HISTORIA YA KISWAHILI
Kwa kuwa msamiati mwingi uliopo katika lugha
ya Kiswahili unatokana na lugha ya kiarabu ni dhahiri kuwa lugha hii inatokana
na kiarabu. Jadili.
Mjadala kuhusu asili ya Kiswahili umejadiliwa
na wataalam mbalimbali na wametumia vigezo mbalimbali kuthibitisha madai yao.
Wapo wanaodai kuwa Kiswahili ni kiarabu, wanaoshadidia dai hili, kigezo
kimojawapo wanchokitumia ni kigezo cha msamiati, kwamba lugha ya Kiswahili ina msamiati
mwingi wa kiarabu na kwa hiyo kwakuwa Kiswahili kina msamiati mwingi wa kiarabu
basi pia Kiswahili ni kiarabu, kwa kweli dai hili halina mashiko. Kabla
hatujaanza kufafanua kwamba kwa nini dai hili halina mashiko ni vema tukaangalia fasili ya dhana muhimu
kama zinavyojitokeza katika swali la mjadala. Dhana hizo ni kama zifuatazo:
‘Istilahi asili,’ kwa mujibu wa Massamba na
wenzake (1999:3) asili ni jinsi kitu au
jambo lilivyotokea au lilivyoanza. Fasili
hii ni nzuri na inajitosheleza kwa maana kwamba jambo au kitu kinaweza kutokea
kibahati kama ilivyo katika lugha au linaweza kuanzishwa.
Msamiati kwa mujibu wa TUKI (2004) ni jumla ya
maneno katika lugha. Fasili hii iko wazi kwamba jumla ya maneno yote katika
lugha ndio huunda msamiati wa lugha husika.
Wataalam wanaodai kuwa Kiswahili ni kiarabu
kwa kutumia kigezo cha msamiati, hoja zao ni kama zifuatazo:
Khalid (2005) anasema kuwa neno lenyewe
Kiswahili limetokana na neno la kiarabu sahil
katika umoja ambalo wingi wake ni sawahili likiwa na maana ya pwani au
upwa. Hivyo kutoka na jina la lugha hii
ya Kiswahili kuwa na asili ya neno la kiarabu sahil hivyo hudai kuwa Kiswahili ni kiarabu.
Khalid anaendelea kusema kuwa Kiswahili kina msamiati
mwingi wenye asili ya kiarabu. Hapa ni baadhi ya mifano ya msamiati wa
Kiswahili wenye asili ya kiarabu kama alivyobainisha Khalid:
Maneno
yanayoonesha muda.
Asubuhi dakika
Wakati alfajiri
Karne alasiri
Magharibi
saa
Maneno
yanayowakilisha namba.
Nusu robo
Sita saba
Tisa ishirini
Thelathini arubaini
Hamsini sitini
Sabini
themanini
Tisini mia
Elfu
Mtandao wa jamiiforum pia wameonesha mifano ya msamiati wa Kiswahili wenye asili
ya kiarabu kama ifuatavyo:
Kiswahili Kiarabu
Dirisha drisha
Karatasi kartasi
Debe
dabba
Samaki
samak
Mustakabali mustakabal
Madrasa madrasa
Lodh (2000:97) naye anasema kiasi kikubwa cha
nomino za Kiswahili zimetokana na mizizi ya maneno ya kiarabu. Mifano ya maneno
hayo ni kama yafuatayo:
Hesabu/hisabu mahisabu/hisabati
Harka harakati
Safiri
- msafiri
Safari
- msafara
Fikiri
- fikara/fikra
Hata hivyo kigezo hiki cha msamiati kina udhaifu;
Massamba (2002) ameonesha udhaifu wa kigezo hiki kuwa ni pamoja na kwamba:
Hakuna ushahidi wowote wa kitakwimu ambao
unaonesha idadi ya maneno ya kiarabu
yaliyopo katika lugha ya Kiswahili yanayoweza kuhitimisha kuwa Kiswahili
ni kiarabu.
Kigezo cha msamiati peke yake hakijitoshelezi
kuelezea kuwa Kiswahili ni kiarabu, walipaswa waangalie vigezo vingine kama
vile kigezo cha kihistoria kwa kuchunguza masimulizi mbalimbali ya kale na
kigezo cha kiisimu; katika kigezo hiki walipaswa kuchunguza fonolojia,
mofolojia , na sintaksia ya Kiswahili kwa kulinganisha na kiarabu na ndipo
wangepata hitimisho sahihi la madai yao.
Vilevile kigezo hiki cha msamiati hakina
mashiko kwa sababu lugha ina tabia ya kuathiriana, lugha huathiriana na lugha
nyingine endapo kutakuwa na mwingiliano baina ya wanajamii lugha hizo. Kwa mfano Kiswahili kimetokea kuathiriana na
kiarabu kutokana na uhusiano uliokuwepo hapo zamani katika biashara kati ya
waarabu na watu wa upwa wa Afrika Mashariki na hii ikapelekea msamiatia wa
kiarabu kuingia katika lugha ya Kiswahili, hivyo kwa hoja hii hatuwezi kusema
Kiswahili ni kiarabu kwa sababu msamiati wa kiarabu unaonekana katika lugha ya
Kiswahili.
Hata hivyo si lugha ya kiarabu tu ambayo
msamiati wake unaonekana katika lugha ya Kiswahili vilevile kunamsamiati wa
lugha zingine za kigeni katika lugha ya Kiswahili kwa mfano, neno lenye asili
ya kireno katika Kiswahili ni kama vile meza,
leso pia yapo maneno yenye asili ya kijerumani kwa mfano schule kwa Kiswahili shule na maneno yenye asli ya kiingereza
ni kama vile mashine, televisheni,
sekondari, redio, kompyuta na maneno mengine yenye asli hiyo. Basi ingekuwa
msamiati wa kigeni kuonekane kwenye lugha fulani huifanya hiyo lugha kuwa na
asili ya lugha ya kigeni basi tungesema pia Kiswahili ni kiingereza kwa sababu tu msamiati mwingi wa kiingereza
unonekana katika Kiswahili.
Pia kigezo hiki kinaonekana kuwa ni dhaifu kwa
sababu hawakufanya utafiti katika nyanja zote za matumizi ya lugha kwa mfano
msamiti unaotumika katika nyanja ya elimu, afya, utamaduni na kadhalika. Kwa
hiyo madai haya yanaonekana kutokuwa na mashiko kwa ufinyu wa utafiti wake.
Kutoka na kigezo hiki cha msamiati kutokuwa na
mashiko kuhitimisha kuwa Kiswahili ni kiarabu, basi hatuna budi kusema kuwa
Kiswahili sio kiarabu bali ni kibantu. Katika kuthibitisha madai haya
tutajikita zaidi katika kigezo cha kiisimu ambacho tunaamini kuwa ni kigezo
pekee kinachoweza kutupatia taarifa sahihi kwani ni kigezo cha kisayansi lakini
pia tutaangalia kwa ufupi vigezo ambavyo vinatoa ushahidi juu ya ubantu wa
Kiswahili ambavyo ni ushahidi wa kihistoria, kiakiolojia na kiethinolojia.
Kigezo hiki cha kiisimu kimetumiwa na wataalam
mbalimbali katika kuonesha ubantu wa Kiswahili Massamba (ameshatajwa) amewataja
wataalam mbalimbali ambao wamehusika na utafiti juu ya ubantu wa Kiswahili,
wataalam hao ni pamoja na Carl Meinhof katika kitabu chake cha Introduction to the phonology of the Bantu
language, Duke (1935 – 1945), Malcom
Guthrie (1967), Dereck Nurse na Thomas Spear (1985). Hawa walijadili ubantu wa
Kiswahili kwa kutumia kigezo cha kiisimu, kihistoria na kiakiolojia.
Kwa kuanza na kigezo cha kiisimu tutaangalia vipengele kama
vile kufanana kwa msamiati wa msingi, muundo wa kifonolojia, muundo wa
kimofolojia, muundo wa kisintaksia mpangilio wa ngeli za majina.
Mizizi ya msamiati wa msingi wa lugha za
kibantu na Kiswahili hufanana kwa kiasi kikubwa, mifano ifuatayo huweza
kuonesha ukweli huu.
Mfano,
Kiswahili
|
Kikurya
|
Kinyiha
|
Kijita
|
Maji
|
Amanche
|
Aminzi
|
Amanji
|
Jicho
|
Iriso
|
Iryinso
|
Eliso
|
Katika mifano hiyo hapo juu tunaona mifano hiyo
hapo juu tunaona kuwa mizizi maji, manche, minzi, manji inafanana kwa kiasi
kikubwa, kwa hiyo huu ni ushahidi tosha kutuonesha kuwa kuna uhusiano wa
kinasaba kati ya Kiswahili na lugha za kibantu.
Pia mofolojia ya Kiswahili na lugha za kibantu
hufanana kwa kiasi kikubwa, yaani mfumo wa maumbo ya maneno ya lugha ya
Kiswahili na lugha za kibatu hufanana. Kwa mfano, namna viambishi
vinavyopachikwa katika mzizi wa maneno hufuata kanuni ileile kama inavyotumika
katika lugha ya Kiswahili yaani viambishi vinaweza kupachikwa kabla au baada ya
mzizi na uwa na uamilifu bayana. Hebu tuchunguze mifano ifuatayo:
Kiswahili
|
Kisukuma
|
Kisimbiti
|
Kinyiha
|
A-na-lim-a
|
a-le-lem-a
|
a-ra-rem-a
|
i-nku-lim-a
|
a-na-chek-a
|
A-le-sek-a
|
a-ra-sek-a
|
a-ku-sek-a
|
Kwa
kuangalia mifano hii utagundua kwamba katika kutenganisha viambishi hufuata
kanuni moja kwamba mahali kinapokaa kiambishi kwa mfano cha njeo, ndipo pia
hukaa kwa upande wa lugha za kibantu, kwa mfano –na- na –ra- katika lugha ya
kisimbiti. Hivyo tunaweza kusema kuwa kuna unasaba baina ya lugha hizi.
Vilevile sintaksia ya lugha ya Kiswahili na
lugha za kibantu hufanana kwa karibu sana. Kwa mfano jinsi ya mpangilio wa
vipashio na kuunda sentensi hufanana yaani mpangilio wa maneno hufuata kanuni
maalum ambazo hufanana katika Kiswahili na lugha za kibantu. Katika Kiswahili
sentesi ina kuwa na pande mbili yaani upande wa kiima na upande wa kiarifu,
katika upande wa kiima kipashio chake kikuu ni nomino na katika upande wa
kiarifu kipashio chake kikuu ni kietnzi. Hii inamaana kwamba katika kuunda
sentensi ni lazima nomino ianze na baadaye kitenzi. Hebu tuangalie mifano
ifuatayo:
Kiswahili
|
Mama / anakula
N (K) T (A)
|
Kijita
|
Mai / kalya
N(K) T (A)
|
Kihehe
|
Mama/ ilya
N(K) T(A)
|
Kihaya
|
Mama / nalya
N(K) T(A)
|
Katika mifano hii tumeona kwamba muunndo wa
kiima-kiarifu katika lugha za kibantu unafanana sana na ule wa Kiswahili yaani
nomino hukaa upande wwa kiima halikadhalika kitenzi hukaa upande wa kiarifu,
kwa hiyo kwa mifano hii tunaweza kusema kuwa lugha ya Kiswahili ni jamii ya
lugha za kibantu.
Pia mfumo wa sauti (fonolojia) wa lugha za
kibantu unafana sana na ule wa Kiswahili, yaani mpangilio wa sauti katika
kuunda silabi, na miundo ya silabi kwa ujumla hufanana. Kwa mfano katika lugha
ya Kiswahili hakuna muundo wa silabi funge yaani silabi ambayo inaishia na
konsonanti, muundo asilia wa silabi za Kiswahili ni ule unaoishia na irabu
vilevile katika lugha za kibantu hufuata muundo wa silabi wazi, yaani silabi
zote huishia na irabu. Mifano ifuatayo hufafanua zaidi:
Kisawhili
|
Baba
|
K+I+K+I
|
Kikurya
|
Tata
|
K+I+K+I
|
Kiha
|
Data
|
K+I+K+I
|
Kijita
|
Rata
|
K+I+K+I
|
Kipare
|
Vava
|
K+I+K+I
|
Tanbihi: K= konsonanti I= irabu.
Kwa mifano hii tunaona kwamba mifumo ya sauti
katika lugha za kibantu hufanana na ule wa Kiswahili, kwa hiyo tunaweza
kuhitimisha kwa kusema kuwa lugha hizi ni za familia moja.
Pia vilevile mfumo wa ngeli za majina katika
lugha ya Kiswahili hufanana sana na ule wa kibantu hususani katika upachikaji
wa maumbo ya umoja na wingi na maumbo ya upatanisho wa kisarufi. Katika lugha
ya Kiswahili viambishi vya umoja na wingi hupachikwa mwanzoni kabla ya mzizi wa
neno, hivyohivyo katika lugha za kibantu. Kwa mfano:
Umoja
|
Wingi
|
|
Kiswahili
|
m-tu
|
wa-tu
|
Kikurya
|
mo-nto
|
abha-nto
|
Kiha
|
umu-ntu
|
abha-ntu
|
Kikwaya
|
mu-nu
|
abha-nu
|
Mifano hiyo hapo juu inadhihirisha wazi kwamba
vipashio vyote vya umoja na wingi hujitokeza kabla ya mzizi wa neno, hivyo ni
dhahiri lugha hizi zina uhusiano wa nasaba moja.
Vilevile katika upatanisho wa kisarufi lugha za kibantu na Kiswahili huelekea kufanana viambishi
vya upatanisho wa kisarufi hususani viambisha vya nafsi.
Kwa mfano:
Kiswahili
|
Mtoto a-nalia
|
Kizanaki
|
Umwana a-rarira
|
Kisukuma
|
Ng’wana a-lelela
|
Kikurya
|
Omona a-rakura
|
Tunaona hapo juu kwamba kiambishi ‘a’ cha
upatanisho wa kisarufi hujitokeza katika lugha zote, hivyo tunashawishika
kusema kuwa Kiswahili kina uhusiano mkubwa na kibantu.
Pamoja na ushahidi wa kiisimu kutupatia
vithibitisho tosha juu ya ubantu wa Kiswahili pia kuna ushahidi mwingine kama
vile ushahidi wa kihistoria, kiakiolojia na kiethinolojia.
Ushahidi wa kihistoria huchunguza masimulizi
na vitabu mbalimbali vya kale ambavyo huelezea asili na chimbuko la wakazi wa
upwa wa Afrika Mashariki. Vilevile ugunduzi wa kiakiolojia huonesha kuwa kulikuwa na wakazi
wa asili wa upwa wa Afrika Mashariki ambao walikuwa na utamaduni wao na
maendeleo yao hata kabla ya kuja kwa wageni. Katika ushahidi wa kiethinolojia,
huchunguzwa tarihi mbalimbali zinazojaribu kutoa historia ya watu pwani ya
Afrika Mashariki na lugha yao.
Kwa ujumla vyanzo hivi vyote huonesha kuwa
pwani ya Afrika mashariki ilikuwa na wakazi wake wa asili ambao walikuwa na lugha
yao, utamaduni wao na pia maendeleo yao, vyanzo hivi pia huhitimisha kwa kusema
kuwa lugha ya wakazi hawa ilikuwa ni Kiswahili.
Kwa hiyo, kwa hoja hizi tunaweza kuhitimisha
kwa kusema kuwa, madai ya kusema kwamba msamiati mwingi wa kiarabu katika lugha ya Kiswahili hayana mashiko; Kwani
hakuna ushahidi wa kutosha kusimamia hoja hiyo. Kama ilvyojadiliwa hapo
juu, vigezo vya kiisimu, kihistoria, kiakiolojia na kiethnolojia ndivyo vitoavyo
ushahidi wa kina na kutoa hoja zenye mashiko kuthibitisha kuwa Kiswahili sio kiarabu na badala yake Kiswahili ni kibantu.
Insha hii imeandaliwa na wanafunzi wa Kiswahili Chuo Kikuu Cha Dar es salaam kama kazi ya kuwasilisha darasani,
23 comments:
kazi nzuri sana. mapendekezo yangu ni kuwa kazi hii ingepakiwa tena baada ya kusahihishwa na mwalimu wa somo ili kama ku mapungufu tuweze kutambua ili na sisi tusiyarejelee makosa hayo
Usiwe na wasiwasi, kazi hii imesahihishwa, na mapendekezo ya mwalimu yammejumuishwa hapa, unaweza ukarejelea tu.
Safi sana kwa kazi yenu nzuri.
sadakta,maendelezo mazuri,ombi langu ni insha hii ihifadhiwe kwa manufaa ya kizazi kilichoko na kijacho.
kazi nzuri sana.DANIEL NALINGIWA from JOKUCO
Asante! Karibu katika Blogu hii!
Azima unayo,uwezo unao, ujuzi unao himiza zaidi na ustadhi utauwahi. Hongera!
Asante sana! Karibu sana katika neno thabiti.
uhusiano wa fonolojia na mofolojia
Kazi mufti na yenye manufaa kwa yeyote afanyaye kozi kuhusu chimbuko la kiswahili
MWANAFUNZI KUTOKA CHUO KIKUU CHA NAIROBI
Karibu ndugu Alio!
Hongera kwa kazi nzuri ya kusaidia wakereketwa wa lugha tukufu ya kiswahili
ABEL M MUTHEE CHUO KIKUU CHA KENYATTA
Asante Abel! Karibu tukienzi kiswahili.
kazi ni mzuri cha msingi fanyeni utafiti zaidi juu ya uthibitisho kuwa kiswahili ni kibantu kwa kutumia data za kutosha
nimependa kazi yenu, inaonesha wanazuoni mnajituma.endelea kufanya utafiti juu ya hilo. JULIA N. CHARLES, CHUO KIKUU CHA DODOMA
Asante, Karibu sana Bwana Charles
Asante sana, Tutajitahidi kaka.
Kazi nzuri naomba utuwekee Dhana ya uunganishaji katika sentensi
kazi nzuri sana. hongera kwa ukurasa huu wenye maarifa tele. mola akuzidishie hekima na tajriba zaidi. Koki- chuo kikuu cha Kenyatta.
Asante Koki!
Asanteni kwa kazi nzuri. Ningependa kufafanuliwa uhusiano wa isimu na taaluma zingine kama historia, tiba, falsafa, jamii, jiografia, saikolojia, tamaduni na dini.
SWADAKTA ASHANTENI SANA KAZII HII IHIFADHIWE KWA AJILI YA KIZAZI KIJACHO
KAZI KUNTU KABISA,HII ITASAIDIA KIZAZI KIJACHO KATIKA KUELEWA KUWA KISWAHILI NI LUGHA YA KIBANTU NA WAENDELEE KUKIGIZA NA KUKIIMARISHA.
NAMASAKA KENNEDY NAMACHI MWALIMU WA KISWAHILI KUTOKA CHUO KIKUU CHA KIMATAIFA CHA KENYATTA,KENYA.
Post a Comment