Thursday, April 18, 2013

MITAZAMO (NADHARIA) MBALIMBALI JUU YA SANAA ZA MAONYESHO


Kabla hatujaanza kujadili mitazamo hii ni vema tukajua kwanza dhana ya sanaa, kwamba tunaposema sanaa tunamaanisha nini.

Sanaa ni uzuri unaojitokeza katika umbo lililosanifiwa, umbo ambalo mtu hulitumia kueleza hisi zinazomgusa kwa kutoa kielelezo au vielelezo vyenye dhana maalum.  Kuna aina kuu tatu za sanaa. Kwanza ni sanaa ambazo uzuri wake hujitokeza katika umbo la kudumu, umbo ambalo linaweza kuhifadhiwa na uzuri wake kuonyeshwa wakati wowote. Hizi ni sanaa za uonyesho. Nazo ni kama vile uchoraji, uchongaji, ufinyanzi, kutarizi n.k. sanaa amabazo hututolea vitu kama vile picha, vinyago, nguo zilizotariziwa, vyungu n.k.

Aina ya pili ya sanaa ni sanaa za ghibu. Hizi ni sanaa ambazo uzuri wake haujitokezi kwenye umbo linaloonekana kwa macho au kushikika bali katika umbo linalogusa hisia. Mifano ni kama vile usahiri, uimbaji, upigaji muziki n.k. uzuri wa sanaa hizi umo katika kuzisikia.
Aina ya tatu ya sanaa ni sanaa za vitendo. Uzuri wa sanaa za aina hii umo katika umbo la vitendo, na ili kuupata uzuri huu yampasa mtu kutazama vitendo vikifanyika. Umbo hili linalazimisha kuwepo kwa mwanasanaa na mtazamaji wa sanaa mahali pamoja kwa wakati mmoja ama sivyo sanaa haikamiliki. Hali hii ndiyo iliyosababisha sanaa hizi za vitendo kuitwa sanaa za maonyesho, kwa sababu lazima wakati zinapotendeka awepo mtu wa kuonyeshwa, maana uzuri wake umo katika vitendo vyenyewe.