Sunday, August 25, 2013

AINA ZA USHAIRI (BAHARI)




Bahari; hii ni aina mahususi ya  ushairi yenye sifa fulani kiumbo na pengine hata kimaudhui na kimatumizi na zinazoipambanua na aina nyingine ya ushairi.

S.A Kibao (2003)  anasema, ushairi wa Kiswahili umegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni: shairi, utenzi na ngonjeara. Anaendelea kusema, aina zote hizi kanuni zake ni za pamoja isipokuwa utenzi ambao una mpangilio wa namna ya pekee.

S. Robert na Amri Abeid (1954)  wanasema zipo bahari tatu tu za ushairi nazo ni:wimbo, shairi na utenzi.

A.S. Nabhany na wenzake wameainisha bahari 13 za ushairi na kusema kuwa utungo wowote lazima uingie katika bahari mojawapo. Bahari hizo ni hizi zifuatazo:
1.      Ushairi; Ni utenzi wenye mishororo minne na vipande  viwili kila msitari. Kila mstari una mizani 16 na kila kipande kina mizani 8. Maudhui yake yanatokana na jambo lolote lile analoliona mtunzi.

2.      Wimbo; Ni utungo wenye mishororo mitatu kila ubeti na kila mshororo una vipande viwili. Nyimbo nyingi huongelea mapenzi.

3.      Tenzi; Ni utungo wenye vipande vine katika kila ubeti na vina hubadilika kila ubeti isipokuwa kipande cha mwisho. Tenzi nyingi zina mizani nane kila mshororo na nyingine zina mizani 11 na zingine 10.

4.      Inkshafi/Duramandhuma; Imepata jina lake kutokana na utenzi wa Aliinkshafi. Tenzi hizi zina maadili ya kidini japokuwa maudhui yake yanaweza kutumika katika maadili ya kidunia. Kila ubeti una mishororo minne na kila mshororo una mizani 11.

5.      Ukawafi; Hili ni shairi lenye mishororo mitatu au zaidi katika kila ubeti na vipande vitatu katika kila mshororo. Mizani zinaweza zikatofautiana au zikawa sawa.

6.      Wajiwaji/Takhimisa; Una mishororo mitano kila ubeti na mizanai 15 kila mshororo na vipande vitatu katika kila mshororo vina muundo wa mizani 6, 4, 5. Maudhui yake ni ya kidini au kiamisha kwa ujumla, mfano Takhimisa ya Liongo  na tenzi ya Inkshafi.

7.      Hamziya; lipata jina lake kutokana na kaswida ya Hamziya ambao ni utenzi wa kiarabu. Mishororo ya Hamziya ina vipande 3 vya mizani 5, 4, 6

8.      Tiyani-Fatiha;   Ni ushairi wa kidini wa kuomba toba, una mishororo 9 kila ubeti ambayo huweza kutofautiana kwa urefu/mizani.

9.      Utumbuizo; Haina idadi kamili ya mishororo na mizani, urefu wa mstari au mshororo hutegemea pumzi aliyonayo mwimbaji na lengo lake; mfano ni nyimbo za Liyongo kuna tumbuizo.

10.  Wawe; Ni ushairi au wimbo wa kilimo, huimbwa wakati wa kulima au kupanda.

11.  Kimai; Inahusu shughuli za majini, ni bahari ya wavuvi na mabaharia. Idadi ya mishororo na vina si lazima.

12.  Zivindo; Ni ushairi unaofafanua maana za maneno; na kazi yake ni kujifunza lugha na mkuhifadhi lugha.
Mfano: Kata ni kata ya nyoka
             Au kata ya nyweleni
             Kata ya tweka, bandikwayo kichwani

13.  Sama; Neno ‘sama’ ni mahadhi au sauti, hivyo bahari hii hukusanya washairi wote wenye kufuata mahadhi ya kigeni.

15 comments:

Anonymous said...

naomba kujuzwa kuwa bahari za ushairi za A.S Nabhany zina ubora gani na dosari gani?

Anonymous said...

suala la bahari za ushairi ni suala telezi mno kwani kumekua na uainishaji wa aina tofauti tofauti .Mfano Samweli & Akech wao wamegawa katika mitazamo miwili yaani mapokeo na wana usasa ambapo kwa wana mapokeo wameainisha bahari katika makundi 16 na kigezo cha wanausasa 11, pia weendelea kuainisha kwa kigezo cha uradidi .HIVYO SUALA LA BAHARI LINAUTELEZII

Anonymous said...

Hakika,bahari za ushairi ni hazina ya wanafasihi.

iscaca said...

Ushairi hoyeee!

Unknown said...

Kazi nzuri sana, binafsi nimejifunza mengi kutoka kwenye hiz bahari za ushairi.

Linus said...

Kazi nzuri

Unknown said...

Bahari alizoainisha Wamitila zinaonekana kuwa bora zaidi ya za Nabhany hivyo ni vema kumsoma pia Wamitila maana yeye amezingatia vigezo

Komba said...

Naomba kujua mapungufu au madhaifu ya kila bahari.

Unknown said...

Nina swali jaman kuna udhaifu wa bahar za nabhany je tunawezaje kuondoa udhaifu huo

Unknown said...

Nina swali jaman kuna udhaifu wa bahar za nabhany je tunawezaje kuondoa udhaifu huo

Unknown said...

Nina swali jaman kuna udhaifu wa bahar za nabhany je tunawezaje kuondoa udhaifu huo

Unknown said...

Mapungufu yao katika uainishaji ni yapi 😳

Anonymous said...

1. Haiweki vigezo vinavyotumika kupata bahari.
2. Baadhi ya bahari zimeegemea idadi ya mishororo na mizani.
3. Kuna hatari ya kudhani kuwa bahari hizo ndimo ukomo wa ubunifu wa washairi.
4. Bado zipo aina nyingine za ushiri tofauti na hizo.

Anonymous said...

AM
1. Haiweki vigezo vinavyotumika kupata bahari.
2. Baadhi ya bahari zimeegemea idadi ya mishororo na mizani.
3. Kuna hatari ya kudhani kuwa bahari hizo ndimo ukomo wa ubunifu wa washairi.
4. Bado zipo aina nyingine za ushiri tofauti na hizo.

Anonymous said...

Hodi