Dunia inabadilika kila kukicha, sayansi na teknolojia huibuliwa kila kukicha, mambo haya yote huwaweka watu pamoja kutoka kila kona ya dunia, lakini pia watu hawa hawzungumzi lugha moja, wanahitaji kuwasiliana na ili mawasiliano yaweze kufanyika lazima kuwepo na lugha inayowaunganisha. Suala hili ni gumu kwa kuna lugha nyingi sana duniani na kila nchi inasera yake juu ya lugha lakini pia lazma watu wawasiliane na hapa ndipo tunaona umuhimu wa kuwepo mkalimani.
Lugha ya kiswahili inakuwa kwa kasi sana, vyuo mbalimbali duniani hufundisha lugha hii adhimu kwa nini wewe usione fursa hii na uchukue hatua ya kujifunza ukalimmani ili ujiajiri katika soko kubwa kama hikli.
Kabla hujachukua uamuzi hebu jielimishe kidogo juu ya taaluma hii ya ukalimani.
Tafsri na ukalimani ni
taaluma za lugha ambazo mara nyingi watu huchanganya wakidhani kuwa dhana hizi
mbili hufanana lakini kimsingi kuna utofauti mkubwa kati ya tafsiri na
ukalimani, elimu na ujuzi katka taaluma hizi hutofautiana. Kuna tofauti za
msingi zinazotofautisha taaluma hizi, tutazichambua kwa kina katika sura
zinazofuata. Kwa sasa tuangalie kwa kina dhana nzima ya ukalimani ambapo
tutaangalia maana, aina za ukalimani, sifa za mkalimani (mambo ya kuzingatia
katika ukalimani) na mwisho hitimisho.
Maana
ya ukalimani.
Ukalimani wa lugha hulenga
kurahisisha mawasiliano ya lugha ya mdomo au lugha ya alama kati ya watumiaji
wa lugha mbili tofauti.
Kwa mujibu wa Encarta (2009)
ukalimani ni tafsiri ya mdomo ya kile kinachosemwa katika lugha moja kwenda
lugha nyingine ili kusudi wazungumzaji wa lugha tofauti waweze kuwasiliana.
Wikipedia wamefasili
ukalimani kuwa ni uhawilishaji wa ujumbe katika lugha ya mazungumzo au lugha ya
alama kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine.
Fasili zote hizi zinajaribu
kutupa mwangaza hasa juu ya maana ya ukalimani, fasili ya kwanza inakasoro.
Kutumia istilahi yenye maana tofauti na kile kinachojaribu kufasiliwa huleta
mkanganyiko, istilahi tafsiri inamaana tofauti na ukalimani kwa hiyo sio sahihi
kuitumia katika kufasili dhana ya ukalimani. Fasili ya pilli imejaribu kugusa
mambo muhimu katika dhana ya ukalimani, kwamba ni uhawilishaji wa ujumbe katika
lugha ya mazungumzo, kimsingi ukalimani hufanyika katika lugha ya mazungumzo.
Kwa hiyo kutokana na fasili
hizi tunaweza kupata fasili ya jumla kwamba, ukalimani ni zoezi la uhawilishaji
wa mawazo,ujumbe, maana katika lugha ya mazungumzo au lugha ya alama kutoka
lugha chanzi kwenda lugha lengwa.
Hivyo basi mkalimani ni mtu
ambaye huhawilisha mawazo, maana au maelezo kutoka lugha chanzi na kuyaweka
mawazo au maelezo au maana yenye maana inayolingana katika lugha lengwa, katika
wakati halisi. Kazi ya mkalimani ni kufikisha kila kipengele cha kisemantiki
(rejesta,toni) na kila lengo na hisia za ujumbe ambao mzungumzaji wa lugha
chanzi amekusudia kufikisha katika wapokeaji wa lugha lengwa.
Aina
za ukalimani.
Kuna aina tofautitofauti za
ukalimani kulingana na vigezo tofautitofati vinavyotumika katika kuainisha aina
za ukalimani. Kwa kutumia kigezo cha jinsi ukalimani unavyofanywa, tunapata
aina kuu mbili:
Ukalimani
mfululizo; katika ukalimani wa aina hii mzungumzaji wa lugha chanzi
na mzungumzaji wa lugha lengwa huanza pamoja na kumaliza pamoja. Maranyingi vifaa
maalum hutumika, mkalimani hukaa katika chumba chenye kidhibiti sauti akizungumza
kupitia kipaza sauti wakati huo akimsikia na kumwona barabara mzungumzaji wa
lugha chanzi kupitia visikizio. Wasikilizaji wa lugha lengwa hupata ujumbe
kupitia visikizio. Vilevile ukalimani wa aina hii hutumiwa sana na wakalimani
wa lugha ya alama.
Ukalimani
fuatizi; katika aina hii ya ukalimani, mkalimani huzungumza baada
ya mzungumzaji wa lugha chanzi kumaliza kuzungumza. Mkalimani anakua amesimama
au amekaa sambamba na mzungumzaji wa lugha chanzi akiwa anasikiliza napengine kuandika
maneno anayozungumza mzunguzaji wa lugha chanzi ili kumsaidia kukumbua pindi
atakapoanza kukalimani. Wakati mzingumzaji wa lugha chanzi anapumzika au
anamaliza kuongea ndiposa mkalimani anahawilisha kipande cha ujumbe au ujumbe
mzima katika lugha lengwa.
Aina
zingine za ukalimani.
Ukalimani
wa kwenye mikutano; huu ni ukalimani unaofanyika wakati wa mikutano,
huweza ukawa fuatizi au mfululizo, lakini kwa sababu ya mikutano inayokutanisha
lugha nyingi, ukalimani fuatizi hautumiki. Katika ukalimani wa kwenye mikutano
maranyingi mkalimani hufanya ukalimani kutoka lugha za kigeni kwenda lugha yake
ya asili.
Ukalimani
wa mahakamani; ukalimani wa aina hii hufanyika mahakamani,
katika mabaraza ya kutolea hukumu na mahali popote pale ambapo masuala ya
kisheria hufanyika, mfano katika kituo cha polisi hususani wakati wa kuchukua
maelezo au katika ukumbi wa mikutano kwa ajili ya kuapishwa.
Ukalimani
kiungo; ukalimani wa aina hii ni pale ambapo mkalimani humsaidia
mtu au kikundi cha watu katika kutalii, matembezi au katika mkutano.
Ukalimani wa lugha ya alama;
hii ni aina ya ukalimani ambao hufanyika kati ya lugha ya alama na lugha ya
mazungumzo. Mzungumzaji anaweza kuongea mkalimani akahawilisha mawazo kwa njia
ya alama, vilevile wakati mtu asiyesikia akifanya mawasiliano kwa lugha ya
alama, mkalimani atahawilisha maana katika lugha ya mazungumzo. Vilevile
ukalimani huweza kufanyika kati ya lugha ya alama na alama hii ni kwa sababu
lugha ya alama hutofautiana kati ya nchi na nchi.
Ukalimani
wa vyombo vya habari; kulingana na asili yake ukalimani wa vyombo
vya habari hufanyika kwa ukalimani mfululizo. Hufanyika zaidi katika matangazo
ya moja kwa moja ya televisheni au redio. Katika ukalimani wa vyombo vya habari
vifaa kama chumba cha kudhibiti sauti,
kiwamba nakadhalika huhitajika sana.
Ukalimani
wa simu; ukalimani wa aina hii humsaidia mkalimani kufanya
ukalimani kupitia simu. Maranyingi hufanyika katika mazingira ambayo watu
wanaohitaji kuwasiliana tayari wanakuwa wamekwishazungumza kupitia simu.
Ukalimani
wa video; ukalimania wa aina hii hufanyika katika mazingira ambapo
mmoja kati ya wanaowasiliana ni kiziwi au hasikii vizuri au hawezi kuongea
(bubu). Katika mazingira kama haya ukalimani wa lugha ya alama hufanyika zaidi.
Ukalimani
kulingana na muktadha; katika kundi hili kuna aina nyingi
kulingana na jinsi itakavyojidhihirisha aktika miktadha tofautitofauti. Mfano,
ukalimani wa kanisani, ukalimani wa msikitini, ukalimani wa mahakamani, jeshini
nakadhalilka.
Ni matumaini ya ngu utakuwa umenufaika, unaweza pia kutoa maoni yako!.
24 comments:
tofauti iko wapi kati ya ukalimani na utafsiri?
Asante sana kwa swali lako zuri. Karibu katika blogu hii!
Kwa kweli watu wengi wanadhani kuwa tafsiri ni sawa na ukalimani, hii sio sahihi. Ukalimani na tafsiri ni taaluma za lugha ambazo zina uhusiano wa karibu lakini pia kwa nadra sana watu wachache huweza kuzimudu vizuri taaluma zote hizi kwa kiwango kilekile. Tofauti katika ustadi, mafunzo, kipaji na hata uelewa mzuri wa lugha ni mambo muhimu sana katika taaluma za tafsiri na ukalimani ambayo watu wachache wanaweza kufanikiwa kuwa nayo kwa kiwango cha taaluma. Kwa hiyo kwa misingi hiyo, kunatofauti kati ya taaluma ya tafsri na ukalimani, tofauti hizo ni kama hizi rafiki:
i) Tafsiri hufanyika kwa njia ya maandishi, mfasiri huhawilisha mawazo au ujumbe kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa kwa kutumia kalamu na karatasi au kwa kuchapa kwa kutumia kompyuta kinyume na ukalimani, mkalimani huhawilisha kile anachosema mzungumzaji wa lugha chanzi kwenda lugha lengwa kwa njia ya mdomo.
ii) Tafsiri hufanyika kwa kurejelea marejeo mbalimbali kama vile kamusi za aina zote zinazohusika na matini husika pamoja na marejeo mengine muhimu ilihali ukalimani hufanyika bila kurejelea mahali popote.
iii) Katika tafsiri, mfasiri ni lazima asome kwanza matini chanzi kabla haajanza kufasiri kwa lengo la kuihakiki ili aweze kutoa zao bora zaidi la tafsiri lakini katika ukalimani si lazima mkalimani apitie matini chanzi kabla ya kuanza kukalimani kwani ukalimani hufanyika hapo kwa papo.
iv) Katika tafsiri mfasiri ana muda wa kuihakiki matini anayoifasiri ili aweze kurekebisha makosa yanayojitokeza kabla ya kuikabidhi kwa mteja lakini katika ukalimani, mkalimani hana muda wa kufanya marekebisho.
v) Mafunzo yanayotolewa kwa mfasiri ni tofauti na yanayotolewa kwa mkalimani. Mfasiri hufundishwa stadi za uandishi na usomaji mzuri ilihali mkalimani hufundishwa stadi za kuzungumza vizuri mbele ya umma.
vi) Katika ukalimani, mkalimani ni lazima awe na uelewa wa kiwango sawa katika lugha zote mbili yaani lugha chanzi na lugha lengwa, hii ni kwa sababu mkalimani anaweza kulazimika kukalimani kwenda pande zote mbili kwa wakati huohuo lakini kwa mfasiri sio lazima sana aielewe lugha chanzi kwa kiwango sawa na cha luhga lengwa.
vii) Ukalimani hufanyika katika muda halisi yaani zao la ukalimani ni la hapo kwa papo wakati tafsiri haifanyiki katika muda halisi mfasiri anaweza kufanya kazi yake muda wowote kulingana na uhitaji wa mteja wake.
Natumaini utakuwa umeiona tofauti. Karibu sana tushirikiane katika taaluma hii ya Kiswahili.
samahani me hapa nimeelewa lakini swali langu linakuja kuwa taaluma ya kutafsiri inamwingiliano na kazi nyingine za kiswahili, je zinaingiliana vipi? na hizo kazi ni zipi?
Asante kwa swali lako zuri ndungu! Ila sina uhakika kwamba unaposema kazi nyingine za kiswahili unamaanisha nini. Lakini kulingana na swali lako naweza nikakujibu hivi; Taaluma ya Kiswahili haipo peke yake ina mwingiliano mkubwa na taaluma nyingine, kama swali lako kweli lipo kwenye kazi nyingine za kiswahili naomba ufafanue kidogo ili uliweke wazi swali lako.
Lakini kwa kuanza nitalijubu swali lako kama ifuatavyo, kama utaridhika naomba unijulishe. Kama nilivyosema kuna mwingiliano mkubwa kati ya tafsiri na taaluma nyingine na taaluna hizo ni hizi zifuatazo:
Taaluma za kiisimu
Semantiki; hii inahusiana na maana. Katika tafsiri tunazingatia maana ya lugha chanzi ili isitofautiane na maana ya lugha lengwa. Muktadha pia sharti uzingatiwe katika kupata maana.
Isimujamii; huangalia jamii inavyoathiri lugha na lugha inavyoathiri jamii. Katika tafsiri tamaduni, mila na desturi za jamii husika huzingatiwa. Mfano unapokutana na maneno ya kitamaduni katika tafsiri kv salamu, vyakula n.k hapa inabidi utamaduni wa lugha husika uzingatiwe.
Isimu linganishi; katika tafsiri tunalinganisha lugha moja na nyingine ili kuelewa miundo na maumbo kati ya lugha chanzi na lugha lengwa, kwa hiyo isimu linganishi huchukua nafasi yake hapa.
Elimu mitindo; katika tafsiri kuna uainishaji wa mitindo ya lugha na muktadha wa matumizi yake kitu ambacho kipo katika taaluma ya elimu mitindo.
Taaluma zisizo za kiisimu
Uhakiki wa matini; katika tafsri kabla mfasiri hajaanza kutafsiri matini ni lazima ahakiki matini chanzi kwa lengo la kubaini upungufu unaojitokeza na ili kujua namna ya kuweza kukabiliana nao.
Mantiki; hii ni taaluma inayohusu ukweli na usahihi katika kauli au matini Fulani. Taaluma hii humsaidia mfasiri kubaini mfasiri kubaini usahihi na mantiki iliyopo katika lugha chanzi
Falsafa; hii ni taaluma inayosisitiza kutafuta maana za maneno kutokana na matumizi halisi katika matini. Hii humsaidia mfasiri kujua falsafa ya matini husika ili kujua maana yake.
Hata kama nitakuwa sijalijibu swali lako lakini nadhani nitwakuwa nimekupa mwanga fulani na nafikiri unaweza kuliweka sawa swali lako vizuri.
uja tupa umuhimu wa ukalimani na tafsiri kwenye ulimwengu wa sasa
nashukulu kwa kunijibia swali langu lkn swali lenyewe liko hivi, taaluma ya kutafsiri inafanya kazi kwa ujirani au mwingiliano na taaluma nyingine ambazo ni za lugha, taja angalau taaluma tano zinazofanya kazi kwa kushirikiana na taaluma hiyo alafu elezea kwa mifano ni kwa vipi zinaingiliana na taaruma ya kazi ya tafsiri. namba msaada
Sawa, nafikiri hilo swali ndilo nimelijibu, jibu lake ndo hilo nililokwishalijibu. Taaluma nyingine za lugha ndo kama hizo, uhakiki, isimu linganishi, isimujamii, elimu mitindo na nynginezo kama hizo. Jibu lako likijikita hapo utakuwa umejibu swali lako vizuri.
Asante kwa kazi nzuri, naomba unisaidie vigezo vya uainishaji wa ukalimani
Vizuri sana mtaalamu naomba unisaidie dhana kama nne tofauti za ukalimani
Ningependa kujuzwa Umuhimu wa tafsiri na ukalimani katika mawasiliano
Ukipewa nafasi ya kukutana na wajumbe wa katiba 2014 wa bunge la jamuhuri ya Tanzania utawashawishi vipi kuhusu ukalimani
Naomba kujua aina za ukalimani kwa kutuMia kigezo cha lugha na muktadha
Kazi nzuri Sana kaka,lakini wanataaluma wengi Sana dhana ya ukalimani inawakanganya hasa kwakua wanaona ukalimani na tafsiri ni dhana moja. Je wewe Kama mwana taaluma una mtazamo gani kuhusu ilo?
Asante kwa Nazi nzuri
Asante kwa Nazi nzuri
Swali langu ni naomba unitajie mifanano iliyopo kati ya ukaliman n tafsiri
Mkalimani ni kipaza sauti cha mzungumzaji wa lugha chanzi ingawa sio kwa kila jambo. Jadili kwa hoja ukweli na usikweli wa madai haya. Naomba msaada wa majibu
Swali langu ni eleza wahusika katika ukalimani
Mambo ya msingi unapofasili lugha
tofauti kati ya ukalimani wa kutumiya lugha ya maneno n ukalimani wa kutumiya lugha ya alama
Aina za wakalimani na wafasiri
kazi nzuri
Need umuhimu wa ukalimani
Samahani
naomba unisaidie. to faut I ya tafsiri na ukalimani kea kigezo cha mfumo wa lugha na kigezo cha. Stadium za lugha
Post a Comment