Kabla hatujaanza kujadili mitazamo hii ni vema tukajua kwanza dhana ya sanaa, kwamba tunaposema sanaa tunamaanisha nini.
Sanaa ni uzuri unaojitokeza katika umbo lililosanifiwa, umbo ambalo mtu hulitumia kueleza hisi zinazomgusa kwa kutoa kielelezo au vielelezo vyenye dhana maalum. Kuna aina kuu tatu za sanaa. Kwanza ni sanaa ambazo uzuri wake hujitokeza katika umbo la kudumu, umbo ambalo linaweza kuhifadhiwa na uzuri wake kuonyeshwa wakati wowote. Hizi ni sanaa za uonyesho. Nazo ni kama vile uchoraji, uchongaji, ufinyanzi, kutarizi n.k. sanaa amabazo hututolea vitu kama vile picha, vinyago, nguo zilizotariziwa, vyungu n.k.
Aina ya pili ya sanaa ni sanaa za ghibu. Hizi ni sanaa ambazo uzuri wake haujitokezi kwenye umbo linaloonekana kwa macho au kushikika bali katika umbo linalogusa hisia. Mifano ni kama vile usahiri, uimbaji, upigaji muziki n.k. uzuri wa sanaa hizi umo katika kuzisikia.
Aina
ya tatu ya sanaa ni sanaa za vitendo.
Uzuri wa sanaa za aina hii umo katika umbo la vitendo, na ili kuupata uzuri huu
yampasa mtu kutazama vitendo vikifanyika. Umbo hili linalazimisha kuwepo kwa
mwanasanaa na mtazamaji wa sanaa mahali pamoja kwa wakati mmoja ama sivyo sanaa
haikamiliki. Hali hii ndiyo iliyosababisha sanaa hizi za vitendo kuitwa sanaa
za maonyesho, kwa sababu lazima wakati zinapotendeka awepo mtu wa kuonyeshwa,
maana uzuri wake umo katika vitendo vyenyewe.
Kwa
hiyo sanaa za maonyesho ni kitendo chochote chenye sifa nne ambazo ni:
i.
Dhana inayotendeka
ii.
Mtendaji
iii.
Uwanja wa kutendea
iv.
Watazamaji
Sasa
baada ya kuagalia dhana ya sanaa za maonyesho, sasa tuangalie nadharia
zinazojaribu kuelezea sanaa za maonyesho. Nadharia hizi zipo tatu ambazo ni:
Tukizingatia nadharia hii huenda
tukaamini kuwa sanaa za maonyesho ni tamthilia tu. Kitu ambacho kinaleta
mashaka kidogo. Inafahamika kuwa
tamthilia ni utanzu ulioletwa na wakoloni hapa Afrika Mashariki. Kwa hiyo,
kuamini nadharia hii ni sawa na kusema kuwa hakuna sanaa za maonyesho zenye
asili ya hapa Tanzania ama Afrika Mashariki. Au kwa upande mwingine ni sawa na
kusema kuwa kabla ya mkoloni kutuletea tamthilia sisi tulikuwa hatuna sanaa za
maonyesho zetu wenyewe. Wazo hili si kweli na ni wazo potofu. (Taz. Mhando &Balisidya 1976).
Kimsingi mtazamo huu unatokana na
fasili ya sanaa za maonyesho inayodai kuwa sanaa za maonyesho ni kitendo
chochote chenye sifa za mchezo, mchezaji, uwanja wa kuchezea na watazamaji.
Ingawaje ufafanuzi huu ni sawa lakini hata hivyo mtazamo huu ni dhaifu kwani
ulitokana na watu waliokuwa wakifafanua sanaa za maonyesho wakiegemea zaidi kwa
zile za utamaduni wa kizungu. Ufafanuzi huu haukuzifikiria sanaa za maonyesho zenye
ya utamaduni wa Kitanzania.
Dosari kubwa katika ufafanuzi huu
imo katika neno mchezo (play). Neno
hili lina maana duni likilinganishwa na hali na umuhimu wa sanaa za maonyesho
zenye asili ya Kitanzania/Kiafrika. Tukichukua kwa mfano unyago, jando, kusalia
mizimu, au masimulizi ya hadithi, ambayo ni mifano ya sanaa za maonyesho zenye
asili ya Kitanzania, tunakuta zile sifa zote nne zipo. Isipokuwa tunajua kuwa
shughuli zote hizi siyo mchezo na umuhimu wao hauruhusu hata kidogo kuingiza
neno mchezo. Shughuli hizi zina maana muhimu ambayo inahusu maisha ya binadamu
katika jamii yake. Ni shughuli zinazobeba wazo maalum lenye lengo la kujenga
utu wa mwanajamii. Basi vipi tuseme shughuli hizi zina sifa ya mchezo? Wenzetu wazungu wanaridhika na neno hili kwa sababu sanaa za maonyesho za utamaduni wao
mara nyingi zinafanywa kwa masihara tu. Sanaa za maonyesho zao zaidi ni kwa
madhumuni ya kujiburudisha au pengine kutafuta kipato. Lakini kila aina ya
sanaa za maonyesho ya Kitanzania ina dhana fulani ndani yake, kwa mfano dhana
kuhusu maana ya maisha, kuhusu utekelezaji wa madaraka ya kiutu uzima, kuhusu ushujaa, mafunzo ya historia ya jamii
n.k.
Kwa hiyo basi sanaa za maonyesho za
Kiafrika ni dhana zilizo kwenye umbo linalotendeka na siyo mchezo. Kutokana na utamaduni
wa Kiafrika tunaweza kusema kuwa: sanaa za maonyesho ni dhana inayotendeka. Na
ili dhana hii itendeke anahitajika mtu wa kuitenda (mtendaji). Mtendaji huyu
huhutaji uwanja wa kutendea hiyo dhana na wakati akiitenda wanakuwapo
watazamaji.
2. Sanaa za maonyesho ni vichekeso au ni maigizo yanayochekesha.
2. Sanaa za maonyesho ni vichekeso au ni maigizo yanayochekesha.
Wazo
hili linatokana na historia ya sanaa za Maonyesho hapa Tanzania. Wakati mkoloni
alipotuletea sanaa ya Maonyesho ya kikwao sisi tulishiriki katika tamthilia za
Shakespeare kama washiriki au watazamaji tu. Kwani tamthilia hizi hazikuwa na
maana yoyote kwetu kutokana na kuwa zilibeba na ziliongelea utamaduni wa
kizungu. Tulifurahishwa na vile vitendo vilivyofanywa kwenye jukwaa katika
tamthilia hizi na hivyo vitendo hivi vilituchekesha tu. Basi jambo kubwa kwa
Mwafrika ikawa ni vile vichekesho na hivyo kudhani kuwa jambo muhimu katika
tamthilia ni kule kuchekesha kwake.
3.
Sanaa
za maonyesho ni maigizo.
Wazo
hili limetokana na tafsiri mbovu ya neno play ambalo limetafsiriwa kuwa mchezo
wa kuigiza. Inawezekana aliyetafsiri neno hili alifuata nadharia za zamani sana
za drama, ambapo ilidhaniwa kuwa uigizaji (imitation)
ndio kiini cha drama. Hata hivyo nadharia hii ilitupiliwa mbali kwa vile
haikudhihirisha kiini hasa cha drama. Tafsiri hii ndiyo imeleta matatizo hapa
Tanzania katika kufahamu sanaa za maonyesho. Wengi wamepotoshwa na wazo kuwa
uigizaji ndio kiini cha sanaa za maonyesho kama vile neno michezo ya kuigiza
linavyoonyesha. Hivyo, hata katika kutazama sanaa za maonyesho za asili wengi
wamekuwa wakitazama iwapo kuna uigizaji. Na hapa wengi wanakwama kwani katika
unyago, jando, kusalia miungu n.k hakuna uigizaji bali wanaoshiriki wanashika
nafasi fulanifulani. Hivyo ni bora kutumia neno tamthilia pale tunaporejelea
neno plays.
Kwa
ujumla kuwepo kwa mitazamo hii huweza kuwa kumesababishwa na mambo yafuatayo:
- Wakoloni kutokutambua ama kwa makusudi ama kwa kutokuelewa kuwa tulikuwa na sanaa za maonyesho za kwetu, hivyo akatuletea drama kama vile anatuletea sanaa mpya ambayo aina yake haikuwepo hapa kwetu. Hivyo, mkazo wa sanaa za maonyesho ulitiliwa katika drama tu.
- Mkoloni alitumia mbinu mbalimbali za kufuta vitendo vyote ambavyo hasa ndiyo sanaa zetu za maonyesho. Mfano alitumia dini ya Kikiristo kupiga vita vitendo kama vile unyago, jando, kusalia mizimu n.k ambavyo viliitwa vya kishenzi.
- Tafsiri mbovu zinazofuata nadharia zilizopitwa na wakati kama ilivyoelezwa hapo awali.
Kwa
hiyo, tukisema sanaa za maonyesho, tunarejelea vitendo maalum vyenye sifa zilizotajwa
na kujadiliwa hapo awali. Hata hivyo tutambue kuwa sifa hizi ingawaje ziko sawa
lakini kimsingi zinatofautiana katika uzito wake baina ya jamii moja na
nyingine. Hatutazamii sanaa za maonyesho za Kihindi kuwa sawa kabisa na zile za
Kijapani au za Kiafrika. Ingawa zote ni sanaa za maonyesho zina misingi tofauti
kutokana na tofauti za utamaduni wa jamii husika.
10 comments:
Hongera kwa makala nzuri kuhusu sanaa za maonyesho.
Ooh, Asante sana Mwalimu!
asante sana...nilijifunza mengi
Nice for good explanations
Kazi nzr mwl
Ongeza zaidi maana ni nzuri kwa marejeo
maelezo mazuri sana kuhusu sanaa
Ubarikiwe sana
Vizur sana
Wataalamu waliotoa maana ya Sanaa za jadi ni wapi
Post a Comment