Sunday, December 9, 2012

TAFSIRI KATIKA KISWAHILI



Tafsiri ni taaluma ya lugha ambayo imefuata taaluma ya ukalimani, ni taaluma iliyoanza baada ya ugunduzi wa maandishi. Tafsiri za mwanzo kabisa ni zile zilizohusu maandiko ya kiyahudi, kwa mfano tafsiri ya kwanza kufanyika katika nchi za magharibi ni ile ya tafsri ya maandiko ya kiyahudi yaliyotafsiriwa katika lugha ya kigiriki cha koine kati ya karne ya 3 na ya 1 kabla ya kristo.

Maana ya tafsiri.

Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia, tafsiri ni mawasiliano ya maana iliyokatika matini ya lugha chanzi kwa njia ya kuweka maana inayolingana katika matini ya lugha lengwa.
Naye Mwansoko (2006) anasema tafsiri ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi nyingine.
Kihore (1989) anafasili tafsiri kama jaribio la kuhawilisha ujumbe katika maandishi kutoka lugha moja kwenda nyingine.
Kwa ujumla fasili hizi zote ni nzuri kwani zote zimeonesha kuwa tafsiri hufanyika katika maandishi. Kwa hiyo tunaweza kusema kuwa tafsiri ni zoezi la uhawilishaji wa maana, mawazo, dhana au ujumbe ulio katika maandishi kutoka lugha chanzi na kuweka badala yake maana, ujumbe, mawazo au dhana inayolingana na ile ya lugha chanzi katika lugha lengwa.

Dhima ya tafsiri.

Tafsiri kama taaluma ya lugha ina majukumu kadhaa ya kuyashughulikia, majukumu hayo ni kama yafuatayo:
·         Tafsiri ni njia ya mawasiliano baina ya watu wanaozungumza luga tofauti.
·         Tafsiri inatumika kutolea matangazo, mfano, utalii, brosha na kadhalika.
·         Ni kama nyenzo ya kukuza fasihi. Mfano, hadithi ya alfu lela ulela ( siku  elfu moja), treasure island (kisiwa chenye hazina), Robinson Krusoe na kisiwa chake, mabepari wa venisi n.k. waandishi waliweza kuiga mbinu za uandishi na hivyo kuwa na fasihi bora.
·         Ni nyenzo ya kueneza utamaduni, mfano dini za kigeni kama vile ukristo na uislam uliingizwa kwa njia ya tafsiri na ukalimani.
·         Ni nyenzo muhimu ya kujifunza lugha ya kigeni na kujifunza miundo na maumbo ya lugha fulani. Mfano watu wanaofanya utafiti kuhusu luhga fulani hutumia tafsiri kama njia ya kuelezea lugha hizo.
·         Tafsiri humwezesha mtu kujiajiri (kama chanzo cha ajira). Mfasiri anapofanya kazi ya kufasiri anapata pesa na hivyo hizo pesa humsaidia katika maisha yake ya kila siku.
·         Ni kama njia ya kukuza lugha; msamiati mwingi huingia katika lugha lengwa na hivyo kuitajirisha.

Sifa za mfasiri.

Ili mtu kuitwa mfasiri anatikwa awe na sifa zifuatazo:
·         Awe anamudu vizuri sarufi za lugha zote mbili anazofanyia kazi.
·         Awe ana ufahamu wa kutosha juu ya utamaduni wa lugha chanzi.
·         Awe ni mtumiaji mzuri wa kamusi na marejeo mengine muhimu.       
·         Awe na uwezo mkubwa wa kuandika katika lugha chanzi.
·         Angalau awe na ujuzi wa kutumia kompyuta.


Mambao ya kuzingatia wakati wa kutafsiri.

Kuna mambo muhimu ambayo mfasiri anatakiwa kuyazingatia katika kufasiri matini, mambo hayo ni kama yafuatayo:
a)   Mfasiri atalazimika kusoma matini yote kabla hajaanza kufasiri. Atalazimika kufanya hivyo ili kufanya yafuatayo:
·         Ili aweze kuelewa kinachozungumzwa – ujumbe uliomo.
·         Aweze kuandaa marejeo muhimu anayohitaji k.v. kamusi, vitabu n.k.
·         Ili aweze kubaini aina ya matini.
·         Ili aweze kubaini matatizo yanayojitokeza katika matini husika na kuweza kuyatatua matatizo hayo, mfano; matatizo ya kitahajia tungo ambazo hazijakamilika n.k.
·         Ili kusaidia kuigawa kazi; kama ni kazi ndefu anaigawa katika vipande fulanifulani hasa kama kazi ni ya watu wengi.

No comments: