Sunday, August 25, 2013

AINA ZA USHAIRI (BAHARI)




Bahari; hii ni aina mahususi ya  ushairi yenye sifa fulani kiumbo na pengine hata kimaudhui na kimatumizi na zinazoipambanua na aina nyingine ya ushairi.

S.A Kibao (2003)  anasema, ushairi wa Kiswahili umegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni: shairi, utenzi na ngonjeara. Anaendelea kusema, aina zote hizi kanuni zake ni za pamoja isipokuwa utenzi ambao una mpangilio wa namna ya pekee.

S. Robert na Amri Abeid (1954)  wanasema zipo bahari tatu tu za ushairi nazo ni:wimbo, shairi na utenzi.

A.S. Nabhany na wenzake wameainisha bahari 13 za ushairi na kusema kuwa utungo wowote lazima uingie katika bahari mojawapo. Bahari hizo ni hizi zifuatazo:
1.      Ushairi; Ni utenzi wenye mishororo minne na vipande  viwili kila msitari. Kila mstari una mizani 16 na kila kipande kina mizani 8. Maudhui yake yanatokana na jambo lolote lile analoliona mtunzi.

2.      Wimbo; Ni utungo wenye mishororo mitatu kila ubeti na kila mshororo una vipande viwili. Nyimbo nyingi huongelea mapenzi.

3.      Tenzi; Ni utungo wenye vipande vine katika kila ubeti na vina hubadilika kila ubeti isipokuwa kipande cha mwisho. Tenzi nyingi zina mizani nane kila mshororo na nyingine zina mizani 11 na zingine 10.

4.      Inkshafi/Duramandhuma; Imepata jina lake kutokana na utenzi wa Aliinkshafi. Tenzi hizi zina maadili ya kidini japokuwa maudhui yake yanaweza kutumika katika maadili ya kidunia. Kila ubeti una mishororo minne na kila mshororo una mizani 11.

5.      Ukawafi; Hili ni shairi lenye mishororo mitatu au zaidi katika kila ubeti na vipande vitatu katika kila mshororo. Mizani zinaweza zikatofautiana au zikawa sawa.

6.      Wajiwaji/Takhimisa; Una mishororo mitano kila ubeti na mizanai 15 kila mshororo na vipande vitatu katika kila mshororo vina muundo wa mizani 6, 4, 5. Maudhui yake ni ya kidini au kiamisha kwa ujumla, mfano Takhimisa ya Liongo  na tenzi ya Inkshafi.

7.      Hamziya; lipata jina lake kutokana na kaswida ya Hamziya ambao ni utenzi wa kiarabu. Mishororo ya Hamziya ina vipande 3 vya mizani 5, 4, 6

8.      Tiyani-Fatiha;   Ni ushairi wa kidini wa kuomba toba, una mishororo 9 kila ubeti ambayo huweza kutofautiana kwa urefu/mizani.

9.      Utumbuizo; Haina idadi kamili ya mishororo na mizani, urefu wa mstari au mshororo hutegemea pumzi aliyonayo mwimbaji na lengo lake; mfano ni nyimbo za Liyongo kuna tumbuizo.

10.  Wawe; Ni ushairi au wimbo wa kilimo, huimbwa wakati wa kulima au kupanda.

11.  Kimai; Inahusu shughuli za majini, ni bahari ya wavuvi na mabaharia. Idadi ya mishororo na vina si lazima.

12.  Zivindo; Ni ushairi unaofafanua maana za maneno; na kazi yake ni kujifunza lugha na mkuhifadhi lugha.
Mfano: Kata ni kata ya nyoka
             Au kata ya nyweleni
             Kata ya tweka, bandikwayo kichwani

13.  Sama; Neno ‘sama’ ni mahadhi au sauti, hivyo bahari hii hukusanya washairi wote wenye kufuata mahadhi ya kigeni.

Monday, August 19, 2013

NAFASI YA CHAWAKAMA KATIKA KUUNGANISHA VIJANA WA AFRIKA MASHARIKI

Utangulizi
Lugha ya Kiswahili ina historia ndefu hapa Afrika Mashariki kama chombo cha kuunganisha watu wenye tamaduni tofautitofauti tokea enzi za biashara ya utumwa hadi baada ya uhuru. Wafanya biashara wa enzi za utumwa walitumia lugha ya Kiswahili ili kurahisha mawasiliano na kukidhi haja zao za kibiashara, bila kujua, walijikuata wanakieneza Kiswahili kutoka pwani ya Tanganyika hadi bara ya Kongo. Wakoloni nao walipokuja Afrika Mashariki waliona Kiswahili ndio lugha pekee ya kurahisha utawala wao, lakini baadae walikuja kugundua kuwa Kiswahili ilikuwa ni silaha ya kuangamiza utawala wao na hivyo wakahafifisha matumizi ya Kiswahili.

Wanaharakati wa utaifa, wakati wa kupigania uhuru hususani katika nchi ya Tanganyika waliona Kiswahili ndio njia pekee itakayowasidia kupata uhuru bila hata kumwaga tone la damu. Mwalimu Nyerere alitumia fursa hii kuwaunganisha watanganyika wote wenye tamaduni tofautitofauti na waliokuwa wakizungumza lugha tofautitofauti, lakini kwa kupitia lugha ya Kiswahili walikuwa na kauli moja ya kutaka Tanganyika ya watanganyika huru. Umoja huu umedumu hadi leo Tanzania inajulikana kuwa ni nchi ya watu wakarimu na wenye umoja. Isingewezekeana kufukia hapa kama kila mtu angejitukuza kwa kabila lake ila kwa kutumia Kiswahili watanzania sasa ni wamoja, hakuna msamiati katika mazungumzo ya watanzania unaotukuza ukabila.