Friday, March 16, 2012

KISWAHILI NA UKALIMANI

Dunia inabadilika kila kukicha, sayansi na teknolojia huibuliwa kila kukicha, mambo haya yote huwaweka watu pamoja kutoka kila kona ya dunia, lakini pia watu hawa hawzungumzi lugha moja, wanahitaji kuwasiliana na ili mawasiliano yaweze kufanyika lazima kuwepo na lugha inayowaunganisha. Suala hili ni gumu kwa kuna lugha nyingi sana duniani na kila nchi inasera yake juu ya lugha lakini pia lazma watu wawasiliane na hapa ndipo tunaona umuhimu wa kuwepo mkalimani. 
Lugha ya kiswahili inakuwa kwa kasi sana, vyuo mbalimbali duniani hufundisha lugha hii adhimu kwa nini wewe usione fursa hii na uchukue hatua ya kujifunza ukalimmani ili ujiajiri katika soko kubwa kama hikli.
Kabla hujachukua uamuzi hebu jielimishe kidogo juu ya taaluma hii ya ukalimani.


Tafsri na ukalimani ni taaluma za lugha ambazo mara nyingi watu huchanganya wakidhani kuwa dhana hizi mbili hufanana lakini kimsingi kuna utofauti mkubwa kati ya tafsiri na ukalimani, elimu na ujuzi katka taaluma hizi hutofautiana. Kuna tofauti za msingi zinazotofautisha taaluma hizi, tutazichambua kwa kina katika sura zinazofuata. Kwa sasa tuangalie kwa kina dhana nzima ya ukalimani ambapo tutaangalia maana, aina za ukalimani, sifa za mkalimani (mambo ya kuzingatia katika ukalimani) na mwisho hitimisho.
Maana ya ukalimani.
Ukalimani wa lugha hulenga kurahisisha mawasiliano ya lugha ya mdomo au lugha ya alama kati ya watumiaji wa lugha mbili tofauti.
Kwa mujibu wa Encarta (2009) ukalimani ni tafsiri ya mdomo ya kile kinachosemwa katika lugha moja kwenda lugha nyingine ili kusudi wazungumzaji wa lugha tofauti waweze kuwasiliana.
Wikipedia wamefasili ukalimani kuwa ni uhawilishaji wa ujumbe katika lugha ya mazungumzo au lugha ya alama kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine.
Fasili zote hizi zinajaribu kutupa mwangaza hasa juu ya maana ya ukalimani, fasili ya kwanza inakasoro. Kutumia istilahi yenye maana tofauti na kile kinachojaribu kufasiliwa huleta mkanganyiko, istilahi tafsiri inamaana tofauti na ukalimani kwa hiyo sio sahihi kuitumia katika kufasili dhana ya ukalimani. Fasili ya pilli imejaribu kugusa mambo muhimu katika dhana ya ukalimani, kwamba ni uhawilishaji wa ujumbe katika lugha ya mazungumzo, kimsingi ukalimani hufanyika katika lugha ya mazungumzo.
Kwa hiyo kutokana na fasili hizi tunaweza kupata fasili ya jumla kwamba, ukalimani ni zoezi la uhawilishaji wa mawazo,ujumbe, maana katika lugha ya mazungumzo au lugha ya alama kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa.
Hivyo basi mkalimani ni mtu ambaye huhawilisha mawazo, maana au maelezo kutoka lugha chanzi na kuyaweka mawazo au maelezo au maana yenye maana inayolingana katika lugha lengwa, katika wakati halisi. Kazi ya mkalimani ni kufikisha kila kipengele cha kisemantiki (rejesta,toni) na kila lengo na hisia za ujumbe ambao mzungumzaji wa lugha chanzi amekusudia kufikisha katika wapokeaji wa lugha lengwa.
Aina za ukalimani.
Kuna aina tofautitofauti za ukalimani kulingana na vigezo tofautitofati vinavyotumika katika kuainisha aina za ukalimani. Kwa kutumia kigezo cha jinsi ukalimani unavyofanywa, tunapata aina kuu mbili:
Ukalimani mfululizo; katika ukalimani wa aina hii mzungumzaji wa lugha chanzi na mzungumzaji wa lugha lengwa huanza pamoja na kumaliza pamoja. Maranyingi vifaa maalum hutumika, mkalimani hukaa katika chumba chenye kidhibiti sauti akizungumza kupitia kipaza sauti wakati huo akimsikia na kumwona barabara mzungumzaji wa lugha chanzi kupitia visikizio. Wasikilizaji wa lugha lengwa hupata ujumbe kupitia visikizio. Vilevile ukalimani wa aina hii hutumiwa sana na wakalimani wa lugha ya alama.
Ukalimani fuatizi; katika aina hii ya ukalimani, mkalimani huzungumza baada ya mzungumzaji wa lugha chanzi kumaliza kuzungumza. Mkalimani anakua amesimama au amekaa sambamba na mzungumzaji wa lugha chanzi akiwa anasikiliza napengine kuandika maneno anayozungumza mzunguzaji wa lugha chanzi ili kumsaidia kukumbua pindi atakapoanza kukalimani. Wakati mzingumzaji wa lugha chanzi anapumzika au anamaliza kuongea ndiposa mkalimani anahawilisha kipande cha ujumbe au ujumbe mzima katika lugha lengwa.

Aina zingine za ukalimani.
Ukalimani wa kwenye mikutano; huu ni ukalimani unaofanyika wakati wa mikutano, huweza ukawa fuatizi au mfululizo, lakini kwa sababu ya mikutano inayokutanisha lugha nyingi, ukalimani fuatizi hautumiki. Katika ukalimani wa kwenye mikutano maranyingi mkalimani hufanya ukalimani kutoka lugha za kigeni kwenda lugha yake ya asili.
Ukalimani wa mahakamani; ukalimani wa aina hii hufanyika mahakamani, katika mabaraza ya kutolea hukumu na mahali popote pale ambapo masuala ya kisheria hufanyika, mfano katika kituo cha polisi hususani wakati wa kuchukua maelezo au katika ukumbi wa mikutano kwa ajili ya kuapishwa.
Ukalimani kiungo; ukalimani wa aina hii ni pale ambapo mkalimani humsaidia mtu au kikundi cha watu katika kutalii, matembezi au katika mkutano.
Ukalimani wa lugha ya alama; hii ni aina ya ukalimani ambao hufanyika kati ya lugha ya alama na lugha ya mazungumzo. Mzungumzaji anaweza kuongea mkalimani akahawilisha mawazo kwa njia ya alama, vilevile wakati mtu asiyesikia akifanya mawasiliano kwa lugha ya alama, mkalimani atahawilisha maana katika lugha ya mazungumzo. Vilevile ukalimani huweza kufanyika kati ya lugha ya alama na alama hii ni kwa sababu lugha ya alama hutofautiana kati ya nchi na nchi.
Ukalimani wa vyombo vya habari; kulingana na asili yake ukalimani wa vyombo vya habari hufanyika kwa ukalimani mfululizo. Hufanyika zaidi katika matangazo ya moja kwa moja ya televisheni au redio. Katika ukalimani wa vyombo vya habari vifaa kama  chumba cha kudhibiti sauti, kiwamba nakadhalika huhitajika sana.
Ukalimani wa simu; ukalimani wa aina hii humsaidia mkalimani kufanya ukalimani kupitia simu. Maranyingi hufanyika katika mazingira ambayo watu wanaohitaji kuwasiliana tayari wanakuwa wamekwishazungumza kupitia simu.
Ukalimani wa video; ukalimania wa aina hii hufanyika katika mazingira ambapo mmoja kati ya wanaowasiliana ni kiziwi au hasikii vizuri au hawezi kuongea (bubu). Katika mazingira kama haya ukalimani wa lugha ya alama hufanyika zaidi.
Ukalimani kulingana na muktadha; katika kundi hili kuna aina nyingi kulingana na jinsi itakavyojidhihirisha aktika miktadha tofautitofauti. Mfano, ukalimani wa kanisani, ukalimani wa msikitini, ukalimani wa mahakamani, jeshini nakadhalilka.
Ni matumaini ya ngu utakuwa umenufaika, unaweza pia kutoa maoni yako!.