Wednesday, December 25, 2013

JINSI MWANDISHI WA KAZI ZA FASIHI ZA WATOTO NA VIJANA ANAVYOPASWA KUZINGATIA SAIKOLOJIA YA WATOTO NA VIJANA: UCHAMBUZI KUTOKA KATIKA KITABU CHA MWENDO.



Fasihi ni sanaa kama zilivyo sanaa zingine, mvuto ni kitu cha msingi sana katika sanaa. Fasihi ya watotona vijana pia kama sanaa ni muhimu pia kuzingatia kipengele hiki. Kwa mantiki hii, mwandishi ili aweze kufanikisha kuiteka saikolojia ya watoto na vijana katika kazi yake ni lazima ahakikishe kazi hiyo inamvuto kwa watoto. Dhana ya mvuto katika fasihi ya watoto na vijana inahusisha vipengele kadhaa, kabla ya kuangalia vipengele hivi kwa kina ni vema tukafasili dhana muhimu zinazojitokeza katika swali. Dhana hizo ni pamoja na Fasihi ya watoto na vijana na dhana ya saikolojia ya watoto na vijana katika kazi za fashi. Baada ya kuangalia dhana hizi kwa kina ndiposa tutahusianisha na riwaya ya “Mwendo”.

Kwa mujibu wa Wamitila (2003) Fasihi ya watoto ni fasihi maalum inayoandikwa kwa ajili ya watoto.

NOUN (2010) Wanasema Fasihi ya watoto ni dhana inayorejelea fasihi inayowalenga watoto pekee. Wanaendelea kusema, Fasihi ya watoto huweza kuwa hadithi, ushairi, visakale, drama ambazo zimetungwa kwa ajili ya watoto wadogo na vijana. Vilevile wanaongezea kusema kuwa Fasihi ya watoto inajikita katika mambo makuu matatu, jambo la kwanza ni endapo mhusika mkuu ni mtoto au kijana, dhamira inayowahusu watoto na lugha rahisi na Fasihi ya watoto inakuwa fasihi ya watoto endapo tu wazo na dhamira inahusiana na urahisi wa lugha.

Fasili zote hizi,zinatupa mwanga hasa juu ya dhana ya fasihi ya watoto na vijana, vitu vya msingi ni kwamba fasihi hii ni lazima iwe na dhamira pamoja na lugha rahisi. Hivyo basi, tunaweza kusema kuwa, fasihi ya watoto na vijana ni sanaa itumiayo lugha kwa lengo la kufikisha ujumbe kwa hadhira iliyo chini ya umri wa miaka kumi na minane (18).

Dhana ya saikolojia ya watoto na vijana tunaweza kusema ni yale mambo ambayo yanatakiwa kuzingatiwa katika kazi za Fasihi ili kumvutia mtoto na kijana. Sigh na wenzake (2002) wanasema Fasihi ya watoto na vijana lazima iwe inaonesha matendo na maisha ya mhusika kinaganaga, mhusika awe anatia hamasa na lazma iwe inaburudisha.

Kwa ujumla saikolojia ya watoto na vijana katika kazi za fasihi hulenga yale mambo ambayo ni lazima yawepo katika kazi hiyo ili kuwavutia watoto na vijana. Kwa hiyo ili mwandishi afanikiwe kuiteka saikolojia ya watoto na vijana ni sharti azingatie mambo hayo, mambo hayo ni pamoja na haya yafuatayo:

Kazi hiyo ni lazima iwe na mtazamo wa watoto, watoto na vijana wanafikiri tofauti na watu wazima, hivyo mwandishi akiandika kazi inayoendana na fikra zao atakuwa amefanikiwa kuiteka saikolojia yao.

Kazi iwe na lugha rahisi inayoendana na hadhira ya watoto na vijana, miundo migumu na sentensi ngumu hazipendekezwi kutumika katika fashi ya watoto na vijana isipokuwa kama kuna ulazima wa kufanya hivyo.

Pia mwandishi anapaswa kuandikia mada inayowavutia watoto na vjiana, kwa mfano watoto wengi wanapenda kazi zinazosimulia juu jasura, safari na kadhalika kwa hiyo mwandishi akiandika juu ya mada hizi atakuwa amefanikiwa.

Vilevile mwandishi anapoandikia hadhira ya watoto na vijana ni lazima hadithi yake iwe fupi na ya kiutendaji kwani kazi ndefu huwachosha watoto na hivyo huweza kupoteza mvuto kabisa kwa watoto.

Mwandishi anapowachora wahusika wake ni lazima kuwe na mhusika mwema na mhusika mwovu, kwani hali hii huwavutia sana watoto.

Katika kazi za fasihi ya watoto, wahusika kama wanyama wapewe uhai, hii huwavutia sana watoto.
Pia kazi za fasihi za watoto na vijana sharti ziwe na michezo kwani watoto hupenda sana michezo.

Kazi iwe na picha tena za rangi, hii huwafanya watoto kutosahau kwa urahisi kile walichosoma lakini pia huwasaidia kuhusisha matukio katika hadithi na ulimwengu halisi.

Taharuki na fantasia pia ni vitu muhumu katika kazi za watoto, fantasia huleta mvuto wa pekee katika kazi za watoto na hivyo kufanya watoto wengi kufurahia sana kazi ambazo zina fantasia.

Kwa hiyo haya ndio mambo muhimu ambayo kila mwandishi wa kazi za watoto na vijana anapaswa kuyazingatia pale anapotunga kazi inayowalenga watoto na vijana kinyume na hapo watoto na vija huweza kutoipenda kazi yake.

Baada ya kuangalia vipengele muhimu vinavyopaswakujitokeza katika kazi ya watoto na vijana sasa ni wakati wa kuangalia jinsi vilivyozingatiwa katika riwaya ya “Mwendo.”

“Mwendo” ni riwaya iliyoandikwa na Elieshi Lema na kuchapwa na E&D mwaka 1998, ni riwaya inayohusu mila na tamaduni za kimakonde kwa kuangalia jinsi mila hizi zinavyomwandaa mtoto kukabiliana na mabadiliko yanayojitokeza katika makuzi yake. Kwa ujumla riwaya hii inahusu mabadiliko katika makuzi ya mtoto hususani wa kike.

Mwandishi wa riwaya hii amejitahidi kuzingatia mambo muhimu katika utunzi wafasihi ya watoto na vijana ambayo huathiri saikolojia ya watoto na vijana katika kazi ya fasihi. Vipengele alivyojaribu kuvizingatia mwandishi wa riwaya hii ni pamoja na hivi vifuatavyo:

Kwa kiasi kikubwa mwandishi amezingatia kipengele cha picha. Picha katika riwaya hii zimejitokeza kwa kiasi kikubwa sana na picha zilizotumika zinaendana na kile kinachosimuliwa. Kwa mfano picha nyingi zinaonesha utamaduni wa kimakonde wa kuchonga vinyago; na hivyo mtoto au kijana anaposoma riwaya hii anakuwa anavutiwa na hizi picha kwa hiyo anapata ujumbe kwa urahisi, hii inamfanya mtoto apende kuendelea kusoma riwaya hii.

Mhusika mkuu ni mtoto, mwandishi amemtumia Felisia kama mhusika mkuu. Felisia ni mtoto ambaye anasoma darasa la saba mwandishi amemtumia kuwakilisha watoto wengine ambao wanaumri kama  wake na ambao wanahitaji kujua hatua za makuzi yao. Kwa hiyo kazi alizopewa Felisia kama mhusika mkuu zinasadifu uhusika wake kama mtoto. Wahusika wengine watoto ni Hamiata, Bene na wanafunzi. Kwa hiyo mtoto atakapoona  kuwa wahusika wakuu katika riwaya hii ni watoto wanaweza kushawishika kusoma kazi hii.

Wazo kuu la riwaya linawalenga watoto, hiki pia ni kipengele muhimu sana katika utunzi wa fasihi ya watoto na vijana kama wazo kuu haliwalengi watoto na vijana ni hakika kazi hiyo haitapokelewa vema. Katika riwaya hii mwandishi ameonesha ni jinsi gani watoto wanavyopata changamoto katika makuzi yao hususani watoto wa kike, kwa hiyo amefanikiwa katika kipengele hiki.

Vilevile katika riwaya hii mwandishi ametumia lugha ambayo ni rahisi kueleweka, miundo ya sentensi sio migumu pia vielevile msamiati mgumu au misemo migumu haikutumika katika riwaya hii. Kwa msingi huo mtoto hatapata ugumu wowote anaposoma riwaya hii na hivyo atapenda kuendelea kuisoma.

Pia mhusika mkuu (Felisia) amechorwa vizuri; watoto wanapenda mhusika mkuu achorwe vizuri, mwandishi wa riwaya hii amefanikiwa kufanya hivyo kwani amemchora Felisia kama mhusika shujaa na  mwema, baada ya kupitia vikwazo mbalimbali kwa mfano, kuzuiwa kuendelea na masomo lakini tunaona mwishoni anafanikiwa kurudishwa darasani na anashangiliwa na wanafunzi wenzake (ukurasa 65). Watoto wanapenda hali kama hii ionekane katika kazi zao.

Taharuki imetumika katika riwaya hii. Taharuki ni chombo muhimu sana katika fasihi ya watoto na vijana, taharuki inamfanya msomaji wa hadithi aendelee kusoma ili ajue kile kinachofuatia. Katika riwaya hii taharuki zinazoonekana ni pale ambapo Felisia alionekana kukata mawasiliano ghafla na rafiki yake Hamiata (ukurasa 3 na 4), mwandishi hakuonesha sababu yoyote hivyo kumfanya msomaji kuendelea kusoma ili kujua kilichompata Felisia.Taharuki nyingine ni pale ambapo Felisia alifungiwa ndani kwa muda wa mwezi mmoja, akiwa ndani alijiuliza maswali juu ya nini kitakachofanyika siku ya kuchezwa unyago, alijiuliza huwenda atakeketwa na kutoka damu au ni kitu gani kitakachofanyika. Hivyo katika hali kama hii taharuki hutokea na kumfanya msomaji aendelee kusoma ili kujua nini kitakachotokea.

Matumizi ya fantasia pia yameonekana katika riwaya hii. Katika (ukurasa wa 14) kuna hadithi inayosimulia juu ya mwanamme akitembea juu ya nyayo lakini cha kushangaza anasikia nyayo zinaonge, “aaah, mbona unanikanyaga sogea kando”. Kwa hiyo hii ni fantasia ambayo humfanya mtoto aifurahie riwaya hii anapokuwa anasoma. Fantasia nyingine inapatikana (ukurasa 20) hapa tunaona matukio ya ajabu, kitendo cha mwanamke kuongea na mzimu na kisha kuilekeza njia sio jambo la kawaida katika ulimwengu halisi, hivyo hii pia humfanya mtoto apende kusoma riwaya hii kwa sababu ya maajabuajabu haya.

Kitu kingine kinachowavutia watoto na vijana ni mwisho mzuri wa hadithi. Katika riwaya hii mwandishi amezingatia kipengele hiki. Tunaona mhusika mkuu amefanikiwa kurejea darasani lakini pia tunaona amefanikiwa kuondoa wasiwasi wake baada ya kupata elimu ya makuzi anaonekana kujiamini na anaonekana kuwa tayari kukabiliana na ukubwa. Kwa ujumla riwaya hii imeisha vizuri, Felisia na Hamiata wanaonekana kufurahi. Kwa hiyo mtoto atakaposoma riwaya hii naye atafurahi kwani imeisha kwa furaha na sio kwa huzuni.

Hata hivyo licha ya mwandishi kutumia vipengele muhumu vinavyoteka saikolojia ya watoto katika fashi yao pia ameonesha udhaifu, udaifu huo unajitokeza katika vipengele vifuatavyo:

Riwaya ni ndefu.Watoto hawapendi hadithi ndefu, wanaposoma hadithi na kuona ni ndefu sana huwa wanakata tamaa, na hatimaye huacha kuendelea kusoma.Riwaya hii ina kurasa sabini kwa hiyo ni ndefu sana kwa watoto. Kwa hiyo mwandishi anaonekana kushindwa katika kipengele hiki.

Haina michezo. Watoto wanapenda michezo ionekane katika hadithi zao, hii itawafanya wasichoke kusoma hadithi na hivyo kwa njia hii ujumbe utawafikia kwa urahisi. Katika riwaya hii mwandishi hakuzingatia kipengele hiki.

Vilevile riwaya hii sio ya kiutendaji, imejikita katika masimulizi kwa kiasi kikubwa hali ambayo huwachosha watoto wanapokuwa wanasoma hadithi za namna hii. Kwa hiyo watoto hawatavutiwa na riwaya ya namana hii kwa sababu haina utendaji, wahusika sio wa kiutendaji, hivyo mwandishi ameshindwa katika hili.

Kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa mwandishi wa riwaya hii amezingatia kwa kiasi kikubwa saikolojia ya watoto katika utunzi wake. Matumizi ya fantasia, taharuki,picha, lugha nyepesi na kadhalika ni nyenzo muhimu katika kuvutia watoto kupenda kazi yake. Kwa hiyo riwaya hii sio rahisi kukimbiwa na watoto kwani vipengele vingi  vinavyohitajika katika fasihi ya watoto vimezingatiwa. Hata hivyo wandishi angefanikiwa kabisa kuiteka saikolojia ya watoto endapo riwaya ingekuwa ya kiutendaji, yenye michezo na fupi, kwa kuwa vipengele hivi havipo mtoto atakapokuwa anasoma riwaya hii atahisi vitu fulani vinakosekana. Kwa hiyo ni vema waandishi wazingatie saikolojia ya watoto na vijana kwa upekee wake wanapokuwa wanatunga kazi za fasihi inayowalenga watoto na vijana.

 MAREJEO
Lema, E. (1998).Mwendo. Dar es salaam: E&D.
NOUN (2010).Children’s Literature. Lagos: National Open University of Nigeria.
Sigh, M.na wenzake (2002). “Heroes and Heroine in Children’s Literature around the world”                   katika http://www.ericdigests.org/2004-1/heroes.htm 17.05.2012, 12:24. 
Wamitila, K.W. (2003).Kamusi ya Fasihi, Istilahi na Nadharia. Nairobi: Focus Publication.

No comments: