutengeneza, kuhifahdi, kuchakata na kutumia habari katika mifumo
yake tofautitofauti (data, picha, uwasilishaji wa medianuwai na mifumo mingine
mingi) na mabayo huwezesha, kurahisha na kutegemeza mawasiliano. Kwa umahususi
zaidi, TEHAMA inarejelea kukutana au kuingiliana kwa mikroelektroniki, talakirishi na mawasiliano ya kutumia redio, simu au
televisheni ambavyo hufanya kuwezekana kwa data, ikiwa ni pamoja na matini,
video na ishara za video kuweza kusafirishwa mahali popote duniani ambapo
ishara za kidijitali huweza kupokelewa… (Howell na Lundall, wakinukuliwa na
Akinyi 2010). Kwa ujumla TEHAMA inahusu mambo mengi sana, matumizi ya kompyuta,
wavuti, matangazo ya redio na televisheni, satelaiti, picha na mambo mengine
mengi yafananayo na hayo hujumuishwa katika teknolojia ya habari na
mawasiliano.
2.1 Umuhimu wa
TEHAMA katika maendeleo kwa ujumla
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
kwa ujumla imechangia sehemu kubwa kuleta maendeleo hasa katika kipindi hiki
cha karne ya 21 ambapo utandawazi umeenea ulimwengu mzima na kuifanya dunia
kuwa kama kijiji ambapo watu huwasiliana na kufanya kazi na biashara kwa pamoja
kama wapo katika kijiji kimoja, mambo haya yote yanafanikiwa kwa kuwezeshwa na
TEHAMA. Kama asemavyo Kamau (2009) kuwa ushirikiano wa kimataifa katika mambo
kama vile siasa, biashara, uchumi , michezo n.k
huwezeshwa na kurahisishwa na teknolojia ya habari na mawasiliano
(TEHAMA) ambayo imeuunganisha ulimwengu mzima kimawasiliano. Kwa maelezo haya tunaweza kuona ni jinsi gani TEHAMA
ilivyo kuwa muhimu katika ulimwengu wa sasa.
Lugha ni muhimu sana katika suala zima
la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano hatuwezi kuhamisha maarifa yaliyopo
katika teknolojia hii bila kutumia lugha na kwa hiyo ili kuwapo na maendeleo
endelevu kupitia TEHAMA ni lazima pia lugha inayotumika kuhamisha maarifa ya
teknolojia hii iwe inaleweka kwa watumiaji husika. Hii itakuwa rahisi kwao
kuilewa na kuitumia teknolojia hii vilivyo kwa sababu lugha inayotumika ni
lugha wanayoifahamu na ni lugha yao.
Kama tujuavyo bara la Afrika
halijaendelea sana kwa kiwango cha kuzalisha teknolojia zitakazo kubalika
katika masoko ya kimataifa kama yafanyavyo mabara mengine hususani mabara ya
Ulaya na Marekani, kwa hiyo kulingana na hali hii Afrika imekuwa ikiingiza
teknolojia za kigeni kutoka Mabara mengine hasa Marekani na Ulaya, teknolojia
hizi zimekuwa zikiingizwa kwa lugha za kigeni jambo ambalo hufanya watumiaji
wengi wa Waafrika kushindwa kumudu matumizi ya teknolojia hizi kwa sababu
hawajui lugha iliyotumiwa. Kwa mfano kompyuta zinazoingizwa Afrika programu
zake huwa zimeandikwa kwa lugha za kigeni hususani kiingereza, watu mabao
wataweza kuzitumia kwa urahisi ni wale ambao wanazijua lugha hizi vilivyo na
kuwaacha wale wasiojua wakiwa wameduwaa ambao kimsingi ni wengi kuliko wale
wanaojua. Kwa hiyo, ili kuondokana na tatizo hili, upo umuhimu mkubwa wa kuziendeleza
lugha za Kiafrika kiteknolojia. Suala hili ni la msingi sana, kwani kwa kufanya
hivi hatutakuwa tumeendeleza lugha tu bali pia tutakuwa tumeindeleza jamii yetu
kiteknolojia.
2.2 Kwa nini Kiswahili katika TEHAMA
Wataalam wengi wanipigia upatu lugha
ya Kiswahili kuwa lugha ya utandawazi barani Afrika, hii ni kwa sababu lugha ya
Kiswahili imeendelea sana kuliko lugha nyingine za Kiafrika na ndiyo lugha
pekee iliyoonekana kuwa tayari kupokea kwa haraka mabadiliko ya kiteknolojia
yanayoibuka kila siku duniani. Kwa maana kwamba lugha ya Kiswahili ina utajiri
mwingi wa msamiati kiasi cha kukabiliana na teknolojia za kigeni zinazoibuka
bila matatizo yoyote. Kama asemavyo Kamau (2009) “kwa vile utandawazi huhusika
na uunganishaji wa mataifa mbalimbali, basi Afrika yahitaji lugha moja yenye
asili ya Kiafrika kama lugha ya kusambaza utandawazi. Kwa sasa mfano mzuri wa
lugha kama hii ni lugha ya Kiswahili. Lugha hii ndio lugha kutoka barani Afrika
ambayo ina matumizi mapana kuliko lugha nyingine hapa barani na kwingineko”.
Nukuu hii inatuonesha ni jinsi gani lugha ya Kiswahili ilivyo muafaka katika
suala zima la utandawazi wa Afrika. Kimsingi utandawazi husambazwa kupitia
lugha na teknolojia, kwa hiyo tunaweza kuona jinsi lugha ilivyo chombo muhimu
sana katika maendeleo ya teknolojia na kwahiyo Kiswahili kama lugha ya kiafrika
ni muhimu iwe imejiendeleza na kujitosheleza kiteknolojia kwaajili ya mahitaji
ya watu wake.
Kutokana na umuhimu wa TEHAMA kama
ilivyofafanuliwa hapo juu na kutokana na
umuhimu wa lugha katika maendeleo ya kiteknolojia, tunaweza kuona jukumu
la lugha ya Kiswahili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Lugha ya
Kiswahili imebeba jukumu kubwa la kuhakikisha wakazi wa Afrika Mashariki
wanaipata na kuitumia teknolojia mpya kwa lugha wanayoifahamu ambayo ni
Kiswahili. Kwa kufanya hivi matumizi ya teknolojia yataimarika katika ukanda
huu wa Afrika Mashariki. Kwa misingi hii naweza kusema ndio sababu pekee
iliyonisukuma kuichunguza lugha ya Kiswahili katika uwanja wa Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano.
3.
Hatua iliyofikiwa na lugha ya Kiswahili katika
TEHAMA
Kwa kweli lugha ya Kiswahili imepiga
hatuta kubwa sana katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Kama tulivyo
kwisha kusema huko awali kwamba TEHAMA ina uwanja mpana sana, tunapozungumzia
TEHAMA tunazungumzia vitu vingi sana kama vile matangazo ya redio na
televisheni kwa namna yanavyofanywa, matumizi ya kopmyuta kwa namna yake n.k.
Katika makala hii tutajikita zaidi katika matumizi ya kompyuta kwa namna yake,
tutajikita hapa kwani hii ndio inaonekana kuwa teknolojia mpya kabisa katika
mazingira ya lugha ya Kiswahili na dhana mpya zinazidi kuibuliwa kila siku
katika matumizi ya kompyuta.
Kompyuta kimekuwa kifaa muhimu sana
katika shughuli nyingi za kimaendeleo, kwa kutumia kompyuta watu wamekuwa
wakifanya mambo chungu nzima na kwa urahisi sana. Bila shaka umekwisha sikia
kuwa unaweza kununua bidhaa kwa kutumia kompyuta ukiwa nyumbani kwako bila ya
hata kwenda huko sokoni au dukani. Bila shaka umekwisha sikia kuwa mabenki,
hospitali, taa za kuongozea magari barabarani, kamera za usalama, ndege za
abiria na kivita na hata lift unazopanda kila siku unapoingia na kutoka ofisini
katika jengo refu huendeshwa kwa msaada wa kompyuta. Bila shaka umekwisha
jionea mwenyewe au kusikia habari kama hizi. Umekwisha sikia kuwa mtu anaweza
kumchagua mgombea wa urais au ubunge kwa kutumia kompyuta! Haya na mambo chungu
nzima hufanyika kwa msaada wa kompyuta. Katika nchi zilizoendelea matumizi ya
kifaa hiki yanaendelea kushika hatamu kiasi kwamba kila kitu sasa kinafanywa
Kwa kutumia mashine zinazoongozwa kwa kompyuta.
Kwa hiyo unaweza kuona ni jinsi gani
matumizi ya kompyuta yalivyokuwa muhimu sana katika maisha ya kila siku. Serikali
za Jumuia ya Afika mashariki zimekuwa zikisisitiza matumizi ya kompyuta kuanzia
shule za awali, kwa kuzingatia kwamba matumizi ya kompyuta yameongezeka sana katika
ulimwengu wa sasa lakini changamoto zinazoikabili progaramu hii imekuwa ni
lugha ya kufundishia. Kwa mfano Tanzania somo la TEHAMA linafundishwa kuanzia
shule za msingi; shule za msingi kwa Tanzania hutumia lugha ya Kiswahili kama
lugha ya kufundishia na kwa kuwa
programu za kompyuta zimeandikwa kwa kiingereza, italazimika programu hizo
zitafsriwe katika Kiswahili ili ufundishaji uweze kuwa rahisi. Na hapa ndipo
tunapata istilahi mpya za Kiswahili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.
Licha ya uhitaji wa kufundishwa somo
la Kiswahili katika shule za awali lakini pia makampuni makubwa yanayohusika na
mawasiliano ya kompyuta yamekuwa yakitafuta nija ya kujiimarisha kibishara
katika maeneo mbalilimbali duniani. Mbinu moja wapo amabyo wemekuwa wakiitumia
ni kuhakikisha wateja wao wanapata huduma kwa lugha yao. Kwa mfano kampuni ya
Microsoft kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ilianzisha mradi wa
kutafsiri program zake kwa Kiswahili. Kama asemavyo King’ei (2010) “kampuni ya
talakirishi iitwayo microsoft ilitekeleza
hatua ya kihistoria mwaka 2005 kwa
kuanzisha kamusi maalumu inayowawezesha watumiaji wa talakirishi kutumia lugha
ya Kiswahili katika mawasiliano yao yote kwa kompyuta. Programu hii mpya
inamwezesha mtumiaji kompyuta asiyefahamu lugha nyingine kama vile kiingereza
kutumia kompyuta na kuwasiliana bila shida yoyote”.
Msanjila
na wenzake (2011) pia wanasema hadi wakati huu lugha ya Kiswahili imekwisha
ingizwa katika mifumo miwili ya kompyuta ijulikanayo kama linuksi na mikrosofti. Wanaendelea
kusema, kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo hii maana yake ni kwamba mtumiaji
anaweza kuvinjari mifumo hiyo ya kompyuta kwa Kiswahili akiamua kufanya hivyo.
Kwa
mujibu wa maelezo ya wataalamu hawa ni wazi kwamba mpaka sasa hivi Kiswahili
kinatumika katika baadhi ya mifumo ya kompyuta. Katika kufanikisha hili
ujanibishaji wa programu kadhaa za kompyuta ulifanyika. Kahigi (2007) anasema
“Mradi wa ujanibishaji wa Office 2003 na Windows XP kwa Kiswahili sanifu
ulitekelezwa katika kipindi 2004-2005. Malengo ya maradi yalikuwa: (1) kuandaa
istilahi za kompyuta kwa Kiingereza-Kiswahili, na (2) kutafsiri programu nne za
kawaida za Office (Outlook, Excel, Word na PowerPoint) na Windows XP”. Hii
inamaanisha kwamba programu hizi zinapatikana katika lugha ya Kiswahili. Hebu
tuangalie mifano ya istilahi kutoka katika programu hizi za Office 2003 na
Windows XP kama zilivyoorodheshwa na Kahigi, ni istilahi zaidi ya 600 lakini
hapa tutaangalia chache tu:
- Fikia Access
- Kibonye fikishi Access key
- Viziada Accessories
- Amilisha Activate
- Kirekebu Adapter
- Kihadharishi Alert box
- Program matumizi Application
- Makaaba Archive
- Vitome mchoro Bit map
- Kiashiri mada Book mark
- Sakura Browse
- Kisakuzi Browser
- Kwa kaida By default
- Msabidi Configuration
- Sabidi Configure
- Puna Crop
- Kielekezi Cursor
- Tanafsi Custom
- Pakua Download
- Kijachini Footer
- Nakala bayana Hard copy
- Kidakuzi Cookie
- Sanidi Install
- Kicharazio Keyboard
- Kiolezo Template
- Tafutatua Trouble-shoot
- Sanidua uninstall
- Sasaisha Update
- Kidhulishi Highlighter
- Kichapishi Printer
- Kingavirusi Antivirus
Hizi
ni baadhi tu ya istilahi kati ya nyingine nyingi zilizoundwa katika mradi wa
kujanibisha programu za office 2003 na Windows XP. Jitihada za kampuni ya Microsoft hazikuishia hapo tu, mnao
mwezi mei mwaka 2011 kampuni hii ilizindua programu ya Windows 7 kwa Kiswahili,
hatua hii imezidi kukiimarisha Kiswahili katika Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano. Haya ni maendeleo makubwa katika lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo sasa
mtumiaji wa Kiswahili anachaguo la kufanya, ama kuendelea kutumia programu hizi
kwa lugha ya Kiingereza au kwa lugha ya Kiswahili.
4. Changamoto
zinazoikabili lugha ya Kiswahili katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
Kila
jitihada zinazofanywa katika kufikia malengo fulani huwa hakukosi changamoto.
Katika jitihada za kufanya Kiswahili kuwa lugha ya kiteknolojia kumetokea
changamoto nyingi, moja wapo iliyo kuu kabisa ni kwamba lugha ya Kiswahili
haimilikiwi na taifa lolote tajiri kwa hiyo katika harakatika za kuendeleza
inakumbana na changamoto nyingi kama vile ukosefu wa fedha na hata utayari wa
viongozi wa kisiasa kukiendeleza Kiswahili ni mdogo sana, hata hivyo harakati
hizi zinapingwa na mataifa ambayo lugha zao zimeendelea sana kiteknolojia kwa
kuhofia kwamba zitafunikwa na matumizi ya Kiswahili. Wapo tayari kutoa misaada
ili kuendeleza lugha zao kukididimiza Kiswahili kitu ambacho kinafanya harakati
za kukiendeleza Kiswahili kuwa ngumu kwani nchi kinamozungumzwa Kiswahili
hazina pesa za kupambana na mataifa makubwa yanayopigia upatu lugha zao.
Kutokana
na sababu hizo, kasi ya uundaji wa istilahi za kiteknolojia imekuwa ndogo sana,
kwani kufanya hivyo pia kunahitaji pesa, na mara nyingi pesa zimekuwa
zikitolewa na wahisani au makampuni yanayohusika kitu kinachotokea mara moja
baada ya muda mrefu sana.
Pia,
viongozi wa serikali hawajatilia mkazo suala hili, hawajaona umuhimu wa
kukiendeleza Kiswahili kitenolojia. Nguvu zao nyingi wameziweka katika miradi
mingine ya kimaendeleo huku wakisahau kabisa kuwa Kiswahili pia kinahitaji
kwenda sambamba na maendeleo hayo. Kwa hiyo hii imekuwa ni changamoto katika
maendeleo ya lugha ya Kiswahili.
Kwa
kuwa istilahi hizi zimekuwa zikifanywa na watu tofautitofauti, ni muhimu kuwapo na jopo maalumu la
kusanifisha istilahi hizi kabla hazijasamabazwa. Kwa kufanya hivi hakutakuwa na
matumizi tofauti ya istilahi katika dhana moja. Hali hii inajitokeza sana
endapo uundaji wa istilahi utakuwa umefanywa katika makundi tofauti.
Utayari
wa watumiaji; watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili wamekuwa wakilalamika
kuhusu kutumia programu za komyuta kwa lugha za Kiswahili. Madai yao ni kwamba istilahi
za Kiswahili ni ngumu sana na hivyo si rahisi kuzitumia, kwa mfano, wengi
wamezoea kusema password na kwa hiyo
ukiwaambi kwamba password kwa
Kiswahili huitwa nywila au mouse inaitwa puku watabaki wakikushangaa na watona kama unawapa kazi kubwa sana.
Kwa hiyo hii nayo inasabaisha matumizi ya Kiswahili katika vifaa vya
kiteknolojia hususani kompyuta kuwa hafifu.
5. Hitimisho
Katika
makala hii tumeona TEHAMA ni kitu gani na umuhimu wake katika maisha ya kila
siku ya binadamu, tumeona umuhimu wa lugha za kiafrika kuendelezwa katika
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa umahususi zaidi tumeona jinsi Kiswahili
kilivyo muhimu zaidi katika uwanja wa maendeleo ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano. Tumengalia pia maendeleo yaliyofikiwa na lugha ya Kiswahili katika
TEHAMA huku tukionesha baadhi ya istilahi za Kiswahili zinazotumika katika
matumizi ya kompyuta, pia tumeangalia changamotozinazo ikabili lugha ya
Kiswahili katika jitihada za kuiendeleza kiteknolojia. Sasa tuangalie
mapendekezo juu ya nini kifanyike ili kuhakikisha lugha ya Kiswahili inashika
hatamu katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano:
Viongozi
wa ukanda wa Afrika Mashariki waungane kuhakikisha wanaunda sera nzuri
kuhusiana na maendeleo ya lugha ya Kiswahili ikiwa ni pamoja na kuandaa mradi
maalumu wa kuunda istilahi mbalimbali za kiteknolojia, hii itasaidia lugha ya
Kiswahili kuimarika katika matumizi ya teknolojia. Pamoja na hilo pia itenge
bajeti maalumu kwa ajili ya kuandaa na kutekeleza miradi mbalimbali ya kuunda
istilahi za Kiswahili katika teknolojia zinazoibuka ili kuahakikisha
wazungumzaji wa lugha ya Kiswahili hawaachwi nyuma katika matumizi ya
teknolojia mpya ziibukazo.
Pia
kutokana na changamoto ya kutokuwapo na jopo maalumu la kuunda istilahi za
kiteknolojia pindi mradi kama huu unapotokea, hali hii imesababisha kuwapo kwa
istilahi ambazo hazijasanifishwa na pengine kuwapo na istilahi zaidi ya moja
inayorejelea dhana moja, hii ni kwa sababu miradi kama hii hufanywa na watu
tofautitofauti na pengine wataalamu hawa wana ujuzi katika lugha tu lakini
katika teknolojia hususani kompyuta hawana maarifa ya kutosha au hawana kabisa.
Katika hali kama hii ni vigumu kuunda istilahi zinazofanana au zinazobeba dhana
kamili kama ilivyokuwa ikikusudiwa katika lugha chanzi. Kwa hiyo katika uundaji
wa istilahi za kiteknolojia ni vema kuwepo na jopo maalumu amablo lina ujuzi wa
kutosha katika lugha na masuala ya kiteknolojia, hii itasaidia kutoa istilahi
nzuri na zinazoeleweka kwa urahisi kwa watumiaji.
Baada
ya kuundwa istilahi hizi inatakiwa zisambazwe kwa watumiaji kwa kiwango
kinachoridhisha ili waweze kujifunza na kuzifahamu na hatimaye kuzizoea katika
matumizi yao ya kila siku katika Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Nasema
hivi kwa saba usambazaji wa istilahi hizi umekuwa haufanywi kwa kiwango
kinachohitajika, na katika usambazaji, vyombo vya habari vipewe kipaumbele, kwani
istilahi hizi zikitumiwa na vyombo vya habari itakuwa rahisi sana kwa watumiaji wengine kuzitumia.
Wazungumzaji
wa Kiswahili pia wawe tayari kutumia istilahi hizi au programu za Kiswahili
katika matumizi yao ya kopmyuta. Programu kadhaa za kompyuta zimejanibishwa kwa
Kiswahili lakini wazungumzaji wengi wa Kiswahili bado wanatumia programu
zilizoandikwa kwa lugha ya Kiingereza, program ya Windows 7 inapatikana kwa
Kiswahili lakini nina wasiwasi kama miongoni mwetu kuna mtu hata mmoja
anayetumia Windows 7 ya Kiswahili. Kwa hiyo napendekeza kwenu suala hili, kwa
kuwa sisi tumejitoa kueneza na kuienzi lugha ya Kiswahili pia ni jukumu letu
kuchangamkia fursa kama hizi, tuwe wa kwanza kutumia programu kama hizi kwa
Kiswahili pindi zinapotokea, kwa kufanya hivi tutakuwa tunakienzi Kiswahili na
kukikuza kwani watu wanaotuzunguka
watakapotuona tunatumia Windows ya Kiswahili watashawishika na wao kuitumia,
hivyo kwa njia hii tutakuwa tumefanikiwa kukuza na kuienzi lugha ya Kiswahili.
Ninaamini
kila mmoja wetu ana ndoto za kuona lugha
ya Kiswahili siku moja inakuwa lugha ya bara zima la Afrika, kwa maana kwamba Kiswahili
kinazumgumzwa kila kona ya bara hili, basi kama ndio ndoto zetu sote hatuna
budi kupigania maendeleo ya lugha ya Kiswahili kwa nguvu zetu zote, tukifanya
hivi kwa pamoja kwa kijishughulisha na masuala yanayohusika na Kiswahili, kwa
kuandika, kufanya utafiti katika Nyanja mbalimbali za lugha ya Kiswahili ndoto
zetu zitatimia na kumbukumbu zetu zitakumbukwa katika vizazi vinavyokuja kama
anavyokumbukwa leo hii Shaaban Robert. Ninaamini kuwa tunaweza!!
Kiswahili,
Hazina ya Afika kwa Maendeleo Endelevu!
Marejeo
Akinyi, J.J. (2010). Kiswahili usage in ICT in NEPAD secondary
schools in Kenya. Katika TheJournal of Language, Technology &
Entrepreneurship in Africa, Vol. 2. No.1. www.ajol.info/index.php/kcl/article/vieFile
Kahigi, K.K (2007). Ujanibishaji wa
office na windows xp kwa Kiswahili sanifu. Katika Kioo cha Lugha juzuu la 5. Dar es salaam. TUKI.
Kamau, S.N. (2009). Kiswahili,
utandawazi na umoja wa Afrika. Katika journal of language, technology&
entrepreneurship in Africa vol.1. www.ajol.info/index.php/kcl/article/vieFile
Katambi, S (2011). Teknolojia ya Habari na Mawasilianao
(TEHAMA). Dar es salaam: Modecs
Solutions
King’ei, K (2010). Misingi ya isimujamii. Dar es salaam.
Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Msanjila,Y.P, Kihore,Y.M na D.P.B
Massamba (2011). Isimujamii sekondari na
vyuo.
Dar es salaam. Taasisi ya
Uchunguzi wa Kiswahili.
Osborn, D. Z. (2006). African
Languages and Information and Communication Technologies: Literacy, Access, and the Future.
Katika Selected Proceedings of the
35th Annual Conference on African Linguistics, ed.
John Mugane et al., 86-93. Somerville, MA: Cascadilla Proceedings Project.
www.lingref.com, document #1299.
Osborn, D. Z. (2010). African Languages in a Digital Age. Cape
Town: HSRC Press.
CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
TAASISI
YA TAALUMA ZA KISWAHILI
IDARA YA LUGHA YA KISWAHILI NA ISIMU
KI113:MBINU ZA UTAFITI NA UANDISHI WA TASNIFU KATIKA LUGHA NA FASIHI
RIPOTI YA UTAFITI KUHUSU
MBINU ZILIZOTUMIKA KATIKA UUNDAJI WA
ISTILAHI ZA KISWAHILI ZILIZOINGIZWA KATIKA MIFUMO YA MAWASILIANO YA KOMPYUTA: MIFANO
KUTOKA MFUMO WA KOMPYUTA WA LINUX.
JINA: MALAGIRA
ARITAMBA.
NAMBA YA USAJILI: 2010-04-02466
MWALIMU WA SOMO: E. MAHENGE
NA DKT. G. MRIKARIA
SHUKRANI
Utafiti huu umefanikiwa
kwa jitihada kubwa za waalimu wangu wa somo.Napenda nimshukuru kwa dhati
mwalimu Elizabeth Mahenge kwa kutumia muda wake mwingi katika kunielekeza na kurekebisha mada yangu
ya utafiti.Namshukuru pia Mwalimu G.Mrikaria kwa kututia moyo katika
kufanikisha utafiti huu.
Vilevile
nawashukuru wanafunzi wenzangu kwa kunishauri na kunitia moyo katika kuendelea
na utafiti huu.Wanafunzi wafuatao wamekuwa mchango mkubwa katika kufanikisha
utafiti huu;Ally Laila,Thomas Edson,Ndumbaro Eric, Ndege Busalu pamoja na
Ntenga Elias.Nawashukuru pia Boniface Jacob na James Balele kwa utayari wao wa
kunisaidia kuchapa utafiti huu.Na mwisho nawashukuru wote walionisaidia kwa
namna moja ama nyingine,Mungu awabariki sana!
.
YALIYOMO
Sura
ya kwanza:Utangulizi na Nadharia ya uundaji istilahi…………………. 1
1.0 Utangulizi……………………………………………………………………………………1
1.1 Tatizo
la utafiti……………………………………………………………………….3
1.2 Malengo
ya utafiti…………………………………………………………………....3
1.3 Umuhimu
wa utafiti…………………………………………………………………4
1.4 Dhana
ya istilahi,linux na nadharia ya uundaji istilahi……………………………4
Sura ya pili:Mapitio ya marejeo na
mbinu za ukusanyaji data………………..8
2.1
Mapitio ya marejeo………………………………………………………………………….8
2.2 Mbinuza ukusanyaji data ……………………………………………………………..10
Sura ya tatu:Uchambuzi wa data………………………………………………11
3.1
Utangulizi………………………………………………………………………………….11
3.2 Mbinu zilizotumika katika uundaji wa
istilahi za Kiswahili katika Linux………….11
3.3 Ubora na udhaifu wa mbinu
zilizotumika kuunda istilahi za Kiswahili katka Linux…16
3.3.1 Ubora wa mbinu zilizotumika
……………………………………………………16
3.3.2 Udhaifu wa mbinu
zilizotumika…………………………………………………18
3.3.3 Mbinu bora zaidi katika
uundaji wa istilahi za Kiswahili…………………………19
Sura ya nne:Muhtasari na Hitimisho…………………………………………..20
4.1
Matokeo ya utafiti kwa muhtasari…………………………………………………………20
4.2
Hitimisho…………………………………………………………………………………….22
Marejeo
Viambatisho
SURA YA KWANZA
1.0
Utangulizi
Lugha
ni kielelezo cha maisha ya jamii kwani huenda sambamba na mabadiliko au
maendeleo katika jamii. Kila sekta ya jamii iwe
siasa,elimu,sayansi,teknolojia,utamaduni,dini,kilimo,uhandisi,sanaa,uchumi
ama biashara hubadilika kila mara .Uvumbuzi mpya kila mara huzua dhana mpya
ambazo zinahitaji maneno mapya kuzielezea(King’ei 2010)
King’ei(ameshatajwa)
anaendelea kusema kuwa ukuzaji wa
msamiati na istilahi ni jambo la kawaida katika kurekebisha lugha ili iweze
kuambatana na wakati au iwe ya kisasa. King’ei anaendelea kusema kuwa ukuzaji
upya wa istilahi hufanyika kwa sababu mbalimbali.Kwanza kabisa lugha sharti
iweze kuelezea dhana mpya zinazoingia katika jamii kutokana na mabadiliko
katika jamii.Sababu ya pili ni kwamba maana ya maneno yanayotumika katika lugha
hupanuliwa ili kuchukua maana mpya au pana kuliko ile ya awali.Sababu ya tatu
ya kuwepo haja ya kustawisha istilahi mpya katika lugha ni ile haja ya kufasiri
maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine.
Msanjila
na wenzake (2011) wanasema hadi wakati huu lugha ya Kiswahili imekwisha ingizwa
katika mifumo miwili ya kompyuta ijulikanayo kama linuksi na mikrosofti.Wanaendelea
kusema,kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo hii maana yake ni kwamba mtumiaji
anaweza kuvinjari mifumo hiyo ya kompyuta kwa Kiswahili akiamua kufanya hivyo.
Pia
King’ei(ameshatajwa) anaelezea kuwa,kampuni ya talakirishi iitwayo microsoft ilitekeleza hatua ya
kihistoria mwaka 2005 kwa kuanzisha
kamusi maalumu inayo wawezesha watumiaji wa talakirishi kutumia lugha ya
Kiswahili katika mawasiliano yao yote kwa kompyuta,anaendelea kusema,programu
hii mpya inamwezesha mtumiaji kompyuta asiyefahamu lugha nyingine kama vile
kiingereza kutumia kompyuta na kuwasiliana bila shida yoyote.
Katika
mchakato wa kuziweka programu hizi katika Kiswahili, ilihitajika kuunda
istilahi za
Kiswahili
ili kukamilisha shughuli hii mbinu mbalimbali za uundaji istilahi zilitumika.
Katika
uundaji wa istilahi za Kiswahili kuna mbinu mbalimbali zinazotumika. Kwa mujibu
wa
Kiango(2004)
amebainisha mbinu za kuunda istilahi za Kiswahili kuwa ni pamoja na:Kubuni,anasema,njia
hii inaweza kutumika katika kukabili mazigira ya aina mbili; kubuni msamiati ambao
utataja mambo yaliyomo katika jamii ambayo hayajapata msamiati wa Kiswahili.
Pili ni kubuni msamiati ambao utataja mambo kutoka nje ya jamii yenye msamiati
wa kigeni, mbinu nyigine ni kukopa; kukopa kwa kutohoa msamiati wa
kigeni,kukopa kwa kutafsiri msamiati wa kigeni na kukopa kwa kuingiza maneno ya
kibantu na lahaja na njia nyingine ni ya kufupisha maneno.
Kahigi
(2004) anasema mbinu za kuunda istilahi
ni pamoja na: unyambulishaji; unyambulishaji ni kupachika viambishi undaji ili
kuunda neno lenye dhana na muafaka. Mfano, modification→ukumushaji. Mbinu
nyigine ni ukopaji; ukopaji ni kuchukua neno kutoka lugha chanzi na kulitohoa
ili likubaliane na taratibu za kisarufi za lugha pokezi. Mbinu zingine
zilizoainishwa na Kahigi ni: tafsiri mkopo;ni aina ya tafsiri kutoka lugha
chanzi ambayo ni ya moja kwa moja, mbinu nyigine ni uundaji wa maneno mapya,
mbinu hii huhusisha uundaji wa maneno mapya ambayo yalikuwa hayapo kwenye lugha
lengwa, mfano byte > baiti, uambatani; ni uwekaji wa maneno mawili
au zaidi yanayowakilisha dhana moja, mfano magneticfield >ugasumaku,
ufupishaji; hii ni mbinu ya kufinyanza maneno na kupata neno moja, mfano,
UWT(Umoja wa Wanawake Tanzania).
Mtafiti
mwingine ambaye ameelezea mbinu za uundaji istilahi ni Sewangi(2004) yeye anasema
mbinu za uundaji istilahi ni pamoja na: kutohoa,kwa mfano; computer > kompyuta,
program>programu, mbinu nyingine ni kubuni, kwa mujibu wa Sewangi anasema,
mbinu ya kubuni inaweza kufanywa kidhahania au kwa kutumia vigezo mahususi.
Kubuni istilahi kidhahania hutetewa kwa hoja kuwa hakuna uhusiano wa
moja kwa moja baina ya istilahi na dhana inayo bebwa, hivyo neno lolote laweza
kuundwa na kupewa hadhi ya istilahi ya dhana fulani. Njia mojawapo ya kuunda
istilahi kidhahania ni kutumia fomula za kompyuta ambapo maneno mengi yanaweza
kuzalishwa na kupachikwa dhana mahususi katika uwanja fulani wa maarifa. Njia
ya kuunda istilahi kivigezo huweza kufanywa kwa kutumia vigezo mahususi kama
vile
kazi, umbo au mwonekano wa kitu. Kwa mfano kwa kutumia kigezo cha kikazi kisawe
cha calculator kimebuniwa kuwa ni kikokotozi (kitu kinachofanya kazi ya
kukokotoa), kisawe cha data saver kimekuwa kihifadhi data (kitu kinachohifadhi
data). Mbinu nyingine iliyoainishwa na Sewangi ni mbinu ya kupanua maana ya
maneno yaliyopo; njia hii huchukua neno lenye maana ya jumla na kuliongezea
maana ya kihistilahi katika mazingira ya kitaalamu, kwa mfano neno kifaru
ambalo maana yake ya jumla ni mnyama lakini katika mazingira ya utaalamu wa
kijeshi ni kisawe cha tank.
Kwa
kuzingatia maelezo ya wataalamu hawa kuna mbinu tofautitofauti za kuunda
istilahi. Kwa hiyo kutokana na kwaba kuna mbinu tofautitofauti za kuunda
istilahi,utafiti huu hulenga kubainisha mbinu zilizotumika katika kuunda
istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika mfumo wa kompyuta wa linux.
1.1 Tatizo la utafiti
Kulingana
na tafiti za wataalamu hawa,wameelezea kuingizwa kwa Kiswahili katika mifumo ya
kompyuta ya linux na Microsoft,kwa mfano, Msanjila na wenzake
(2011) na King’ei (2010) wameelezea kuhusu hili. Vilevile wataalamu wengine
kama vile Kiango (2004), Sewangi (2004) na Kahig i(2004) wao wameainisha mbinu
mbalimbali za kuunda istilahi za Kiswahili. Kwa ujumla wataalamu hawa
hawajaonyesha mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili
zilizoingizwa katika mifumo ya mawasiliano ya kompyuta hususani mfumo wa
kompyuta wa linux, kwa hiyo utafiti
huu hulenga kuziba pengo hili kwa kuchunguza mbinu zilizotumika katika uundaji
wa istilahi za Kiswahili katika linux.
1.2 Malengo ya utafiti
Malengo
ya utafiti huu yamegawanyika katika sehemu kuu mbili:
1.2.1 Lengo kuu na
1.2.2 Malengo mahususi
1.2.1 Lengo kuu
Lengo
kuu la utafiti huu ni kutaka kutalii istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika
mfumo wa mawasiliano ya kompyuta wa linux
na kuainisha mbinu zilizotumika kuunda istilahi hizo.
1.2.2 Malengo mahususi
Malengo
mahususi ya utafiti huu ni mawili, ambayo ni: kupambanua ubora na udhaifu wa
mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux
na kubainisha mbinu bora zaidi inayoweza kutumika katika uundaji wa istilahi za
Kiswahili.
1.3 Umuhimu wa utafiti
Umuhimu
wa utafiti huu ni kwamba utasaidia kubainisha mbinu bora za uundaji wa istilahi
za Kiswahili. Vilevile utafiti huu utawasaidia watumiaji wa kompyuta wanaotumia
programu hii ya linux kwa Kiswahili kuelewa kwa urahisi istilahi zilizotumika
baada ya kubainisha mbinu zilizotumika katika kuunda istilahi hizo.
1.4 Dhana ya istilahi, linux na
nadharia ya uundaji istilahi
Istilahi ni
dhana iliyofasiliwa na wataalamu mbalimbali na wote wanakubaliana kuwa,
istilahi ni msamiati utumikao katika uwanja fulani maalumu wa lugha. Wataalamu
wanaokubaliana na fasili hii ni pamoja na King’ei(2010), Samson(1988) na
Kiango(2004). Kwa hiyo kulingana na fasili hii si kila msamiati ni istilahi
bali msamiati huwa istilahi pale unapotumika katika Nyanja maalumu za
kitaaluma. Kila uwanja maalumu wa kitaaluma huwa na msamiati wake ambao hauna
maana nje ya taaluma hiyo wala haufahamiki kwa wazungumzaji lugha wasiokuwa
wataalamu wa lugha hiyo. Kwa mfano msamiti unaotumika katika isimu,fasihi,teknolojia
ya habari na mawasiliano na kadhalika ni maalumu na hutumiwa na kueleweka tu na
wataalamu wahusikao na nyaja husika.
Linux
kwa mujibu wa Msanjila na wenzake(2011) ni mfumo wa kompyuta huria unao ruhusu
watu mbalimbali kuchangia katika marekebisho na maendeleo yake. Kimsingi linux ni mfumo endeshi wa kompyuta. Ni
program katika kompyuta iayosaidia programu-tumizi na mtumiaji wa kompyuta
kufikia vifaa fulani katika kompyuta ili kufanya kazi iliyokusudiwa, linux ni sawa na
program-tumizi zingine
kama vile windows (Linux.com).
Nadharia ya uundaji istilahi
hujumuisha mambo kadhaa, kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko(2008) mambo
hayo ni pamoja na sababu za uundaji wa istilahi, njia au mbinu za uundaji
istilahi,vyombo vya uundaji istilahi na misingi ya uundaji istilahi.
Katika
sababu ya uundaji istilahi Tumbo-Masabo na Mwansoko wanasema kuwa, uundji wa
istilahi ni muhimu panapotokea haja ya kushughulikia nyanja ambazo zilikuwa
hazishughulikiwi kwa kutumia lugha fulani. Uundaji huo aghalabu hufanywa ili
kukidhi haja ya mawasiliano katika elimu ya juu, ufundi na utaalamu,na shughuli
zinazohusu serikali na teknolojia. Kwa hiyo nadharia ya uundaji istilahi
huambatana na sababu au haja fulani ya kufanya hivyo. Kwa mfano uundaji wa
istilahi za Kiswahili katika mfumo wa kompyuta wa linux umeambatana na sababu kwamba, kuuweka mfumo huu wa kompyuta katika Kiswahili ili kusudi
watumiaji wa Kiswahili waweze kuutumia mfumo huu kwa lugha wanayo ifahamu.
Vyombo vinavyohusika katika uundaji
wa istilahi.
Katika
kutekeleza kazi ya kuunda istilahi vimewekwa vyombo maalumu vinavyo tekeleza
suala hili, kwa mfano Tanzania chombo kilchopewa jukumu hili na serikali ni
Barza la Kiswahili la Taifa (BAKITA).
Vilevile
katika nadharia ya misingi ya uundaji istilahi huzingatia mambo yafuatayo:
·
Uundaji wa istilahi ni budi uanzie
kwenye dhana.
·
Dhana hizo zieleweke kwa ukamilifu na
uwazi.
·
Uhusiano baina ya dhana ndio uwe msingi
wa uundaji wa istilahi, istilahi kopwa zichukuliwe kama zilivyo katika umbo
lake la asili kwa kufanya marekebisho machache tu kulingana na sarufi na
matamshi ya lugha kopaji.
·
Istilahi inafaa ziwe fupi iwezekanavyo
lakini zieleweke.
·
Istilahi ziwe na muundo unaoeleweka
yaani zifuate mofolojia ya lugha.
·
Uundaji wa istilahi kwa vifupisho na
akronomia uepukwe hasa kama istilahi kamili si ndefu sana.
·
Istilahi zisiwe na sinonimia au
homonimia.
·
Istilahi ziundwe kwa njia ambayo itakuwa
rahisi kuunda istilahi nyingine kwa
mnyambuliko.
·
Istilahi zitolewe kufuatana na mfumo wa
dhana yaani ziainishwe kuliko kuandikwa kwa alfabeti.
·
Muundo wa istilahi udokeze maana yake
kwa watumiaji wa lugha husika. Kwa hiyo misingi hii haina budi kufuatwa katika
mchakato wa uundaji istilahi.
Nadharia
nyingine kama ilivyoainishwa na Tumbo-Masabo na Mwansoko(wameshatajwa) ni njia
za uundaji istilahi. Katika uundaji wa istilahi kuna njia kuu mbili ambazo
zinatumika zaidi, njia hizo ni pamoja na:
(i)
Kutafsiri hasa kutoka kwenye lugha
zinazojulikana kuwa ni za kimataifa kama vile Kifaransa, Kiingereza, Kihisipania.
(ii)
Kuunda istilahi kutokana na mifumo ya
dhana.
Njia
ya kutafsiri hutumiwa sana na vyombo vingi vya uundaji istilahi kinyume na
misingi ya uundaji ambayo inasisitiza kuwa uundaji huo uanze na dhana, msingi
wa njia hii ni istilahi za lugha chasili ambazo aghalabu hupangwa kwa alfabeti.
Faida ya njia hii ni kwamba istilahi nyingi zinaweza kushughulikiwa kwa muda mfupi pia istilahi za lugha lengwa
huweza kutafsiriwa katika lugha za kimataifa. Hata hivyo hasara ya njia hii ni
kwamba kwa vile kila istilahi hushughulikiwa peke yake, hali hii huweza
kusababisha mtiririko wa mfumo wa istilahi usio na ulingano.
Kahigi
(2004) anasema kuunda istilahi kutokana na mifumo ya kidhana ni kwamba istilahi
huundwa kufuatana na mifumo hiyo. Kwa mfano katika hisabati kuna mifumo ya
elimu-maumbo, elimu-namba, vipimo na kadhalika. Mathalani katika kuunda
istilahi za dhana ya pembe itabidi dhana zifuatazo zishughulikiwe zote kwa
pamoja: pembekali, pembenukta, pembetatu, pembemshabaha, pebemstari na
kadhalika. Faida ya mkabala huu ni kwamba mwishowe mifumo yote ya dhana huwa na
mtiririko wenye ulingano.
Katika
nadharia hii ya njia za uundaji istilahi mbinu mbalimbali hutumika, mbinu hizo
ni pamoja na:mwabatano; hii ninjia ya
uundaji istilahi kwa kuambatanisha maneno mawili au zaidi yaliyo
huru.
Mfano ; mbwa kichaa.
Mnyambuliko;ni
uundaji wa neno jipya kwa kuambatisha viambishi kewenye mzizi au shina la neno.
Mfano;wekeza > uwekezaji.
Muungano;
hii mbinu ni sawa na mwambatano isipokuwa katika muungano maneno mawili au
zaidi huunganishwa ili kuunda neno moja, mfano;kiini+macho > kiinimacho.
Kupanua maana ya maneno;
huu ni mchakato ambapo neno lililopo kwenye lugha hupewa maana pana zaidi ya
maana yake ya awali. Mfano butu maana yake ya kawaida ni –sio kali,-sio kata.
Maana ya kihistilahi ni pembe ambayo ni zaidi ya nyuzi 90 na ndogo kuliko nhyuzi180(hisabati).
Ufupisaji;
ni mbinu ambayo inatumika kufinyanza fungu la maneno ili kuunda neno
moja,mfano; BAKITA (Baraza la Kiswahili laTaifa).
Ukopaji;
ni matumizi ya neno kutoka lahaja ama lugha nyingine, aghalabu neno hilo
hubadilishwa ili lishabihi muundo wa lugha lengwa.
Tafsiri-sisisi;
ni aina ya tafsiri kutoka lugha chasili ambayo ni ya moja kwa moja. Mfasiri
habadili lolote ila anahakikisha tu tafsiri inakuwa sahihi kwa mujibu wa lugha
lengwa. Kwa hiyo katika mchakato wa uundaji wa istilahi za Kiswahili mbinu hizi
hutumika.
SURA
YA PILI
Mapitio
ya marejeo na mbinu za utafiti.
2.1 Mapitio ya Marejeo
Kutokana
na mabadiliko yanayotokea katika jamii wataalamu wameonesha umuhimu wa lugha
kuyakabili mabadiliko hayo. King’ei(2010) anasema lugha ni kielelezo cha maisha
ya jamii siasa, elimu, sayansi, teknolojia, utamaduni, dini, kilimo, uhandisi, sanaa,
uchumi ama biashara hubadilika kila mara, uvumbuzi mpya kila mara huzua dhana
mpya ambazo zinahitaji maneno mapya ya kuzielezea.
Kulingana
na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano,lugha ya Kiswahili haina budi
kuyakabili mazingira haya. King’ei(ameshatajwa) anaelezea hatua ya kihistoria
iliyochukuliwa na kampuni ya Microsoft
mwaka 2005 kwa kuanzisha kamusi maalumu inayowawezesha watumiaji wa kompyuta kutumia
lugha ya Kiswahili katika mawasiliano yao yote kwa kompyuta. Kwa maana kwamba
katika programu hii mpya inamwezesha mtumiaji kompyuta asiyefahamu lugha
nyingine kama vile kiingereza, kutumia kompyuta na kuwasiliana bila shida
yoyote kwa Kiswahili.
Mtafiti
mwingine ni Msanjila na wenzake(2011) wanasema hadi wakati huu lugha ya
Kiswahili imekwisha ingizwa kwenye mifumo miwili ya kompyuta ijulikanayo kama linuksi na mikrosofti. Wanaendelea kusema kuingizwa kwa Kiswahili katika
mifumo hii maana yake ni kwamba mtumiaji anaweza kuvinjari mifumo hiyo ya
kompyuta kwa Kiswahili akiamua kufanya hivyo.
Kimsingi
hatua ya kuingiza Kiswahili katika mifumo hii ya kompyuta ni hatua muhimu sana
katika maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano, katika mchakato wa
kuiweka mifumo hii katika lugha ya Kiswahili ilihitajika kuundwa istilahi za
Kiswahili ili mifumo hii iwekwe katika Kiswahili. Katika kuunda istilahi za
Kiswahili mbinu mbalimbali hutumika, wataamu mbalimbali wamejadili kuhusu mbinu
hizo:
Tumbo-Masabo
na Mwansoko(2008) wanasema mbinu za uundaji istilahi ni pamoja na: Muungano wa maneno, mfano; mwanaisimu, mwambatano wa maneno, mfano; nusu
kipenyo,
8
Unyambulishaji,
mfano;
ambisha > uambishaji, upanuzi wa maana za maneno, uhulutishji,
mfano; kizigeu > kiziogeu, ukopaji (kukopa kutoka lugha za kigeni, lugha za kibantu au lahaja)
na tafsiri-sisisi (tafsiri mkopo), mfano;
measure of time > kipimo cha wakati.
King’ei(2010)
ameainisha mbinu za uundaji wa istilahi za Kiswahili kuwa ni pamoja na uunganishaji wa maneno, ukopaji, kutafsiri
maneno ya kigeni, mbinu ya ufupishaji mfano;UKIMWI (Upungufu wa Kinga
Mwilini) na utohozi.
Kahigi
(2004) anasema mbinu za uundaji wa istilahi za Kiswahili ni pamoja na:unyambulishi, uambatani, uhulutishi, ufupishaji,
utemaji, ukopaji, tafsiri mkopo na uundaji wa maneno mapya kabisa.
Vilevile
Kiango (2004) ameanisha mbinu zifuatazo katika undaji wa istilahi za Kiswahili: kubuni na kukopa (kutoka lugha za kigeni, lugha za kibantu na lahaja).
Kwa
hiyo kulingana na wataalamu hawa tunaweza kuanisha mbinu za uundaji wa istilahi
za Kiswahili kuwa ni:
·
Unyambulishji
·
Muungano wa maneno
·
Mwambatano wa maneno
·
Ukopaji
·
Tafsiri mkopo(tafsiri sisisi)
·
Uhulutishaji
·
Ufipishaji
·
Utemaji
·
Upanuaji wa maana ya maneno yaliyopo na
·
Kubuni
Tafiti
za wataalamu hawa zina umuhimu mkubwa kwani zimesaidia kujua kuingizwa kwa
Kiswahili katika mifumo ya kompyuta ya linux
na Microsoft na vilevi zimetusaidia
kujua mbinu za uundji istilahi za Kiswahili. Kwa hiyo katika utafiti wetu
tutabainisha mbinu zilizotumika
kuunda istilahi za
Kiswahili katika linux kati ya hizo
zilizoainishwa na wataalamu hao
2.2 Mbinu za ukusanyaji data
Katika
utafiti huu mbinu iliyotumika ni moja, yaani mbinu ya kusoma marejeo mbalimbali
hii ni kwa kuwa utafiti huu ni wa kimakitaba. Mbinu hii imetumika katika
ukusanyaji wa data zinazohusu istilahi za Kiswahili zilizoingizwa katika mfumo
wa kompyuta wa linux, ambapo mbinu hii imetumika kwa kusoma marejeo kwa njia ya
wavuti na kukusanya istilahi za Kiswahili zilizokuwepo katika mfumo wa kompyuta
wa linux.
Mbinu
hii pia imetumika katika kukusanya data zinazohusu mbinu za uundaji istilahi za
Kiswahili. Kwa kusoma marejeo mbalimbali data zinazohusu mbinu za uundaji wa
istilahi za Kiswahili zilikusanywa.
Vilevile
mbinu hii imetumika katika ukusanyaji wa data zinazohusu ubora na udhaifu na
udhaifu wa mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux. Na pia mbinu hii imetumika katika
ukusanyaji wa data zinazohusu kubainisha mbinu bora katika kuunda istilahi za
Kiswahili.
Data
katika utafiti huu zimekusanywa kutoka faharasa ya teknolojia ya habari ya KILinux(KlnX) juzuu ya kwanza. Faharasa
hii inajumuisha orodha ya istilahi 700.
Sampuli ya utafiti huu inajumuisha istilahi 100. Sampuli hii imechukuliwa
kinasibu (kiholela) yaani hakuna mpangilo au utaratibu wowote maalumu uliofutwa
katika uchukuaji wa sampuli.
SURA
YA TATU
Uchambuzi
wa data
2.1 Utangulizi
Utafiti
huu umegawanyika katika sehemu kuu mbili, sehemu ya kwanza inahusu uchambuzi wa data zinazohusu mbinu
zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux na sehemu ya pili inahusu kupambanua ubora na udhaifu wa mbinu
zilizotumika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux na kubainisha mbinu iliyo bora katika kuunda istilahi za
Kiswahili. Katika uchambuzi wa data hizi tutatumia nadharia ya uundaji istilahi
za Kiswahili ambayo imekwishaongelewa katika kipengele cha 1.4.
2.2
Mbinu zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili zilizoingizwa
katika linux.
Mbinu
zilizotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux ni kama
zilivyobainishwa hapa chini:
Unyambulishi;
katika mbinu hii kitenzi kinaweza kugeuzwa kikawa nomino au kivumishi kinaweza
kugeuzwa kikawa kitenzi au au nomino. Mbinu hii imetumika kwa kiasi kikubwa,
mifano ifuatayo hudhihirisha matumizi ya mbinu hii.
·
Accessing >
ufikio ( viambishi u-i-o vimeambatiswa katika shina fika).
·
Accsess >
fikio (viambishi i-o vimenyambulishwa katika shina fika )
·
Allocation >
utengaji (viambishi u-aji vimeambatishwa katika shina tenga)
·
Bookmark link >
alamisho (viambishi ish-o vimeambatishwa katika shina alama).
·
Bookmark >
alamisha(t) (viambishi ish-a vimeambatishwa na kuunda kitezi alamisha)
·
Deleting >
ufutaji (viambishi u-aji vimeambatishwa katika kitenzi futa )
·
Deletion >
mfuto (viambishi m-o vimeambishwa katika kitenzi futa nakupata neno mfuto)
·
Input
> ingizo (kiambishi –o
kimeambishwa katika shina ingiza na kuunda istilahi ingizo).
·
Interactive >
wasilianifu ( kiambishi –ifu kimeambishwa katika shina wasiliana na
kuunda neno wasilianifu).
·
Allocation(n) >
mtengo (viambishi m-o vimeambishwa katika shina tenga na kuunda nomino
mtengo ikiwa na dhana ya matokeo).
Mwabatano;
hii ni njia inayotumika kwa kuambatanisha maneno mawili au zaidi. Katika linux
kuna istilahi zenye mwambatano wa maneno mawili na mwambatano wa maneno matatu.
Mifano ifuatayo inadhihirisha matumizi ya mbinu hii:
·
Add-on help >
msaada nyongeza ( yameambatishwa maneno msaada na nyongeza).
·
Alphabet text character >
kiwambo alfabeti (kiwambo + alfabeti).
·
Aperture value >
thamani upenyo (thamani + upenyo)
·
Background colour >
rangi usuli (rangi + usuli).
·
Block device >
kitunza data ( (ki)tunza + data).
·
Bullet list >
orodha tobwe (orodha + tobwe).
·
Composer >
programu tumizi (programu+ tumizi).
·
Configuration utility >
programu sanidi (programu + sanidi).
·
Checksum >
namba thibitishi (namba + thibitishi).
·
Encrypted >
msimbo fiche (msimbo + fiche).
Vilevile
kuna istilahi zilizoundwa kwa kuambatanisha maneno matatu. Mfano:
·
Encrypted text >
matini-msimbo fiche (matini + msimbo + fiche).
·
Full-screen mode >
modi-skrini nzima (modi + skrini + nzima).
·
Small caps >
herufi kubwa ndogo (herufi + kubwa + ndogo)
·
Column spam >
upana-safu wima (upana + safu + wima).
·
Default search engine >
injini tafuti-msingi (injini + tafuti + msingi).
·
Com port (communication port) > mlango wa mawasiliano(mlango+wa+mawasiliano).
Muungano;
hii ni mbinu ya kuunganisha maneno mawili au zaidi ili kupata neno moja mbinu
hii pia imetumika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux. Mifano ifuatayo inabainisha
kutumika
kwa mbinu hii:
·
Anonymity >
ufichojina (uficho + jina).
·
Arccosine >
kosinitao (kosini + tao).
·
Backslashes >
mkwajunyuma ( mkwaju + nyuma).
·
Data area >
eneodata (eneo + data).
·
Data bank >
kanzidata (kanzi + data).
·
Data base >
kihifadhidata ( (ki)hifadhi + data).
·
Footnote >
tiniwayo (tini + wayo).
·
Hypertext >
matinifora (matini + fora).
·
Keybody >
baobonye (bao + bonye).
·
Newsgroup >
kundihabari (kundi + habari).
·
Spreadsheet >
lahajedwari (laha + jedwari).
Ukopaji;
njia hii pia imetumika kuunda isuilahi za Kiswahili katika linux. Mifano
ifuatayo inaonyesha kutumika kwa mbinu hii.
·
Account >
akaunti
·
Adapter >
adapta
·
Ampersand > ampasendi
·
Applet
> apuleti
·
Autoformat >
fomati otomati
·
Baud
> baudi
·
Boolean
> buleani
·
Buffer
> bafa
·
Cursor
> kasa
·
Daemon
> dimoni
·
Dial
> dayo
·
Digit
> dijiti
·
Icon
> ikon
·
Kilobyte >
kilobaiti
·
Pixels
> pisel
·
Printer
> printa
Mbinu
hii ya ukopaji imetumika kwa kiasi kikubwa katika uundaji wa istilahi za
Kiswahili zilizopo katika linux.
Mbinu
nyingine iliyotumika kwa kiasi kikubwa katika uundaji wa istilahi za Kiswahili
katika linux ni mbinu ya tafsiri mkopo
(tafsiri sisisi). Tafsiri mkopo nitafsiri ya moja kwa moja kutoka lugha
chanzi. Mifano ifuatayo inathibitisha matumizi ya mbinu hii katika uundaji wa
istilahi za Kiswahili katika linux.
·
Actions menu >
menyu vitendo.
·
Address book >
kitabu cha anwani.
·
Alert me >
nitahadharishe.
·
Auto complete >
kamilisha kiotomati.
·
Boolean operations >
matendo buleani.
·
Certificate manager >
meneja ithibati.
·
Certificate viewer >
kionyeshi hati.
·
Chat group >
kundi sogozi.
·
Colour capability >
uwezo kirangi.
·
Connection failure >
unganisho shinde.
·
Control panel >
paneli dhibiti.
·
Country code >
msimbo nchi.
·
Device manager >
meneja vifaa.
·
Dialogue box >
kisanduku cha mawasiliano.
·
Drag and drop >
kokota na dondosha.
·
Eject
> fyatua.
·
Flow control >
udhibiti wa mtiririko.
·
Word processor >
kichakata matini.
·
Web master >
mtawala tovuti.
Mbinu
nyingine ni mbinu ya kuunda maneno mapya
kabisa mbinu hii imetawaliwa na maneno ya mkopo. Mfano:
·
Icon
> ikoni
·
Italic
> italiki
·
Label
> lebo
·
Megabyte(MB) >
megabaiti(MB)
·
Menu proxies >
menyu proksi
·
Manager
> meneja
·
Pixels
> piseli
·
Program >
programu
·
Scan
> skani.
·
Scanner >
skana
·
Tab
> tabo
·
Tag
> tagi
Mbinu ya ufupishaji
pia imetumika katika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux; hii ni mbinu
inayotumika kufinyanza fungu la maneno na kupata neno moja. Mifano ifuatayo
huonyesha matumizi ya mbinu hii:
·
Alt(alternate) >
Kbdl (kibadala)
·
BSS (Bulletin Board Service) >
HUM (Huduma za Ubao wa Matngazo)
·
Ctrl (ontrol) >
Kdbt (kidhibiti)
·
ESC (escape) >
Epa (epuka)
·
FAQ (frequently asked quetions) >
MYM (Maswali Yaulizwayo Mara kwa mara)
·
FTP (file transfer protocol) >
IKF (Itifaki ya Kuhawalisha Faili)
·
FYI (For Your Information) >
KTY (Kwa Taarifa Yako)
·
Megabyte (MB) >
megabaiti (MB)
·
Ref: > Yah:
·
Re: > Jb:
·
TCP (Transfer Control Protocol) >
IKU (Itifaki ya Kudhibiti Urushaji)
·
URL (Uniform Resource Location) >
KISARA (Kioneshi Sanifu Rasilimali)
·
WWW (World Wide Web) >
WWW (Wavu Wa Walimwengu)
Uhulutishi
ni mbinu pia liyotumika katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux, mbinu hii hutumika katika uundaji
wa istilahi kwa kuunganisha sehemu za maneno na kuunda neno moja. Mbinu hii
imetumika kwa kiasi kidogo sana, rejea mifano ifuatayo:
·
Bitmap
> taswidoti ( (taswi)ra +
doti)
·
Multimedia >
medianuwai ((medi)a + anuwai)
Mbinu
nyingine iliyotumika katika uundaji wa istilahi za kiswahili katika linux lakini kwa kiasi kidogo sana ni
ile mbinu ya upanuzi wa maana za maneno,
upanuzi wa maana za maneno ni kuongezea maana maalumu za kihistilahi katika
maneno ya Kiswahili. Mfano:
·
Mouse >
puku
Puku
kwa maana ya kawaida ni panya pori lakini hapa limepewa dhana mahususi katika
kompyuta kwa maana ya kifaa kinachotumika katika utumiaji wa kompyuta.
Utemaji
(clipping) ni mbinu pia iliyojitokeza kwa kiasi kidogo sana, kwa kutumia mbinu
hii istilahi huundwa kwa kukata sehemu ya neno na sehemu ya neno itakayobaki
hutumika kama istilahi. Mfano: key (on keyboard) >
kibonye ( kutoka neno bonyeza na kuongeza kiambishi cha ngeli ya saba
ki-).
Kwa
hiyo hizi ndizo mbinu zilizobainika kutumika katika uundaji wa istilahi za
Kiswahili zilizoingizwa katika mfumo wa kompyuta wa linux.
2.3 Ubora na udhaifu wa mbinu
zilizotumika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux.
2.3.1 Ubora wa mbinu zilizotumika.
Kwa
kiwango kikubwa mbinu zilizotumika zimezingatia misingi na kanuni za uundaji
istilahi. Kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko (2008) wanabainisha kuwa
misingi mahususi
katika
uundaji wa istilahi ni pamoja na: Uangavu wa wa istilahi iliyoundwa yaani
istilahi ziakisi sifa bainifu za dhana zinazoziwakilisha. Mbinu zilizotumika
katika uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux kwa kiasi kikubwa
zimezingatia msingi huu. Kwa mfano:
Ufikio >
accessing, ingizo >
input, alamisha >
bookmark.
Istilahi
hizi zinaonyesha wazi dhana zinazowakilishwa, kwa mfano, alamisha inabeba dhana
ya kitendo cha kuweka alama hivyo kwa
msingi huu inadhihirisha mbinu zilzotumika ni bora. Vilevile mbinu zilizotumika
zimezingatia msingi wa uundaji istilahi unaosema, istilahi sharti ziwe na uwezo
mkubwa wa kunyambuliwa na kuunda istilahi nyingine za kikoa au ukanda
unaohusika. Msingi huu umefuatwa katika kuunda istilahi za kwenye linux, kwani istilahi nyingi zilizoundwa
zina uwezo wa kunyambulishwa. Mfano:
·
Add
> ongeza
·
Add-on
> nyongeza
·
Alert(n) >
thadhari
·
Alert(v) >
tahadharisha
Pia
uundaji wa istilahi za kwenye linux
umezingatia msingi wa uundaji istilahi unaosema,uwakilishi wa istilahi moja kwa
dhana moja. Msingi huu umezingatiwa kwa kiasi kikubwa kwani istilahi takribani
zote huwakilisha dhana moja isipokuwa zile zilizoundwa kwa kupanua maana ambazo
ni chache sana.
Mfano:
configuration > usanidi
Configuration file >
faili sanidi
Vilevile
mbinu zilizotumika ni bora kwani hazijatumia kwa kiasi kikubwa mbinu za
uhulutishi na mbinu ya kupanua maana ya maneno yaliyopo, hii ni kwa sababu
misingi ya uundaji wa istilahi za Kiswahili husisitiza kuepuka matumizi ya
mbinu hizi; hii ni kwa kuwa istilahi zinazo uundwa kwa mbinu ya uhulutishi huwa
na uvulivuli wa maana na kufanya kuwa ngumu kukumbukwa na kutumiwa. Pia uundaji
wa istilahi kwa kupanua maana ya maneno yaliyopo husababisha watumiaji wa
istilahi hizi kushindwa kutofautisha maana zake za kawaida na zile za
kihistilahi.
Mbinu
za uundaji istilahi za Kiswahili katika linux, pia zimezingatia msingi wa
uundaji wa istilahi za Kiswahili unaosema, istilahi sharti ziwe fupi na zenye
kueleweka. Istilahi nyingi zimeundwa kwa kuzingatia msingi huu.
2.3.2 Udhaifu wa mbinu zilizotumika
Katika
uundaji wa istilahi za Kiswahili za kwenye linux,
kuna baadhi ya mbinu zilizotumika zinazoonyesha kuvunja kanuni na misingi ya
uundaji istilahi. Kwa mfano kuna istilahi zilizoundwa kwa kukiuka msingi wa uundaji
istilahi unaosema, istilahi sharti ziwe fupi na zenye kueleweka. Kuna baadhi ya
istilahi ambazo ni ndefu na hivyo kukiuka huu msingi. Mfano:
·
Allow popup from this site >
ruhusu udukizi kutoka tovuti hii
·
Com port > mlango wa mawasiliano
Istilahi
hizi zimeonekana kuwa ndefu kwa sababu mbinu iliyotumika ni ya mwambatano wa
maneno, na kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko wanasema, “iwapo istilahi
zitaundwa kwa kutumia mbinu za muungano na mwambatano wa maneno basi mambo
yafuatayo itabidi yazingatiwe”:
i.
Idadi ya maneno yanayounganishwa au
yanayoambatanishwa yafaa yasizidi mawili.
ii.
Vistari visitumike kutenga istilahi
ambatani kwani katika Kiswahili istilahi za namna hii hutamkwa kama neno moja
lenye mkazo mkuu kwenye silabi moja tu.
iii.
Istilahi za namna hii yafaa zisiwe na
silabi zaidi ya nane kwani kwa kawaida maneno ya Kiswahili yanawastani kati ya
silabi moja na tano tu. Kwa msingi huu mifano ya itilahi zilizotolewa hapo juu
zimeundwa na maneno zaidi ya mawili na silabi zaidi ya nane. Mfano ; mlango wa
mawasiliano (silabi 10), ruhusu udukizi kutoka tovuti hii (silabi 15) na hivyo
huu ni udhaifu uliojitokeza.
Vilevile
matumizi ya mbinu za uhulutishi na upanuzi wa maana ya maneno yaliyopo
zimetumika, huu ni udhaifu kwani misingi ya uundaji wa istilahi za Kiswahili
inasema, mbinu ya
uhulutishaji
iepukwe kwani etimolojia yake ina uvulivuli na uundaji wa istilahi kwa kupanua
maana ya maneno yaliyopo yafaa uepukwe kwani istilahi za namna hii
zinawakanganya wengi hasa zinapotumika nje ya muktadha au kwenye taaluma zenye
mahusiano ya karibu.
Mifano
ya istilahi zilizoundwa kwa uhulutishaji ni:
·
Taswidoti >
bitmap
·
Medianuwai >
multimedia
Na
mfano wa istilahi iliyoundwa kwa upanuzi wa maana ya neno ni:
Puku >
mouse. Puku ni istilahi iliyopanuliwa maana ambapo maana yake ya kawaida
ni panya pori lakini maana yake maalumu ni kifaa kinachotumika katika utumiaji
wa kompyuta.
Kwa
hiyo huu ndio udhaifu wa istilahi zilizotumika katika uundaji wa istilahi za
Kiswahili katika linux.
2.3.3 Mbinu bora zaidi katika
uundaji wa istilahi za Kiswahili.
Kulingana
na utafiti huu mbinu zilizoonekana kuwa bora zaidi na ambazo zinatumika sana
katika uundaji wa istilahi za Kiswahili ni pamoja na, unyambulishaji, ukopaji,
mwambatano, muunganiko pamoja na tafsiri mkopo. Mbinu hizi zimeonekana kuwa bora
katika uundaji wa istilahi za Kiswahili kwa sababu zinaruhusu uundaji istilahi
kwa wingi iwezekanavyo na mbinu hizi huzingatia misingi ya uundaji istilahi za
Kiswahili. Misingi hiyo ni pamoja na ufaavu wa kiisimu, uwekevu wa kiisimu,
unyambulifu , uwakilishi wa istilahi moja kwa dhana moja, udhahiri na
utoshelevu pamoja na uangavu. Mbinu hizi huakisi kwa kiasi kikubwa misingi hii
na hivyo kupendekezwa na waunda istilahi katika uundaji wa istilahi za Kiswahili.
SURA
YA NNE
Muhtasri na Hitimisho
4.1 Matokeo ya utafiti kwa
muhtasari
Utafiti
huu umeongelea malengo matatu. Kwanza utafiti huu umebainisha mbinu za uundaji
istilahi zilizotumika katika linux. Pili utafiti umepambanua ubora na udhaifu
wa mbinu za uundaji istilahi za Kiswahili zilizotumika katika linux. Tatu
umebainisha mbinu bora zaidi katika uundaji wa istilahi za Kiswahili.
Utafiti
huu umeonyesha kuwa mbinu kumi za uundaji istilahi za Kiswahili zimetumika
katika istilahi za linux. Mbinu hizo ni pamoja na:
Unyambulishi;
mifano ya istilahi zilizoundwa kwa mbinu hii ni kama vile:
·
Ufikio
> accessing
·
Utengaji >
allocation
·
Alamisho >
bookmark link
·
Ingizo
> input
Muungano wa maneno;
mifano ya istilahi zilizoundwa kwa mbinu hii ni pamoja na:
·
Ufichojina >
anonymity
·
Mkwajunyuma >
backslashes
·
Kanzidata >
databank
Ukopaji;
mbinu hii pia imetumika katika kuunda istilahi za kwenye linux. Mfano:
·
Akaunti >
account
·
Apuleti >
applet
·
Dayo
> dial
Tafsiri mkopo (tafsiri sisisi);
mifano ya istilahi zilizoundwa kwa kutumia mbinu hii ni:
·
Menyu vitendo >
actions menu
·
Meneja ithibati >
certificate manager
·
Paneli dhibiti >
control panel
Mwambatano; mbinu hii vilevile imebainishwa kutumika
katka uundaji wa istilahi za Kiswahili katika linux:
Mifano: Rangi usuli >
background color
Orodha tobwe >
bullet list
Thamani upenyo >
aperture value
Kuunda maneno mapya kabisa;
mbinu hii pia imetumika. Mfano.
·
Ikoni
> icon
·
Italiki >
italic
·
Menyu proksi >
menu proxies
Ufupishaji;
katika utafiti huu mbinu hii pia imetumika. Mfano:
·
Kbdl (kibadala) >
Alt (alternative)
·
Kdbt (kidhibiti) >
Ctrl (control)
·
Epa (epuka) >
Esc (escape)
·
KISARA (Kioneshi Sanifu Rasilimali
) > URL (Uniform Resource Location)
Uhulutishi;
mbinu hii pia imetumika. Mfano:
·
Taswidoti >
bitmap
·
Medianuwai >
multimedia
Upanuzi wa maana;
mfano, puku (panya pori) > mouse.
Utemaji (clipping);
mbinu hii pia imetumika. Mfano, kibonye
> key (on keybody).
Kwahiyo
hizi ndizo jumla ya mbinu zilizo tumika kuunda istilahi za Kiswahili katika linux.
Matokeo
ya utafiti huu yanaonyesha mbinu zilizotumika ni bora kwa kiasi kikubwa hii ni
kutokana na sababu kwamba, mbinu zilizotumika zimezingatia misingi na kanuni za
uundaji istilahi kwa kiasi kikubwa. Lakini vilevile baadhi ya mbinu za uundaji
istilahi zimetumika
ambazo kwa mujibu wa misingi ya uundaji
istilahi hazifai kutumiwa katika mchakato wa uundaji wa istilahi za Kiswahili.
Mbinu hizi ni pamoja na uhulutishi na upanuzi wa maana ya maneno yaliyopo.
Pia
utafiti huu umebainisha mbinu bora katika uundaji wa istilahi za Kiswahili kuwa
ni unyambulishaji, muungano wa maneno,
uambatishi, mkopo pamoja na tafsiri mkopo. Hii ni kwa sababu mbinu hizi
huzingatia misingi ya uundaji wa istilahi za Kiswahili kwa kiwango kikubwa.
3.2 Hitimisho
Katika
mchakato wa uundaji wa istilahi za Kiswahili kuna misingi ambayo hainabudi
kufuatwa. Ili kuunda istilahi zilizobora mwanahistilahi hanabudi kuzingatia
misingi hii.
Kwa
mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko (2008) wanasema kuwa ili kuinua ubora wa
istilahi za Kiswahili waundaji istilahi wanasisitizwa kuzingatia mambo matatu
muhimu. Kwanza wanasisitizwa kwa kadri iwezekanavyo wafuate kwa makini kanuni
na taratibu za uundaji istilahi za Kiswahili. Kwa kufanya hivi itawezesha kwa
kiwango kikubwa kuundwa istilahi za Kiswahili zenye kulandana vizuri kisarufi.
Pili
waundaji istilahi wanahimizwa kuachana na mtindo wa kuunda istilahi moja moja
kukidhi mahitaji yao ya istilahi ya papo kwa papo kwani mtindo huu unasababisha
uundaji wa istilahi zisizo na mtiririko na
utimilifu wa kuridhisha. Kwa kuwa dhana zinazo wakilishwa na istilahi
kwa kawaida huwa hazikai pweke pweke bali hukaa kama seti au mifumo maalumu,
basi ni vema uundaji istilahi ufuate vilevile mifumo hiyo ya kidhana. Kulingana
na maelezo haya kinachosisitizwa ni uundaji wa istilahi kwa kuzingatia mifumo
ya kidhana. Kwa mujibu wa Tumbo-Masabo na Mwansoko (wameshatajwa) wakimnukuu
Mkude (1989:34) wanasema,
uundaji
wa istilahi kwa kuzingatia mfumo wa kidhana unafaida kuu nne:
(i) Utawasaidia
waunda istilahi kuonyesha wazi mantiki ya uhusiano baina ya istilahi za ukanda
mmoja.
(ii) Utawahimiza
waunda istilahi kubainisha vizuri zaidi tofauti ndogondogo lakini muhimu baina
ya istilahi zinazokaribiana.
(iii) Utawasaidia
kutambua haraka mapengo katika nasaba au upungufu katika maelezo.
(iv) Utawasaidia
waunda istilahi kuona haraka ni istilahi zipi zitaweza kuathiriwa upesi iwapo kutatokea mabadiliko katika istilahi moja
wapo.
Hivyo
utaratibu wa uundaji istilahi kinasaba ukitumiwa utaepusha uundaji wa istilahi
zinazogongana na zisizo na mtiririko wenye mantiki.
Jambo
la tatu kama ilvyoainishwa na Tumbo-Masabo na Mwansoko ni kwamba uundaji wa
istilahi haunabudi kuzingatia tofauti za watumiaji, mathalani viwango vyao vya
elimu, mazingira yao na kadhalika. Kwa hali hii ili kuhakikisha istilahi bora
za Kiswahili zinaundwa ni muhimu hadhira mahususi za watumiaji istilahi
ziainishwe na istilahi ziundwe kufuatana na viwango vya elimu ya watumiaji
lengwa. Ni kwa kufanya hivyo dhana kama vile istilahi angavu au istilahi zenye
uvulivuli zitakuwa na maana halisi kwani zitahusishwa na vikundi mahususi vya
watumiaji istilahi.
Na Aritamba Malagira.
Haki zote zimehifadhiwa.
MAREJEO
Kahigi,K.K
(2004).Ujanibishaji wa office na windows
xp kwa Kiswahili sanifu katika
http//ajol.info.
Kiango,J.G
(2004). Uundaji wa msamiti mpya katika
Kiswahili: Zoezi lenye njia mbalimbali
katika Kiango.htm.
King’ei,
K (2010). Misingi ya isimujamii. Dar
es salaam. Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
Msanjila,Y.P,
Kihore,Y.M na D.P.B Massamba (2011). Isimujamii
sekondari na vyuo.
Dar es salaam. Taasisi ya
Uchunguzi wa Kiswahili.
Samson,
H.R (1988). Ufundi wa magari, mfano wa
ukuzaji wa istilahi za Kiswahili katika
Mulika na.21. Dar es
salaam. Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili.
Sewangi,S.S
(2004). Maana katika uundaji wa istilahi
katika Sewangi,pdf.
Tumb-Masabo,Z.N.Z
na Mwansoko,H.J.M (2008). Kiongozi cha
uundaji istilahi za Kiswahili.
Dar es salaam. Taasisi
ya Uchunguzi wa Kiswahili.
17 comments:
kazi nzuri sana shukrani
Asante sana! Karibu Katika blogu hii, kama una kitu tunaweza kushirikiana.
Asante sana ndugu. Tafadhali nieleze kwa kifupi tu upungufu wa mbinu za ufupishaji wa maneno.
sadakta mwana kaka
Karibu sana!
kazi nzuri sana, kwa hilo nakupa kongole
Basi nisipotoa shukurani nitakuwa ni mkorofi wa aina gani? Kwa kweli sana maneno halisi ya kutumia kwa kuonyesha furaha yangu kwa utafiti huu hapa. Ahsante sana ndugu.
Je, kuna tofauti kati ya unyambulishaji na uambishaji??
Habari,
Nisaidie tafsiri ya neno BRAND
hodi ni wewe katika haraka haja mkopo kulipia kuanza yako madeni ya kuanzisha biashara au nyumba ??? Kisha inakuja teksi kampuni una imani na relay juu ya 100% uhakika sababu hii ni kampuni ambapo i cashed mkopo wangu kwa mama yangu Stella dawa leo ili kuwasiliana na René Mikopo Firm halisi kupimwa na kuaminiwa na leo mimi nina furaha i got mkopo wangu wa $ 120,000 leo ili kupata kushikamana leo mrsstellareneloanfirm@hotmail.com} {barua pepe hapa chini na kupata jibu la matatizo yako yote kwa sababu Siwezi Kunyamaza ushuhuda huu mkubwa peke yangu binafsi ili i aliamua kuandika kwenye tovuti kwa sababu kula furaha kubwa kwa yangu moyo na leo mimi nina kuishi maisha mapya shukrani kwa wote Stella René
kolochatechee
Nakupa kongole kwa kazi nzuri. Katika utafiti wako nimeona maneno haya yamechangaywa kidogo, Je Mause ni punu au crop ndio punu? Kuna mahala umeita mouse=Punu na kuna mahala umeita Crop=Punu. Ufafanuzi please.
Habari ndugu,
Nadhani hukuangalia vizuri maneno hayo "Mouse" na "Crop" tofauti zake zimewekwa bayana. "Mouse" ni "Puku" na "Crop" ni "Puna".
Niko hapa kutoa ushuhuda kubwa Nimejaribu michache ya jukwaa wengine wote katika kutafuta nzuri kampuni mkopo ambayo itasaidia yangu kwa mkopo kwa bahati mbaya kwa ajili yangu mimi kukutana 3 mkopo kampuni waliokuwa tu baada ya kile mimi naweza kuwapa na si kusaidia me walichukua fedha kutoka kwangu na hamkunipa majibu yoyote chanya wote I got ilikuwa hadithi. Kisha mimi nikajikuta uchapishaji kutokana na huduma mkopo na tu aliamua Email na kusikia kile got kusema lakini basi mimi aligundua kwamba wao alizungumza vizuri na akapiga halisi mimi kufundishwa kuhusu hilo na akawapa kesi hiyo. Hatimaye I got mkopo masaa 24 tu baada ya mazungumzo kama kwamba alikuwa si wote mimi got kukutana mkopo katika akaunti yangu jioni ya pili ya siku mimi aliwasiliana nao. wow! hatimaye kitu kimoja kwamba Ilinichukua miaka ya kupata kutoka kampuni nyingine mkopo pia mimi masaa 24 tu kupata kutoka kwao. Tangu wakati huo mimi tumeamua kusaidia Msemaje na kutangaza yao kwa watu ambao kukutana kuwa katika viatu nilikuwa au kwa watu ambao wanahitaji huduma hapa ni pale kampuni pepe: diamondloancompany01@yahoo.com kuwapa kesi na kumshukuru mimi baadaye hawana hata kujua nafanya hivyo. njia tu kidogo ya kusema Asante.
kazi nzuri
Kazi safi nimeelewa zaidi endelea!
Post a Comment