Utangulizi
Lugha ya Kiswahili ina historia ndefu hapa Afrika Mashariki kama chombo cha kuunganisha watu wenye tamaduni tofautitofauti tokea enzi za biashara ya utumwa hadi baada ya uhuru. Wafanya biashara wa enzi za utumwa walitumia lugha ya Kiswahili ili kurahisha mawasiliano na kukidhi haja zao za kibiashara, bila kujua, walijikuata wanakieneza Kiswahili kutoka pwani ya Tanganyika hadi bara ya Kongo. Wakoloni nao walipokuja Afrika Mashariki waliona Kiswahili ndio lugha pekee ya kurahisha utawala wao, lakini baadae walikuja kugundua kuwa Kiswahili ilikuwa ni silaha ya kuangamiza utawala wao na hivyo wakahafifisha matumizi ya Kiswahili.
Wanaharakati wa utaifa, wakati wa kupigania uhuru hususani katika nchi ya Tanganyika waliona Kiswahili ndio njia pekee itakayowasidia kupata uhuru bila hata kumwaga tone la damu. Mwalimu Nyerere alitumia fursa hii kuwaunganisha watanganyika wote wenye tamaduni tofautitofauti na waliokuwa wakizungumza lugha tofautitofauti, lakini kwa kupitia lugha ya Kiswahili walikuwa na kauli moja ya kutaka Tanganyika ya watanganyika huru. Umoja huu umedumu hadi leo Tanzania inajulikana kuwa ni nchi ya watu wakarimu na wenye umoja. Isingewezekeana kufukia hapa kama kila mtu angejitukuza kwa kabila lake ila kwa kutumia Kiswahili watanzania sasa ni wamoja, hakuna msamiati katika mazungumzo ya watanzania unaotukuza ukabila.
WANACHAWAKAMA KATIKA UFUNGUZI WA KONGAMANO |
Katika makala hii tutaangalia nafasi ya Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili vyuo vikuu Afrika Mashariki (CHAWAKAMA) katika kuunganisha vijana wa Afrika Mashariki, tutaangalia kwa kina changamoto zinazokikabili chama hiki na mwisho ni wito kwa serikali za jumuia ya Afrika Mashariki katika kukiwezesha chama hiki ili kiweze kufikia malengo yake.
Chawakama ni Nini
CHAWAKAMA husimama badala ya Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili vyuo vikuu Afrika Mashariki. Chama hiki kilianzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kukuza na kueneza Kiswahili katika eneo lote la Afrika Mashariki kupitia wanafunzi wanaosoma Kiswahili vyuoni. Wanachama wa chama hiki ni wale wanosoma Kiswahili na hata wale wenye mapenzi ya lugha ya Kiswahili pia wanaweza kujiunga na chama hiki.
Kama nilivyokwisha sema hapo awali, chama hiki kina nafasi kubwa sana katika kuwaunganisha vijana wa Afrika Mashariki. Lengo kuu la chama hiki ni kueneza Kiswahili lakini sasa wanakienezaje? Wanachama wa chama hiki ambao ni nchi wanachama wa jumuia ya Afrika mashariki wanakawaida ya kuandaa makongamano kwa ngazi ya kitaifa na ngazi ya kimataifa. Kwa ngazi ya kitaifa kila nchi huandaa kongamano kila mwaka ambalo linawakutanisha wanachama wote kutoka vyuo mbalimbali katika nchi husika. Katika kongamano hilo mada mbalimbali zinazohusu lugha ya Kiswahili na mustakabali wake hujadiliwa lakini pia maazimio mbalimbali huchukuliwa juu ya maendeleo ya chama. Sasa katika mijadala kama hii inatoa nafasi ya Kiswahili kukua kwani makala mbalimbali huandikwa ambazo pia husomwa na watu mbalimbali. Makala hizi pia zimekuwa zikichapishwa katika majarida ya chuo husika na pia zimekua zikichapishwa mtandaoni ambapo hutoa fursa kubwa kwa watu wengi zaidi kuzifikia na kusoma, hivyo kwa njia hiyo Kiswahili kinakua kimeenea.
MWANACHAWAKAMA AKIWASILISHA MAKALA |
Kwa upande wa makongamano ya kimataifa, chama kimekuwa kikiandaa kongamano moja kila mwaka na kongamano hili linakua likizunguka katika nchi zote wanachama wa jumuia ya Afrika Mashariki. Sasa hapa ndipo panapatikana fursa ya kuwaunganisha vijana wengi wa Afrika Mashariki kutoka Kenya, Tanzania, Rwanda, Burundi na Uganda. Vijana hawa wanapokutana kinachowaunganisha ni lugha ya Kiswahili. Mawasiliano yote yanakuwa yakifanyika kwa lugha ya Kiswahili na kila mmoja anahamasika kutumia lugha ya Kiswahili kadri awezavyo na kila mtu huona fahari kuzungumza lugha ya Kiswahili.
Sasa kwa nini nasema chama hiki kinaweza kuwaunganisha vijana wa Afrika Mashariki. Kwanza kabisa kinachowaunganisha vijana hawa ni lugha ya Kiswahili, kupitia lugha ya Kiswahili kila mtu anakuwa na hisia za kuona kwamba anatoka katika familia moja, anahisi kwamba waafrika mashariki ni wamoja hii ni kwa sababu wanazungumza lugha moja. Na kwahiyo wakiisha jisikia hivyo ile hali ya umoja na mwingiliano inakuwa ni kubwa sana kitu ambacho kinaimarisha mahusiano baina ya vijana hawa wa Arfika mashariki.
Kitu kingine wanapokuwa wamekutana wote wanakuwa na malengo sawa – malengo ya kukienzi na kukieneza Kiswahili Afrika Mashariki nzima. Hili pia ni jambo ambalo huweka umoja baina ya vijana hawa, kwani ili kufikia lengo hili ni lazima wote wafanye kazi kwa pamoja na kwa umoja. Kwa kweli wamekua wakishirikiana kwa ukaribu sana na hata panapokuwa na uaandaaji wa makongamano vijana wote kutoka nchi zote wanachama wanashirikiana ili kufanikisha kongamano hilo. Pia watu wanaohudhuria kwenye makongamano ya CHAWAKAMA ni wengi kiasi cha kutosha. Kwa hiyo hawa vijana wanaporudi nchini mwao wanakuwa mabalozi wazuri wa lugha ya Kiswahili nchini mwao, kwa hiyo kwa kufanya hivyo vijana wengi watakua wamekielewa CHAWAKAMA vizuri na na hivyo watakuwa wameunganishwa na vijana wenzao wa Afrika mashariki.
GAVANA WA JIMBO LA NGOZI |
Kupitia CHAWAKAMA vijana wengi wamehamasishwa kuuthamini umoja wa Afrika mashariki na vijana pia wamekuwa na mwitikio mkubwa sana. Kwa mfano kongamano la mwaka jana (2012) lililofanyika Burundi lilitoa hamasa kubwa kwa vijana wa Burundi na hata taifa zima la Burundi juu ya dhana ya umoja wa jumuiya ya Afrika mashariki. Kabla ya hapo warundi wengi waliamini kuwa lugha ya Kiswahili, si lugha ya kistaarabu – ni lugha ya majambazi, wezi, lugha ya watu wajanjawajanja kwa hiyo sio lugha ya kujifunza na kuifahamu. Lakini baada ya CHAWAKAMA kufanya kongamano Burundi vijana wenyewe wa Burundi walikiri kuwa waliielewa vibaya lugha ya Kiswahili hii ni baada ya vijana wa CHAWAKAMA kushiriki katika shughuli za kijamii ambapo walisaidia kosomba mawe kwa ajili ya jengo la serikali katika ofisi ya Gavana wa jimbo la Ngozi. Gavana huyo alifurahishwa sana na kitendo cha wanaCHAWAKAMA na akaahidi ataaliita hilo jengo kwa jina la “Jengo la vijana wa Afrika Mashariki”. Kwa hiyo kitendo hiki pia kilijenga hisia za umoja ndani ya vijana hawa wa CHAWAKAMA lakini pia kiliacha mawazo mapya juu ya lugha ya Kiswahili, kwamba sio lugha ya majambazi, na watuwasio wastaarabu bali ni lugha ya watu wenye utu, heshima na watu wanaopenda umoja na ushirikiano.
WANACHAWAKAMA WAKIONESHA USHIRIKIANO |
Changamoto katika CHAWAKAMA
Kama tulivyokwisha ona hapo nyuma CHAWAKAMA ni chama kinachowahusisha wanafunzi. Kwa mazingira haya ni dhahri kwamba hata uwezo wa kujiendesha ni mdogo sana. Mapato yake hutekemea michango ya wanafunzi ambayo pia ni kazi sana kuipata, kwa hiyo chama hujikuta kinashindwa kufikia malengo yake kutokana na ukosefu wa pesa za kujiendesha. Na kwa hiyo hali hii inasababisha chama kuwa na maendeleo hafifu sana.
Jambo linguine ni kutotambulika kwa chama katika vyombo husika vya serikali. Kwa mfano hapa Tanzania, CHAWAKAMA hakitambuliki serikalini hii ina maana kwamba chama hakina usajili wa kudumu. Kwa kweli hii ni changamoto kubwa sana, hali hii inasababisha hata chama kinapowaendea watu wa serikalini kuomba misaada kwa ajili ya kufanikisha malengo fulani inakuwa ni vigumu sana kuipata kwani chama hakitambuliki serikalini. Chama kinaposajiliwa kinapata utambulisho rasmi serikalini na hii inakuwa rahisi kwa chama kuendesha shuguli zake ikiwa ni pamojana na kuandaa machangizo na pia kuomba msaada kutoka vyombo vya serikali vinavyohusika na kuweza kusikilizwa au hata kusaidiwa.
Sasa tunaweza kusema tatizo lipo wapi? Kwa nini chama hakijasajiliwa hadi sasa hivi? Mi nadhani viongozi wenye dhamana wa CHAWAKAMA hawajawa makini na suala hili, kusajili chama hakuhitaji pesa nyingi, ni pesa kidogo sana! Na usajili sio wa kuzunguka kiasi hicho, hata pesa za ada za wanachama zinatosha kwa usajili. Mi ningependa kuwashauri viongozi wa CHAWAKAMA Tanzania, kwamba lichukulieni kwa umakini suala hili, kwani chama kitakapotambulika serikalini hata mtakapokwenda kwenye kongamano katika nchi nyingine mtatambuliwa na balozi na pia atawatendeeni vema kwa kuwa mnaiwakilisha nchi huko. Kwa hiyo hakuna sababu ya kuendelea na changamoto hii, viongozi wakiwa makini chama kitapata usajili wake rasmi na hivyo kutambulika rasmi serikalini.
OFISI ZA GAVANA WA JIMBO LANGOZI |
Changamoto nyingine katika chama hiki, ni suala la kujitangaza. Chama hakijitangazi vya kutosha, watu wengi hawajui kama kuna uwepo wa CHAWAKAMA, vyombo vya habari vichache sana ndivyo vinajua kuwa kuna uwepo wa chama hiki na kujaribu kukitangaza. Achilia mbali vyombo vya habari mitandaoni nako chama hiki hakionekani, isipokuwa unapotafuta CHAWAKAMA mtandaoni utakutana na CHAWAKAMA-UDSM ambalo ni tawi tu la CHAWAKAMA lakini hutakutana na wavuti wa CHAWAKAMA kanda au Afrika mashariki. Hili pia ni tatizo, katika enzi hizi za TEHAMA sehemu nzuri na rahisi ya kukitangaza chama ni mtandaoni. Chama kinatakiwa kitengeneze wavuti ambao kwa kweli utasaidia kukitangaza chama, na katika wavuti huo wanaweza kuweka makala na taarifa mbalimbali za chama ambazo pia kwa kweli zitawavutia watu wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Pia kupitia huo mtandao watu wanaweza kujisajili na chama kwa urahisi. Kwa mfano, hivi sasa kuna chama cha ukuzaji Kiswahili duniani CHAUKIDU watu wanaweza kujisajili na chama hiki kupitia mtandaoni na hii inasaidia kusajili watu wengi kwa urahisi. Kwa hiyo wavuti ni kitu muhimu sana katika kukitangaza chama. Labda nitoe mfano wa CHAWAKAMA-UDSM, toka blogu hii ianzishwe kwa kweli watu wamekua wakiitembelea kwa wingi kutoka pande mbalimbali za dunia, na wengi wanaonekana kufurahishwa na taarifa mbalimbali zinazohusu CHAWAKAMA na makala zilizojapishwa mle zinazohusu Kiswahili ambazo kwa kweli ndio kivutio kikubwa kwa watu wengi wanaotembelea blogu hii. Kwa hiyo unaweza kuona jinsi mtando ulivyo muhimu katika kukitangaza chama.
Mwamko mdogo wa vijana wengi wanaosoma Kiswahili pia ni changamoto inayokikabili chama hiki katika kukua kwake. Tunaweza sema kuwa vijana wengi hawajawa na mwamko wa kutosha juu ya umuhimu wa lugha ya Kiswahili kama kiungo muhimu cha watu wa Afrika Mashariki.
Wengi wanadhani Kiswahili ni cha watu duni, watu wenye mitazamo iliyopitwa na wakati, kwa sababu hii hawaoni sababu ya kujishughulisha na na Kiswahili. Wao lugha ya kisasa ni lugha za kigeni hasa kiingereza, ukizungumza kiingereza au ukijishughulisha na lugha ya kiingereza ndio utaonekana msomi na kwamba uko makini na taaluma yako, lakini huyu anayejishughulisha na Kiswahili yeye anaonekana kama kakosa jambo la msingi la kufanya. Hali kama hii kwa kweli huwavunja vijana hawa moyo, lakini kwa upande mwingine pia hawatakiwi kuvunjika moyo kwa sababu wanajua kile wanachokifanya. Wao wanaelewa vizuri manufaa ya Kiswahili, na hawa wanojaribu kuwavunja moyo wanakua bado hawajaelewa kwa nini nyinyi mnajishughulisha na lugha ya Kiswahili. Kwa hiyo jambo la msingi ni kuwaelimisha na kuwaondo huo ujinga.
Sasa unaweza kujiuliza tutawaelimishaje watu wa namna hii? Makongamano na midahalo ifanyike kwa wingi sana. Makongamano yakifanyika kwa wingi sana, kile kinachozungumzwa kitakaa masikioni mwa watu kwa kujirudiarudia na hatimaye wataanza kuzinduka. Hii itawezekana endapo tu chama kitakuwa na uwezo wa kutosha kifedha. Uandaaji wa makongamano na midahalo huhitaji pesa.
Wito kwa serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki
WANACHAWAKAMA WAKIWAJIBIKA |
Vijana wa jumuiya ya Afrika mashariki wameamua kuuenzi utamaduni wao kwa vitendo, hamasa ya vijana hawa imekua na mvuto mkubwa sana kwa watu wengi. Hawakusukumwa na mtu yeyote lakini kwa kuona kuwa Kiswahili ni chombo muhimu sana cha kuweka watu wa jumuiya ya Afrika mashariki kwa pamoja ndio wakaamua kuunda chama hiki. Swali langu ni hili; ina maana viongozi wa Afrika mashariki kama kweli nia yao ni kuwa na jumuia ya Afrika mashariki yenye umoja hawaoni kwamba Kiswahili ni njia muhimu ya kutia hamasa kufikia lengo hilo? Watu wakiwa wanazungumza lugha moja wataona kwamba wao ni wa moja na hata itatia hamasa ya ushirikiano na hivyo lengo la Afrika mashariki yenye umoja litatimia. Kama kweli na wao wanaamini Kiswahili ni nyenzo muhimu ya kuwaunganisha wanajumuiya ya Afrika mashariki sioni kwa nini wanashindwa kuwekeza katika vikundi vinavyojaribu kutumia lugha ya Kiswahili kuwaunganisha wanajumuiya.
Lugha ya Kiswahili inatambulika rasmi katika katiba ya Kenya kama lugha ya taifa na katika rasimu ya katiba ya Tanzania ya 2013 Kiswahili kimetambuliwa sio kama lugha ya taifa tu bali pia tunu ya taifa. Kama tunu ya taifa ina maana kwamba ni hazina muhimu sana ya taifa letu ambayo kwa gharama yoyote ile taifa halitakubali kuipoteza. Na kama kweli serikali hizi zinataka Kiswahili kiendelee kuwa tunu na lugha ya taifa ni lazima kuwekeza katika lugha hii. Serikali zithamini mchango wa CHAWAKAMA katika kuendelza na kukuza lugha ya taifa na hivyo ziwe tayari kuwasaidia vijana hawa pindi wanapowaendea na pia ziweke jitihada za maksudi katika kuchangia maendeleo ya lugha ya Kiswahili.
No comments:
Post a Comment