Sunday, December 8, 2013

Tofauti nyeti za kimaana za maneno; Chapa, charaza, tandika, zaba, nasa, kafua, nyuka,kung’uta, twanga, timba. (katika muktadha wa kitendo cha kumpiga mtu kwa kumwadhinu) kwa kuzingatia madai ya wataalam kwamba hakuna sinonimia kuntu katika lugha yoyote ile



Katika kuangalia mjadala huu tutaanza kuelezea maana ya sinonimia kwa mujibu wa wataalamu kisha tutaonesha maana za msingi za maneno katika data kwa mujibu wa kamusi, tutabainisha na kufafanua kanuni za msingi za kubainisha sinonimia kuntu, tutazijaribu sinonimia hizo kwa kuzitungia sentensi na kisha kubadilisha nafasi ya kila sinonimia katika kila sentensi na mwisho kabisa tutatoa hitimisho.

Kwa mujibu wa Habwe na Karanja (2004) sinonimia ni visawe vya dhana moja. Kwa ufafanuzi juu ya maelezo haya tunaweza kusema kuwa sinonimia ni maneno tofauti yanayobeba dhana inayofanana. Kimsingi fasili hii inajitosheleza kwani tunaposema sinonimia tuna maana kwamba maneno yenye maana sawa au inayokaribiana. Maneno kuwa na maana sawa au inayokaribiana maana yake ni kwamba maneno haya hurejelea dhana moja.

Kabla hatujaanza kupima sinonimia hizi katika sentensi ni vema tukaangalia maana za msingi za maneno haya. Kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili sanifu maneno haya yana maana zifuatazo:

·           
  • Chapa – piga  kwa kutia adabu au kuumiza
  • Charaza – piga kwa mfululizo, kwa fimbo.
  • Tandika – piga, chapa (piga kwa kuumiza)
  • Zaba – piga kwa kofi
  • Nasa – piga, zaba (piga kwa kofi)
  • Kung’uta – kupigapiga kwa fimbo au kwa kubamiza kwenye kitu kingine.
  • Kafua – ondoa makapi ya nafaka kwa kupigapiga, kupiga kwa kupura
  • Nyuka – piga kwa nguvu, piga sana.
  • Twanga – piga vibaya kwa ngumi
  • Timba – kanyaga kitu k.v tope, kupiga kwa kukanyagakanyaga.

Kwa kutumia mbinu za msingi sasa tunaweza kutofautisha sinonimia hizi kwa mujibu wa data tuliyopewa. Kanuni za kutofautisha sinonimia kuntu zipo mbili ambazo ni:
Kuangalia miktadha mbalimbali ya matumizi ya sinonimia husika katika mazungumzo au katika maandishi. Kwa mujibu wa swali letu tutaangalia sinonimia hizi katika muktadha wa kitendo cha kumpiga mtu kwa kumwadhibu.

Kutunga sentensi kadhaa tofauti kwa kutumia kila sinonimia moja kwa sentensi moja kisha kubadilisha nafasi ya kila sinonimia katika sentensi na kuweka sinonimia nyingine. Kwa hiyo kanuni hizi ndizo tumezitumia katika kubainisha endapo sinonimia katika data ni kuntu au la.
Baada ya kuangalia kanuni hizi sasa tuanze kuzijaribu sinonimia hizi kwa kuzitungia sentensi. Hebu tuangalie sentensi zifuatazo:
  1.  Ukijikojolea kitandani nitakuchapa viboko
  2. Mwalimu wa zamu aliwacharaza fimbo wanafunzi waliochelewa kufika shuleni.
  3. Juma alimzaba kibao Asha
  4.   Mkuu wa wilaya aliwatandika walimu waliokwenda kinyume na maadili ya kazi
  5.  Alipokuwa anajaribu kujitetea alijikuta amenaswa kibao shavuni 
  6. Wanafunzi walimkafua mwizi alipokuwa anajaribu kuiba nguo. 
  7. Wee, ukinigusa nitakunyuka viboko! 
  8. Alipokatisha uchochoroni alitwangwa kwa nondo. 
  9. Baba alipokuwa amelewa alimtimba mama kwa kuchelewa kumfungulia mlango. 
  10. Mama alimkung’uta dada kwa mwiko.
Baada ya kuzitungia sentensi sinonimia hizi hebu sasa tuzijaribu kwa kuingiza kila sinonimia katika kila sentensi ili kuona kama maana inayorejelewa katika sentensi moja na sinonimia tufauti tofauti ni ileile au la!

Ili iweze kuwa rahisi kujaribisha sinonimia hizi katika kila sentensi tutatumia jedwali ambapo kila jwedwali litakuwa na sentensi moja ya awali na kisha sinonimia zote zitaorodheshwa sambamba na sinonimia ya msingi iliyotumika katika sentensi ya awali.
1.      Ukijikojolea kitandani
nitakuchapa
viboko

nitakucharaza




nitakuzaba *


nitakutandika*


nitakunasa *


nitakukafua *


nitakunyuka *


nitakutwanga*


nitakutimba *


nitakung’uta *




 



Sinonimia zilizotiliwa alama ya nyota (*) zinamaana kwamba hazileti maana angavu katika muktadha wa sentensi hii, neno zaba na nasa hueleweka vizuri kama yakiwa yameambatana na neno kibao/vibao hali kadhalika maneno twanga na kutimba hayaleti maana katika muktadha wa kumpa mtoto adhabu, dhana ya kupiga katika maneno haya ni kupiga kwa lengo la kujeruhi kabisa au kuumiza, hivyo hayawezi kuchukua nafasi ya sinonimia chapa.
2.       Mwalimu wa zamu
aliwacharaza
fimbo wanafunzi waliochelewa shuleni

aliwachapa

aliwazaba*
aliwatandika

aliwanasa *
aliwakafua *

aliwanyuka
aliwatwanga *
aliwatimba *
aliwakung’uta
Katika muktadha wa sentensi hii maneno yenye alama ya nyota (*) hayawezi kubadilishana nafasi na sinonimia charaza kwa sababu hayawezi kuleta maana angavu hii ni kutokana na neno fimbo, neno hili haliwezi kutangamana na sinonimia zilizowekewa nyota. Kwa mfano maneno zaba na nasa maana yake inakuwa hafifu kama yasipoandamana na na neno kibao/vibao na pia maneno kafua, twanga na timba dhana yake ni kupiga kwa nguvu  ama kwa kutumia kitu fulani ama kwa mateke na ngumi, kwa muktadha wa sentensi hii maneno haya hayawezi kubadilishana nafasi na sinonimia charaza.

3.      Juma
alimnasa
Asha kibao

alimchapa

alimcharaza*
alimzaba
alimkafua *
alimnyuka *
alimtwanga *
alimtimba *
alimkung’uta *
alimtandika
Maneno yote yaliyotiliwa nyota katika sentensi hii hayaleti maana yanapokuwa yamebadilishana nafasi na sinonimia nasa neno kibao limeyaengua maneno haya yote kwa kuwa neno kibao hutangamana na sinonimia zaba, nasa na wakati mwingine watu huweza kutumia chapa au tandika, lakini matumizi ya sinonimia hizi katika muktadha wa sentensi yetu pia huweza kubadili maana. Mtu anaposema alimtandika/chapa kibao huonesha uzito wa kupigwa kibao, kwamba kibao alichopigwa kilikuwa ni cha nguvu na kilikuwa na lengo la kumuumiza kwelikweli.

4.      Mkuu wa wilaya
aliwatandika
walimu waliokwenda kinyume na maadili ya kazi.

aliwanasa*
aliwachapa
aliwacharaza*
aliwazaba *
aliwakafua *
Aliwanyuka *
aliwatwanga*
aliwakung’uta*
aliwatimba *
Katika sentensi hii sinonimia nasa na zaba hazileti maana angavu bila kuambatana na neno kibao au kofi pia vilevile sinonimia kafua, twanga na timba maranyingi humaanisha kupiga kwa nguvu kwa lengo la kuumiza au kujeruhi na hutolewa kwa mtu mmojammoja hivyo haziwezi kutumika kwa kujumuisha. Na sinonimia chapa huweza kubadilishana nafasi na sinonimia tandika bila kuathiri maana ya sentensi kwani zote zinabeba maana moja ya kumpiga mtu kwa lengo la kumtia adabu.

5.      Alipokuwa anajaribu kujitetea aliajikita
amenaswa
kibao shavuni

amechapwa
amezabwa
ametandikwa
amekafuliwa*
amenyukwa *
ametwangwa*
ametimbwa *
amekung’utwa*
amecharazwa *
Maneno yote yaliyotiliwa nyota hayawezi kubadilishana nafasi na sinonimia nasa na kuleta maana ileile kwani neno kibao halitangamani na sinonimia zilizotiliwa nyota na badala yake hutangama na sinonimia  nasa, zaba na wakati mwingine tandika au chapa. Lakini sinonimia hizi zinapotumika katika muktadha wa kutangamana na neno kibao maana yake pia hubadilika, sinonimia hizi huonesha uzito wa kibao alichopigwa, kwamba kilikuwa ni cha nguvu sana na huwenda kilimjeruhi kabisa.

6.      Wanafunzi
walimkafua
mwizi alaipokuwa anajaribu kuiba nguo

walimchapa *

walimzaba *
walimtandika*
wamnasa *
walimcharaza*
walimnyuka
walimtwanga
walimtimba
walimkung’uta
Katika sentensi hii kulingana na uzito wa kipigo sinonimia nasa na zaba, tandika, chapa na charaza  zinahafifisha maana kama zikitumiwa katika muktadha wa sentensi hii. Kipigo cha mwizi huwa kikubwa na huwa kinalenga kujeruhi na kuua kabisa. Kwa mantiki hii huwezi kumpiga mwizi kwa kumchapa, kumzaba au kutandika na badala yake mwizi hukung’utwa, hutwangwa au hutimbwa.

7.      Wee, ukinigusa
nitakunyuka
viboko

nitakuchapa

nitakucharaza
nitakuzaba *
nitakutandika
nitakutwanga *
nitakutimba *
nitakukung’uta
nitakukafua *
Maneno yaliyowekewa nyota hayawezi kubadilishana na sinonimia nyuka na kuleta maana kwa ni maneno haya hayatangamani na neno viboko katika muktadha wa sentensi kwani neno viboko huendana na sinonimia chapa, nyuka, tandika na kung’uta.

8.      Alipokatisha uchochoroni
alitwangwa
kwa nondo

alizabwa *

alitandikwa
alinaswa *
alikafuliwa
alinyukwa *
alitimbwa *
alikung’utwa
alicharazwa *
Katika sentensi hii maneno yaliyowekewa nyota  hayawezi kubadilishana nafasi na sinoimia twanga hii ni kwa sababu ya kuwepo neno nondo ambalo linaibua uzito wa kipigo lakini pia huonesha zana ya kupigia kwa mantiki hii sinonimia kama vile zaba, nasa, charaza, nyuka na timba zinakuwa zinajiengua kwa sababu haziwezi kutangamana na zana yenyewe ya kupigia yaani nondo au maana zake ni hafifu kulingana namuktadha wenyewe wa kupiga.

9.      Baba alipokuwa amelewa
alimtimba
mama kwa kuwa alichelewa kumfungulia mlango

alimchapa*

alimcharaza*
alimnasa *
alimzaba *
alimtandika
alimkafua
alimnyuka
alimtwanga
alimkung’uta
 Maneno charaza, chapa, nasa na zaba hayaleti maana angavu yanapobadilishwa na sinonimia timba hii ni kwa sababu katika muktadha wa kupigana kati ya mke na mume na wakati huo mume amekwisha lewa hatutegemei kama ugomvi wa hapo utakuwa ni wa kuchapa au kucharaza bali utakuwa ni wa kunyuka, kukafua na kutwanga. Kwa hiyo hii ndio sababu sinonimia zilizotiliwa nyota haziwezi kubadilishana nafasi na sinonimia timba.

10.     Mama
alimkung’uta
dada kwa mwiko

alimchapa

alimcharaza
alimzaba*
alimtandika
alimnasa *
alimkafua*
alimnyuka*
alimtwanga*
alimtimba *
Katika sentensi hii tunaona kuwa sinonimia zilizotiliwa nyota (*) haziwezi kubadilishana nafasi na sinonimia kung’uta na maana ikabaki ileile, katika muktadha wa mzazi kumwadhibu mwanae, adhabu inayotolewa huwa ni ya kuadibu na huwa haina lengo la kuumiza au kujeruhi. Kwa hiyo katika muktadha huu maneno yaliyotiliwa nyota mengine yana maana ya adhabu kubwa kwa mfano timba, kafua, twanga, nyuka lakini mengine hayatangamani na maneno yaliyotumiwa mfano sinonimia nasa, zaba, timba.

Kwa kuhitimisha; kulingana na sentensi tulizoziona tumeona kwamba sio sinonimia zote zinaweza kuchukua nafasi ya sinonimia nyingine katika sentensi na hii hutokana na sababu zifuatazo:
Mahusiano ya maneno katika sentensi kulingana na maana inayorejelewa; sinonimia nyingine zina maana ya kipigo kizito, kwa mfano katika sentensi na. 6 neno mwizi linahusiana kwa karibu zaidi na sinonimia kafua kuliko linavyohusiana na sinonomia nasa au zaba. Kitendo cha kumpiga mwizi huwa ni kwa lengo la kumuumiza au hata kwa lengo la kumuua kabisa. Kwa hiyo sinonimia nasa na zaba haziwezi kuibua  dhana hii kwa uangavu.

Utangamano wa maneno; katika data hii kuna sinonimia ambazo haziwezi kuleta maana angavu isipokuwa kwa kuandamana na maneno mengine mfano; katika sentensi na. 3 sinonimia nasa au zaba isingeleta maana angavu kama isingeandamana na neno kibao. Kwa sababu hii ndio maana sinonimia nyingine hazikuweza kuchukua nafasi ya sinonimia nasa na kuleta maana.

Tofauti katika maana za msingi za sinonimia pia huweza kuwa sababu ambayo inaonesha kuwa hakuna sinonimia kuntu; kwa mfano katika sentensi zetu tumeona baadhi ya sinonimia zinabadilishana katika mukutadha fulani wa sentensi lakini kwa sababu ya utangamano wa maneno, kwa mfano katika sentensi namba 5 tunaona kuwa sinonimia chapa na tandika zinabadilishana nafasi na sinonimia nasa lakini kimsingi maana ya sentensi inabadilika. Nasa  kibao inaonesha ukawaida wa kipigo lakini tandika kibao inaonehsa ukubwa wa kipigo hicho. Kwa hiyo kwa msingi huu tunaona kuwa maneno yanaweza kubadilishana nafasi lakini maana pia ikabadilika.

Kwa hiyo kutokana na sababu hizi kutoka katika mifano tuliyoitoa tunaweza kusema kuwa hakuna sinonimia kuntu.



 MAREJEO
Habwe, J. na Karanja, P (2004) Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers.
TUKI (2004). Kamusi ya Kiswahili Sanifu, toleo la pili. Dar es Salaam: Oxford University Press.

No comments: